• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:56 PM
Muhoozi Kainerugaba: Je, Museveni anasimika familia kwa uongozi wa taifa?

Muhoozi Kainerugaba: Je, Museveni anasimika familia kwa uongozi wa taifa?

NA WANDERI KAMAU

JE, Rais Yoweri Museveni wa Uganda anapanga kuendeleza udhibiti wa familia yake katika uongozi wa taifa hilo?

Mnamo Alhamisi wiki iliyopita, Bw Museveni alitangaza kumteua mwanawe, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kuwa Mkuu wa Majeshi (CDF) mpya.

Muhoozi alichukua nafasi ya Jenerali Wilson Mbasu Mbadi, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Biashara, kufuatia mabadiliko ya baraza la mawaziri yaliyotangazwa na kiongozi huyo.

Kabla ya uteuzi wake, Muhoozi alikuwa akihudumu kama mshauri wa babake kuhusu operesheni maalum.

Uteuzi huo ulijiri siku chache baada ya kiongozi huyo kuliongeza jeshi nguvu za kiutawala.

Kwenye teuzi hizo mpya, Rais Museveni alimteua Luteni Jenerali Samuel Okiding kuwa Naibu Mkuu wa Majeshi. Alichukua nafasi ya Jenerali Peter Elwelu, ambaye Rais Museveni alimteua kama mmoja wa washauri wake wakuu.

Kutokana uteuzi huo mpya, wadadisi wanasema kuwa ni wazi kwamba Rais Museveni anajitayarisha kung’atuka uongozini, japo kwa kuhakikisha familia yake bado inaendelea kudhibiti siasa na uongozi wa taifa hilo.

Pia, wanasema hatua ya Rais Museveni kuliongeza nguvu jeshi mara tu baada ya kumkweza Muhoozi, inaonyesha kiongozi huyo “anajitayarisha kumwachia mwanawe uongozi japo bila kusema”.

“Kilicho wazi ni kuwa Rais Museveni anajitayarisha kung’atuka uongozini, japo kwa kuhakikisha familia yake inaendelea kushikilia uongozi wa taifa hilo kupitia mwanawe, Muhoozi,” asema Bw Kirwok Koech, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za kimataifa.

Kulingana na mdadisi huyo, mwelekeo anaochukua Museveni unaachilia dalili za kiongozi ambaye hayuko tayari kuacha uongozi wa taifa hilo mikononi mwa mtu mwingine, isipokuwa familia yake.

“Miaka ya Rais Museveni imesonga na ni wazi ameanza kuhisi kwamba wakati umefika amwachie mtu mwingine uongozi. Hata hivyo, anahisi kutokuwa salama kisiasa kutoacha uongozi kwa mtu ambaye hamwamini au huenda akamgeuka kisiasa,” akasema Bw Kirwok.

Hatua ya Bw Museveni, hata hivyo, imekosolewa na baadhi ya wadadisi na wanaharakati wa kisiasa, wakionya kuwa huenda Bw Museveni akawasha moto wa maasi ya kisiasa, kama baadhi ya nchi katika ukanda wa Afrika Magharibi.

Kulingana na Prof Tom Mboya, ambaye ni mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Maseno, huenda hatua hiyo ikazua maasi dhidi ya Bw Museveni, kwa “kuujenga upinzani bila kujuia” ikiwa hatatahadhari.

Baadhi ya viongozi maarufu wa upinzani nchini humo ni mwanamuziki Bobi Wine (Robert Kyagulanyi), Kizza Besigye kati ya wengine.

“Lazima Bw Museveni atahadhari; kwa kuhakikisha hakutazuka maasi yoyote dhidi ya utawala wake ambayo huenda yakageuka kuwa uungwaji mkono dhidi ya upinzani,” akasema Prof Mboya.

Anasema kiongozi huyo anafaa kujifunza na michakato ya uchaguzi katika baadhi ya mataifa kama Kenya, Senegal, Botswana kati ya mengine, ambako marais waliopo huwa wanang’atuka uongozini mihula yao inapokamilika.

  • Tags

You can share this post!

Tshisekedi na Kagame wakubali kukutana kujadili amani...

Serikali sasa yaahidi kusaidia familia za waliokufa...

T L