Jamvi La Siasa

Mikakati ya Gachagua na Kalonzo kuivisha muungano 2025

Na BENSON MATHEKA January 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

LICHA ya kuonekana kutengwa na vigogo wakuu wa kisiasa nchini, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, wangali wanasuka muungano huku ikisubiriwa kuona iwapo watahimili mawimbi makali ya kisiasa ukuruba wa Rais william Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ukidumu.

Ingawa Gachagua na Musyoka wanaonekana kutengwa, duru zinasema kambi zao zinaendelea na mipango ya kusuka muungano wa kukabili Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027 ambaye hali ya kisiasa ikidumu ilivyo nchini, atakuwa na mrengo wa wazito wa kisiasa Raila Odinga, Uhuru Kenyatta na washirika wao.

Dkt Ruto anaonekana kupata uungwaji mkono na aliyekuwa kiongozi wa Mungiki Maina Njenga ambaye mkesha wa mwaka mpya alimuonya naibu rais huyo wa pili kujiandaa kwa makabiliano makali kuelekea 2027.

Bw Njenga alitaja jina la Uhuru akisema wataungana dhidi ya Bw Gachagua mlimani japo haikubainika iwapo alikuwa na baraka za rais huyo mstaafu.

Njenga ataja jina la Uhuru

Kulingana na wadadisi, lengo la Rais Ruto kuvuta Kenyatta na Njenga upande wake ni kujaribu kuokoa kura za Mlima Kenya baada yake kutofautiana na Gachagua.

Duru zinasema Gachagua na Musyoka wanapanga muungano uliofumwa kama chama kikuu cha upinzani ambao utajumuisha kiongozi wa Chama cha DAP-K Eugene Wamalwa na viongozi wengine wa Azimio ambao wametofautiana na Raila.

Mshirika wa mmoja wao ambaye aliomba tusimtaje jina kwa sababu za kibinafsi alisema wawili hao wameunda kamati ya kiufundi ya watu wanne kila upande kushughulikia mipango ya muungano wao mwaka huu.

“Hii ya kutengwa haiwashtui kwa kuwa wanaamini wako na wapigakura tofauti na tabaka la wanasiasa ambao wameungana kuunga serikali inayobebesha raia mateso ikiwemo ushuru na kuwanyima utawala wa sheria kwa kuwateka nyara wakosoaji na kuwatokomeza,” akasema.

Inasemekana kila upande unawakilishwa na wanachama wanne katika kamati ya awali ya kiufundi ikiunganisha pamoja mpango wa ushirikiano ambao utaunda mfumo mkubwa wa kisiasa kwa uchaguzi wa 2027.

Wadadisi wa siasa wanasema muungano wa wawili hao na wanasiasa wengine wa kimaeneo, unaweza kufaulu tu iwapo hisia za raia dhidi ya serikali zitadumu hadi 2027.

“Kwa ubabe wa kisiasa na kifedha, wamepungua na kinachoweza kuwapiga jeki ni hisia za raia ambao wameonyesha chuki dhidi ya serikali,” akasema mdadisi wa siasa Faith Abuka.

Gachagua na Kenyatta

Anasema muungano wao unaweza kupata nguvu iwapo juhudi za chini ya maji za kupatanisa Gachagua na Kenyatta zitafua dafu kabla ya 2027.Wawili hao wanajipanga huku ushirikiano wa Bw Odinga na Rais Ruto ukionekana kuimarika siku baada ya siku na kuungwa mkono na viongozi wa kanda.

Mnamo Alhamisi, Dkt Ruto na Bw Odinga waliungana na Rais wa Uganda Yoweri Museveni katika kilele cha tamasha za kusherehekea utamaduni wa Waluo kaunti ya Siaya.

Mbali na washirika wakuu wa Bw Odinga kuteuliwa serikalini, wabunge na baadhi ya maafisa wa chama akiwemo mwenyekiti wa ODM Glady’s Wanga na kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa wametangaza kuwa wataunga Rais Ruto 2027.

Washirika wa Bw Kenyatta akiwemo Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni ambao wamekuwa wakionekana kuunga Bw Musyoka wamekuwa wakimshambulia vikali Bw Gachagua.

Mnamo Alhamisi, Bw Kioni alimkemea vikali Gachagua kwa kile alichotaja kama kuchukulia mzaha suala zito la utekaji nyara wa vijana hasa kwa kuahidi kufichua wanaohusika na kukataa kufanya hivyo.

Hii ilikuwa mara ya pili kwa mbunge huyo wa zamani wa Ndaragua na mshirika wa Bw Kenyatta katika Jubilee kumsuta Bw Gachagua.

Mwaka jana akiwa katika hafla moja Embu ambayo Bw Musyoka alihudhuria, Bw Kioni alimshambulia Gachagua kwa kudai eneo la Mlima Kenya lina deni la kisiasa la kulipa makamu rais wa zamani Kalonzo Musyoka.

Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka na mwenzake wa DAP-Kenya (Kushoto), Eugene Wamalwa. PICHA|HISANI

Mnamo Jumatano, Bw Kioni aliungana na Bw Musyoka, kiongozi huyo wa Wiper alipotoa hotuba ya kukaribisha mwaka na kisha baadaye akatoa taarifa tofauti kwa niaba ya chama cha Jubilee ambayo alikemea serikali ya Kenya Kwanza kwa kukolea kwa ufisadi na utepetevu kiasi cha kutoweza kukombolewa.

Kabla ya krismasi, Bw Musyoka na Bw Kenyatta walihudhuria harusi ya binti ya aliyekuwa waziri Fred Matiang’i ambayo wadadisi walisema ilitoa kidokezo cha kisiasa kwa kuwa viongozi wa serikali hawakuwepo.

Bw Matiang’i anasemekana kuwa na azma ya urais sawa na Bw Musyoka.Pia inasemekana kuna msukumo mkubwa wa kutaka Gachagua apatanishwe na Uhuru kabla ya uchaguzi wa 2027.