Mipango ya Gachagua kupata chama yaiva, asubiriwa kutoa tangazo
ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua ameanza kujenga nyumba yake ya kisiasa huku akijipanga kwa uchaguzi mkuu wa 2027 ambao hana uhakika atagombea kufuatia kutimuliwa kwake na Bunge la Kitaifa mwaka jana.
Huku akitarajiwa kutoa tangazo ambalo anasema litapatia eneo la Mlima Kenya dira ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, na ikiwa wazi kuwa hatakiwi katika chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA), Bw Gachagua yu mbioni kuunda chama kuleta pamoja wakazi wa eneo hilo.
Kwa muda wa wiki kadhaa, amekuwa akikutana na washirika na washauri wake katika nyumba yake kijijini Wamunyoro, Mathira kaunti ya Nyeri kuweka mikakati ya kisiasa inayohusisha kubuni au kupata chama cha kisiasa na kukivumisha kubomoa umaarufu wa UDA na Jubilee cha aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta katika eneo la Mlima Kenya.
Bw Kenyatta ambaye chama chake ni cha pili kwa ukubwa Mlima Kenya alichangamkia serikali ya Rais William Ruto baada ya Bw Gachagua kutimuliwa ofisini na wadhifa wa naibu rais ukakabidhiwa Prof Kithure Kindiki.
Kumekuwa na majaribio ya kuzima umaarufu wa mbunge huyo wa zamani wa Mathira kwa kuvuruga mikutano yake ambayo wachambuzi wa siasa wanasema yanasaidia kumjenga mashinani.
Mnamo Ijumaa, Bw Gachagua aliashiria kuwa mipango yake kuwa na chama cha kisiasa imeiva.
“Leo nimeshinda na timu ya watakaokuwa watu mashuhuri ya viongozi waliochaguliwa tukazungumza na kubadilishana mawazo na maoni. Timu hii inayojulikana kama ‘Sauti Ya Mwananchi’ na ndio kwa sasa sauti ya pekee inayozungumza kwa niaba ya watu wa Kenya siku hizi. Nilipowasikiliza, inaonekana mbele iko sawa,” Bw Gachagua alisema kupitia taarifa.
BW Gachagua amekuwa akisisitiza kuwa eneo la Mlima Kenya halitawahi kuingia katika makubaliano ya kisiasa bila chama akisema alipata funzo kwa kumwamini Rais William Ruto kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.
“Hatutawahi kucheza kamari na kura zetu tena,” Gachagua alisema mwezi Desemba.
Duru zinasema Bw Gachagua analenga kuwa na chama kitakachokuwa na ushawishi mkubwa katika eneo la Mlima Kenya ambacho hata kama hataruhusiwa kugombea wadhifa wowote kufuatia kutimuliwa kwake, atakitumia kushawishi siasa za kitaifa.
Kwa sasa anasubiri uamuzi katika kesi aliyowasilisha kulalamikia mchakato wa kumtimua.
Huku akionekana kutengwa na vigogo wengine kisiasa za kitaifa, Bw Gachagua ameanzisha ukuruba na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa DAP- Kenya Eugene Wamalwa.
Seneta wa Makueni Dan Maanzo ameonekana kuhakikisha kuwa muungano wa Wiper na Gachagua umeiva.
“Wiper itaunda muungano na Rigathi Gachagua. Tutaunda muungano mkubwa, ambao utapata asilimia 50+1 ya kura katika raundi ya kwanza,” alisema akizungumza kwenye Citizen TV.
Duru zinasema washirika wa Bw Gachagua wamekuwa mbioni kupata chama cha kisiasa huku wakipanga vita dhidi ya Rais William Ruto.
Aliyekuwa Mbunge wa Thika Mjini Wainaina Jungle majuzi aliashiria kuwa mipango ya Gachagua kuwa na chama imeiva kwa kusema naibu rais huyo wa pili wa Kenya na washirika wake hawatapigia magoti chama cha UDA.
“Walipoamua kumfukuza Naibu Rais Gachagua, walidhani tungeporomoka … badala yake, Gachagua amekita mizizi na tayari ni vuguvugu ambalo kila mtu anataka kuwa sehemu yake,” alisema.
Inafahamika kuwa timu ya Gachagua ina uhakika kwamba haitakiwi katika chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) na Rais Ruto anasubiri tu wakati mwafaka ili kuwatimua.
“Gachagua amesema mara kwa mara kwamba atatoa tangazo kupatia Mlima Kenya mwelekeo wa kisiasa na japo kumekuwa na majaribio kadhaa ya kumzima atafanya hivyo hivi karibuni na siasa za ukanda huu zitabadilika pakubwa,” alisema mbunge mmoja kutoka Kiambu ambaye aliomba tusitaje jina kwa kuwa angali UDA.