Jamvi La Siasa

Mizimu ya kuvunja ANC yamwandama Mudavadi wanasiasa wakijipanga kwa 2027

Na BARNABAS BII, JUSTUS OCHIENG January 1st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

UAMUZI wa kuvunja Chama cha Amani National Congress (ANC) huenda ulimhakikishia Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi nafasi ndani ya serikali, lakini umeibua upya maswali magumu kuhusu mustakabali wake wa kisiasa.

Katika maeneo mengi ya Magharibi mwa Kenya, hatua hiyo inatafsiriwa kama kujisalimisha kwa Rais William Ruto na chama chake cha United Democratic Alliance (UDA).

Lakini huku shinikizo za kuwasilisha mgombea urais kutoka eneo la Magharibi mwaka wa 2027 zinavyozidi, mizimu ya ANC imeanza kumwandama Bw Mudavadi.

Mizimu hiyo sasa inaonekana kudhoofisha msimamo wake nyumbani, kupunguza uwezo wake wa kujadiliana kitaifa na kuibua mashaka mapya kuhusu ndoto yake ya muda mrefu ya urais.

Kwa mara ya kwanza baada ya miongo kadhaa, Bw Mudavadi anajikuta akishiriki siasa bila chama anachomiliki au kudhibiti, akiwa mgeni ndani ya UDA inayomilikiwa na Rais Ruto.

Wanasiasa kadhaa kutoka Magharibi mwa Kenya wanasema ANC haikuwa chama cha kawaida, bali kilijengwa kwa uangalifu kuvumisha Bw Mudavadi kama kiongozi anayependa mageuzi na mwenye uwezo wa kuleta maridhiano, aliye na mizizi mizito eneo hilo.

“Kukivunja kulimaanisha kusalimisha chama hicho cha kisiasa na kujiunga na chama kikubwa chenye utamaduni na ngazi zake,” anasema wakili na mchambuzi wa siasa Chris Omore. Ndani ya UDA, anasema, wanachama wa zamani wa ANC wanaweza kuonekana bila sauti ya mamlaka.

Ndani ya UDA iliyojaa vigogo, Bw Mudavadi sasa anashindania ushawishi, uteuzi na nafasi ya kimkakati. Nguvu ya kuwa na chama humwezesha kiongozi kujadiliana, kudai marupurupu au hata kutishia kujiondoa. Kwa kuvunja ANC, Bw Mudavadi alijivua nguvu hiyo.

Ingawa alipata wadhifa mkubwa wa Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni, washirika wake wabunge, wanaotaka kugombea wanahangaika kupata nafasi ndani ya UDA.

Wengi waliingizwa kama manaibu bila majukumu muhimu.

Kwa mfano, Gavana wa Lamu Issa Timamy, aliyekuwa Naibu Kiongozi wa ANC, alimezwa na UDA kama Naibu Kiongozi wa Pili.

Bw Omboko Milemba, aliyekuwa Katibu Mkuu wa ANC, akawa Naibu Katibu Mkuu wa UDA; huku Kelvin Lunani, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitaifa wa ANC, akishushwa hadi Naibu Mwenyekiti—ishara ya kupoteza ushawishi.

Athari kubwa zaidi zimeonekana mashinani. ANC ilikuwa imejenga uaminifu sehemu za Magharibi mwa Kenya. Kumezwa na UDA kuliwachanganya wafuasi; wengine walihamia DAP-K, Ford Kenya na ODM.

Mnamo Jumanne katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Lugari Cyrus Jirongo, viongozi wa Waluhya walimshambulia Bw Mudavadi wakimlaumu kwa kusaliti jamii.

Mbunge wa Bumula Jack Wamboka, alisema viongozi walio serikalini wanajinufaisha binafsi huku jamii ikisalia pembeni, akisisitiza kuwa 2027 watawasilisha mgombea urais wao.

Kiongozi wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa, Mbunge wa Saboti Caleb Amisi na Seneta wa Kakamega Boni Khalwale, waliunga mkono wito wa umoja na kumkosoa Bw Mudavadi kwa kuvunja ANC.

Wakati huo huo, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alionya dhidi ya kuua roho ya demokrasia ya vyama vingi, kauli iliyochukuliwa kama kukosoa kuvunjwa kwa ANC.

Bw Mudavadi alimjibu kwa kusema Jubilee yenyewe ilizaliwa kupitia kuungana kwa vyama.

Alisisitiza kuwa siasa za miungano ndizo mustakabali wa Kenya, akisema hakuna chama kinachoweza kushinda peke yake.

Hata hivyo, wachambuzi wanasema kuvunjwa kwa ANC ni upanga wenye makali mawili, mamlaka ya muda mfupi na sintofahamu ya muda mrefu.