Jamvi La Siasa

Mpango wa Ruto ‘kuleta Singapore’ ni ujanja wa kujitafutia kura, Upinzani wasema

Na LABAAN SHABAAN December 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MPANGO wa Serikali wa kuchochea uchumi wa nchi kupitia Hazina za Ustawishaji Miundomsingi umekumbwa na pingamizi, wakosoaji wakishuku unanuiwa kuwa mbinu ya kuwinda kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Mpango huo sasa umetajwa na Upinzani kuwa mkakati wa kampeni za Rais William Ruto kujipigia debe achaguliwe kwa Muhula wa Pili.

Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro anasema huu si wakati wa kutoa ahadi bali kutekeleza manifesto ya 2022.

Wachambuzi wa kisiasa nao wanasema kuwa Kenya haiwezi kuendelea zaidi iwapo matatizo ya kimsingi hayajatatuliwa yakiwemo gharama ya maisha, uboreshaji sekta ya afya na elimu.

Tangu Rais William Ruto atoe hotuba kuhusu Hali ya Taifa katika Bunge Novemba 20, 2025, ngoma ya kustawisha uchumi wa Kenya kufikia Mataifa Yaliyostawi kama Singapore imezidi kurindima.

Lakini viongozi wa Upinzani wamekuwa wakimkaba koo Rais Ruto kwa ajenda hii wakisema ni ahadi hewa kwa wananchi wanaotaabika kwa gharama ya juu ya maisha.

“Hili jambo tunalosikia kuhusu Hazina ya Ustawishaji Miundomsingi na gumzo kuhusu Singapore ni maandalizi ya uzinduzi wa kampeni za 2027. Tumekuwa hapa na tushawahi kusikia vitu kama hivi awali,” anasema Bw Nyoro.

Anashikilia kwamba sababu pekee ya serikali kuchaguliwa ni kutimiza ahadi ilizotoa wakati wa kampeni, si kutoa ahadi mpya ilhali zile zilizotolewa bado hazijatimizwa.

“Serikali ina jukumu la kueleza Wakenya inachofanya sasa, si kuwaambia inachopanga kufanya,” akasema mbunge huyo wa Kiharu.

Hata hivyo, Serikali ya Kenya Kwanza inasukuma hazina ya Sh5 trilioni ya ujenzi wa miundomsingi kwa angalau miaka kumi ijayo.

Ni mpango alioutangaza Rais Ruto bungeni wiki nne zilizopita akishangiliwa na wabunge.

“Laiti kungekuwa na wabunge wengi zaidi wanaokosoa serikali. Lakini mnavyojua, bunge hili si la kidemokrasia kama ambavyo tungependa. Natumai labda kadri muda unavyosonga tutapata watu (wabunge) zaidi wa kuzungumzia jambo hili kwa sababu ni muhimu,” akasema Bw Nyoro akikashifu wabunge wanaounga baadhi ya sera za serikali bila kukosoa.

Mtaalamu wa masuala ya kisiasa Martin Andati anakubaliana na Bw Nyoro kwa kiwango fulani lakini anahisi mbunge huyo anapinga serikali kwa sababu alivuliwa Uenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Ugavi katika Bunge la Kitaifa.

Huku mpango wa serikali ukionekana wa kuvutia, wakosoaji wanaibua hofu kuhusu utumizi wa rasilimali za nchi na usimamizi wa mashirika ya serikali.

“Ninachoshuku ni kwamba huenda kuna njama ya kutwaa fedha za malipo ya uzeeni. Walio uongozini wanatafuta mbinu za kuchota pesa za NSSF na kujaribu kuziweka kwenye muundomsingi,” anasema Bw Andati.

Anashauri kuwa ili Kenya istawi, lazima kwanza sekta za elimu, afya, kilimo miongoni mwa nyingine ziimarishwe pamoja na serikali tawala kufuata nyayo za marais wa awali kama Marehemu Mwai Kibaki.

“Rais angemalizia utekelezaji wa Ruwaza 2030 kwa sababu inaeleza bayana kabisa kinachohitajika kufanywa kustawisha Kenya,” asema Bw Andati.

Rais pia anapewa changamoto kukabili zimwi la ufisadi uliokithiri katika sekta ya umma na kupunguza mikopo inayofyonza bajeti ya nchi.