Jamvi La Siasa

Mkakati butu wa Suluhu kusaka maridhiano TZ

Na BENSON MATHEKA November 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ya kuhimiza vyama vya upinzani kuungana na kuonyesha mshikamano wa kitaifa inaonekana kuwa mkakati butu wa kisiasa huku akiendeleza ukandamizaji wa wapinzani wake wakuu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Bunge la 13 mnamo Ijumaa, Novemba 14, 2025, Rais Samia aliwataka viongozi wa vyama vyote vya siasa kutafakari makosa yaliyofanywa awali, kuyarekebisha, na kusonga mbele kwa mshikamano kwa ajili ya amani na utulivu wa taifa.
“Kwa hivyo basi, naomba makundi yote ya Watanzania, hasa vyama vya siasa, tuangalie tumekosea wapi, turekebishe, tuendelee na safari yetu ya taifa lenye amani na utulivu,” alisema.
Kauli hii imetajwa kama mkakati butu wa kisiasa unaolenga kurekebisha makosa yaliyofanywa katika uchaguzi uliopita badala ya kutambua changamoto zinazokabili mfumo wa uchaguzi, na kuanzisha mageuzi kuimarisha imani ya wananchi katika demokrasia.
Wachambuzi wa siasa wanasema Rais Suluhu anajaribu mkakati wa kumfanya atambuliwe na jamii ya kimataifa baada ya uchaguzi uliokubwa na ghasia na ambao ulikosolewa na makundi ya kimataifa ya waangalizi.
“Huu ni wito butu wa maridhiano. Hauwezi kuomba maridhiano huku ukizuilia mpinzani wako mkuu kwa sababu ya kutumia haki zake. Kiongozi wa Chadema, Tundu Lissu angali anakabiliwa na kesi ya uhaini na hivyo wito wa Suluhu ni butu,” asema mchambuzi wa siasa James Wakahiu.
Anasema hatua ya Rais Samia kuondoa mashtaka dhidi ya vijana walioshiriki maandamano ya Oktoba 29, 2025 haitoshi kuhalalisha uchaguzi uliotajwa kuwa usiotimiza misingi ya demokrasia na makundi ya waangalizi wa kimataifa wakiwemo wa Muungano wa Afrika.
“Sambamba na mambo mengine, katika hotuba yangu ya kulifungua Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimevielekeza vyombo vya sheria hasa Ofisi Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuwafutia makosa vijana na watoto wetu ambao kwa kutojua, walifanya makosa kwa kufuata mkumbo Oktoba 29 mwaka huu. Nikiwa Mama na Mlezi, ninawasihi vijana wote kuendelea kulinda amani na mshikamano wa nchi yetu, na hata siku moja msikubali kushawishiwa kuichoma nchi yenu wenyewe,” Suluhu alisema.
Rais Suluhu alionekana kulenga kutuliza vijana wa Tanzania ambao walizua ghasia wakiandamana wakati na basda ya uchaguzi huku ikisemekana polisi waliwaua wengi.
“Mimi na wenzangu serikalini tumefikiria kuwa na wizara kamili itakayoshughulikia masuala ya vijana. Tumeamua kuwa na wizara kamili badala ya kuwa na idara ya vijana ndani ya wizara yenye mambo mengi. Pia ninawaza kuwa na mshauri wa masuala ya vijana ndani ya ofisi yangu ya rais,” aliongeza bila kifafanua hatua za kuleta mageuzi ya uchaguzi na demokrasia katika nchi hiyo
Wachambuzi wanasema mkakati wa Rais Samia unalenga kupunguza migogoro na kuleta mshikamano wa kitaifa. Hata hivyo, bila nia na hatua madhubuti za kuleta mageuzi wito wake unabaki kuwa butu.
“ Hawezi kulenga kutuliza vijana bila kutatua kilichowafanya kuandamana na kuzua ghasia ambacho ni mfumo wa uchaguzi usio wa haki na kukadamiza wapinzani.
Kwa maoni ya gu anapalilia shida badala ya kutafuta maridhiano ya dhati,” asema Wakahiu. Anasema kilichotokea Tanzania ni matokeo ya mfumo usio wazi unaohitaji mageuzi makubwa na sio kauli za uhu mwema anavyofanya Rais Suluhu.