Mgawanyiko Mlimani: Hofu matukio ya 1992, 1997 yanajirudia
Na LUCAS BARASA
HOFU ya migawanyiko iliyopelekea Mlima Kenya kubaki kwenye upinzani katika uchaguzi wa 1992 na 1997 na kudumaa kimaendeleo imerejea katika eneo hilo.
Hii inafuatia shinikizo za baadhi ya viongozi kumpiga vita Naibu Rais Rigathi Gachagua na kutaka kubuniwa kwa chama cha mashinani ili kutetea maslahi ya Mlima Kenya.
Hatua ya Mlima Kenya kuwa na wagombeaji wawili maarufu-Ford-Asili Kenneth Matiba na Mwai Kibaki wa DP ilimwezesha Daniel Moi wa Kanu kuendelea kuwa mamlakani katika uchaguzi wa 1992.
Katika uchaguzi wa mwaka huo, Moi alipata 1,962,866 sawa na asilimia 36.35 ya kura zilizopigwa, huku Matiba akizoa kura 1,404,266 (asilimia 26).
Kibaki alipata kura 1,050,617 (asilimia 19.45) huku Jaramogi Oginga Odinga wa Ford-K akizpa kura 944,197 (asilimia 17.48).
Mnamo 1997, upinzani uligawanyika zaidi na kumwezesha Moi kushinda kwa asilimia 40.40 ya kura, akifuatiwa na Kibaki (asilimia 30.89), Raila Odinga (asilimia 10.79), Michael Kijana Wamalwa (asilimia 8.17) na Charity Ngilu (asilimia 7.89).
Mambo yalibadilika kwa Mlima Kenya wenyeji wengi walipomuunga Mwai Kibaki na kumpa ushindi mkubwa dhidi ya Uhuru Kenyatta wa Kanu mwaka wa 2002. Kibaki alirejea mamlakani katika uchaguzi uliokuwa na ushindani wa karibu wa 2007, akimshinda Raila Odinga kabla ya eneo hilo kuungana nyuma ya Uhuru 2013 na 2017.
Baada ya uchaguzi wa 1997, eneo lilionekana kujifunza makosa yake na kila mara lilipiga kura dhidi ya watu au masuala ambayo yalionekana kutaka kugawanya wakazi.
Eneo hilo lenye wingi wa kura hata hivyo linakabiliwa na msukosuko wa kisiasa huku kukiwa na dalili za migawanyiko kufuatia kuibuka kwa mirengo inayoshinikiza mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro kuchukua nafasi ya Bw Gachagua kama mgombea mwenza wa Ruto katika uchaguzi wa 2027.
Kundi hilo ambalo lilisitisha makabiliano ya kisiasa baada ya Rais Ruto kuingilia kati na kutaka kusitishwa kwa mjadala wa kumrithi, pia lilitaka Nyoro awe mpeperusha bendera wa urais wa Mlima Kenya mwaka wa 2032.
Mnamo Ijumaa, Bw Gachagua alijitokeza kuwanyamazisha wapinzani wake mbele ya Rais Ruto akisema eneo hilo limepata funzo kufuatia migawanyiko ambayo ililisukuma katika upinzani 1992 na 1997 baada ya kuteseka kwa miaka 24 ya utawala wa Moi.
Wakati huo, uchumi wa eneo hilo ulidorora kufuatia utendaji duni wa sekta ya kilimo.