Msimu wa kujipanga mwandani wa tatu wa Ruto akiondoka serikalini
KUJIUZULU kwa Naibu Mkuu wa Wafanyakazi katika Afisi ya Rais, Eliud Owalo mnamo Jumapili kumeongeza idadi ya wanasiasa wanaomtoroka Rais William Ruto, maswali yakiibuka kuhusu makusudi yao hasa ya kujiondoa.
Bw Owalo aliyekuwa anahudumu katika Afisi ya Rais akihusika na ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya serikali kuhakikisha ajenda ya maendeleo ya serikali inatimia, alisema lengo lake la kujiuzulu ni kujiandaa kuwania urais mwaka wa 2027.
Anajiunga na waziri wa zamani wa Utumishi wa Umma, Moses Kuria na mwanasiasa Peter Mbae ambao walijiuzulu ghafla mwaka jana.
Mnamo Julai 8 mwaka jana, Bw Kuria alijiuzulu kama mshauri wa masuala ya kiuchumi wa Rais Ruto.
Alikuwa amehudumu miezi 11 kama waziri wa Biashara na Uwekezaji na miezi tisa kama waziri wa Utumishi wa Umma kisha miezi 10 kama mshauri wa masuala ya kiuchumi wa Rais Ruto.
Naye Bw Mbae alijiuzulu mnamo Januari 13, 2025 kama mkuu wa ufanikishaji na utekelezaji wa mipango ya serikali, jukumu lililopewa Bw Owalo baadaye.
Alilalamikia mazingira magumu ya kutekeleza wajibu wake akiashiria kulikuwa na tofauti kali kati yake na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei.
Bw Mbae kwa sasa yuko katika kambi ya aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ambako anahudumu kama mshauri wa masuala ya kiuchumi na mipango.
Bw Owalo na Kuria hawakurejeshwa serikalini baada ya maandamano ya Gen-Z ya Juni 2024.
Akizungumza Jumapili alipojiuzulu, Bw Owalo alisema kuwa atakuwa anazunguka maeneo mbalimbali kupiga kampeni kali ya kusaka uongozi wa nchi.
“Kwa zaidi ya miaka 15 na zaidi nimefanya kazi kwa bidii kwa wanasiasa binafsi nchini. Uamuzi wangu umesukumwa na niliyojifunza na baada ya kushauriana na wadau mbalimbali ikiwemo kanisa langu la Nomiya. Nitawania urais mnamo 2027,” akasema Bw Owalo.
Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo ambaye pia ni Kiranja wa Wachache alikejeli hatua ya Bw Owalo husu kuhusu kuwania urais akisema huo ni mzaha huenda.
“Hiyo ni ndoto ya mchana. Hawezi kuupata urais bali analenga tu kuwafumba Wakenya macho. Hasa nia yake iko kwenye ugavana au ubunge,” akasema Bi Millie.
Bw Owalo akiendea ugavana basi atamenyana na James Orengo ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya ODM 2022.
Akiamua kuwania ubunge, atakuwa analenga kumfurusha Otiende Amollo ambaye amehudumu kama mbunge wa Rarieda tangu 2017.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Mark Bichachi naye anasema Bw Owalo analenga tu kusalia hai kisiasa baada ya kupoteza uwaziri.
“Hawezi kutumia UDA na pengine aanzishe chama chake cha kisiasa. Kazi aliyokuwa akifanya pia haikuwa ikihusika na umma moja kwa moja kwa hivyo hii ni mbinu yake ya kusalia vinywani mwa Wakenya badala ya kutokomea kisiasa,” akasema Bw Bichachi.
Baada ya Bw Kuria kujiuzulu, madai yalitanda kuwa alikuwa akitumiwa na serikali kumpiga vita aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ambaye amejizolea ufuasi mkubwa Mlima Kenya.
Jana kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio, Bw Gachagua aliwaambia wakazi wa Mlima Kenya wajiepushe na Bw Kuria akidai ni ‘mradi’ wa Rais Ruto anayetaka kuvuruga kura za upinzani eneo hilo.
Kwenye uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini mnamo Novemba 27, mwaka jana, Bw Kuria kupitia Chama cha Kazi (CCK) alimsimamisha Duncan Mbui ambaye mwanzoni alikuwa akilenga kiti cha chama cha DP.
Bw Mbui aliibuka wa tatu akijizolea kura 2,804, idadi ambayo upinzani ungekuwa nayo katika kapu lake, basi ingekuwa vigumu kwa Leo Muthende wa UDA kuwahi ushindi.
Mnamo Januari 4 mwaka huu, Bw Kuria alimwambia Bw Gachagua athubutu kutembelea Gatundu Kusini iwapo yeye ni mwanamume.
Aidha, mbunge huyo wa zamani wa Gatundu Kusini alimkashifu Bw Gachagua akidai alichangia kuondolewa kwake katika Baraza la Mawaziri na pia kuhamishwa kwake kutoka wizara ya Biashara hadi ile ya Utumishi wa Umma.
“Bw Gachagua wewe ni mwoga na mtu hatari. Kuanzia leo, jiandae kwa vita vikali kwa sababu umevuka mpaka,” Bw Kuria akasema akikashifu kisa cha kuhangaishwa kwa Mwakilishi wa Kike wa Lamu Muthoni Marubu kwenye hafla moja za mazishi Kaunti ya Murang’a.