Jamvi La Siasa

Mjadala wa ugavi wa mapato wafufua ubabe baina ya Rigathi na Kindiki

June 15th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

MJADALA kuhusu ugavi wa mapato ya kitaifa kwa misingi ya wingi wa watu sasa unaonekana kufufua vita vya ubabe kati ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na Waziri wa Usalama Kithure Kindiki.

Kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 Bw Gachagua, wakati huo akiwa Mbunge wa Mathira na Profesa Kindiki, wakati huo akiwa Seneta wa Tharaka Nithi, walikabana koo waking’ang’ania nafasi ya kuwa mgombea mwenza wa Rais William Ruto.

Huku Bw Gachagua akiunga mkono mfumo huo unaojulikana kama “mtu-mmoja, kura-moja, shilingi-moja” Profesa Kindiki ameupinga akisema utatenga baadhi ya maeneo nchini kimaendeleo.

“Siwezi kuhusishwa na mpango unaolenga kugawa na kubagua maeneo fulani ya nchi hii… ndiposa nasimamia mfumo wa bendera moja, taifa moja,” Waziri huyo wa usalama akaeleza.

Kulingana na Prof Kindiki, wale wanaounga mkono mfumo huo wa “mtu mmoja, kura moja, shilingi-moja” hawaelewi madhara yake kwa mustabali wa taifa la Kenya “haswa maeneo ya nchi wanayotaka yafaidi kutokana mfumo huo.”

Lakini akijibu, Bw Gachagua anashikilia kuwa “hatutajalishwa na wale wanaoupinga mfumo huo kwani hata wakati ambapo tulikuwa tukipambana na wakoloni walikuwepo wasaliti kama hao.”

Juzi, Rais Ruto alioenekana kumwonya naibu wake dhidi ya kutumia maneno ya lugha ya Kikuyu kama vile “tukunia, ngati, komerera na kunda ngutume” kuashiria wasaliti akisema yanaweza kupanda mbegu za ukabila nchini.

“Maneno haya ya matusi pia ndio chanzo cha uhasama kati ya Gachagua na baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya.

Kwa hivyo, koma kutumia misamiati kama hii,” Dkt Ruto akasema alipotubu wiki jana katika kongamano la dhehebu la Akorino mjini Nakuru.

Mhadhiri wa chuo kikuu Profesa Macharia Munene akasema hivi: “Vita katika serikali hii havihusu sera na maoni bali uhasama wa zamani unaochipuza miongoni mwa viongozi.”

Anasema hali hiyo inaharibu sura ya serikali na kuikosea heshima afisi ya Naibu Rais.

Kufikia sasa msimamo wa Prof Kindiki kuhusu suala hilo la mfumo wa ugavi wa mapato unaungwa mkono na mwenyekiti wa baraza la washauri wa kiuchumi wa Rais Ruto Dkt David Ndii na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wa.

Nao msimamo wa Bw Gachagua unaungwa mkono na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba na aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Kike Laikipia Catherine Waruguru.

Lakini mjadala huo, sasa unaonekana kujijenga kama ajenda ya kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Hii ni baada ya kuchipuza kwa madai kuwa huenda Rais Ruto akateua mtu mwingine kuwa mgombeaji mwenza wake na kumtema Bw Gachagua.

Itakumbukwa kwamba wakati wa upigaji kura kubaini anayefaa kuwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto, Bw Gachagua alipata kura tatu huku Prof Kindiki akiibuka mshindi kwa kupata kura 27.

Wapigakura walikuwa wabunge kutoka eneo la Mlima Kenya. Hata hivyo, hatimaye Dkt Ruto alimteua Bw Gachagua kuwa mgombea mwenza wake.

“Bw Gachagua ambaye hatimaye aliteuliwa na Ruto kuwa mgombea mwenza wake alipata kura tatu na Prof Kindiki aliibuka mshindi kwa kuzoa jumla ya kura 27,” Gavana wa zamani wa Kiambu, Bw William Kabogo aliyekuwepo katika makazi ya Naibu Rais Karen, Nairobi wakati huo, akaambia Taifa Leo.