Jamvi La Siasa

Mulembe wakasirikia Musalia, Weta kwa kukosa kuwaunganisha maeneo mengine yakijipanga

Na KEVIN CHERUIYOT May 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wakuu wa jamii ya Waluhya wamekashifiwa kwa kukataa kuungana na kutoa mwelekeo mmoja kuhusu siasa za 2027, wanajamii wakisema hii itasababisha uungwaji mkono wao usithaminiwe na mirengo tofauti ya kisiasa nchini.

Kwenye mkutano ulioandaliwa ugani Bukhungu, Kibra mnamo Jumapili, cheche kali zilitawala huku Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangúla wakikashifiwa kwa kushindwa kuhakikisha umoja wa jamii hiyo licha ya kuwa na nyadhifa kubwa serikalini.

Pia waliohudhuria walishikwa na ghadhabu kali baada ya Mabw Mudavadi na Wetangúla kukosa mkutano huo ambao ulishirikisha Waluhya wanaoishi kwenye maeneobunge yote 17 ya Kaunti ya Nairobi.

Wengine ambao walielekezewa cheche kali kwa kukosa mkutano huo licha ya kualikwa ni Waziri wa Biashara Wycliffe Oparanya, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.

Mbunge wa Makadara George Aladwa alisema ni wazi kuwa jamii hiyo haizungumzi kwa sauti moja kutokana na ubabe wa kisiasa kati ya viongozi wake wakuu.

“2027 haipo mbali na viongozi wetu lazima waungane na kutupa mwelekeo. Jamii nyingine zimeungana na juzi uliona jinsi ambavyo Abagusii wameungana nyuma ya Dkt Fred Matiang’ nasi tunastahili kuungana ili tutumie idadi yetu kuamua mustakabali wa kisiasa nchini,” akasema Bw Aladwa akishangiliwa na umati uliohudhuria mkutano.

“Iwapo viongozi wetu wamekataa kuungana, basi tutaandaa mkutano wetu kivyetu na kutangaza mwelekeo wetu bila kuwashirikisha,” akaongeza.

Bw Aladwa ambaye ni mwenyekiti wa ODM Kaunti ya Nairobi aliongeza kuwa mikutano yao na nia yao ya kutaka jamii iungane haifai kufasiriwa kama ya kikabila.

“Hatuwezi kukaa na kusubiri jamii nyingine ziungane. Tumeanza safari hiyo hapa Bukhungu kwa sababu umoja wetu una umuhimu mkondo wa siasa za taifa unapoamuliwa,” akasema Bw Aladwa.

Wakati wa mkutano huo, viongozi wote waliokwepo walikubaliana kuongoza wanajamii wajisajili kama wapigakura kwa wingi ili wadumishe nyadhifa wanazoshikilia Nairobi ikiwemo kiti cha ugavana.

Pia walimtaka Bw Sakaja aanze kuandaa mikutano ya mara kwa mara ili aweke mikakati jinsi ambavyo atatetea wadhifa wake huku akishauriana na jamii nyingine.

Bw Sakaja aliwakilishwa kwenye mkutano huo na Afisa Mkuu wa Michezo Oscar Igaida na mwenzake wa uchumi dijitali David Sande Oyolo. Wawili hao walisema mikakati inastahili kuwekwa ili jamii hiyo ipata zaidi ya viti 35 vya wadi na wabunge wanane jijini Nairobi.

Wakati ambap Mabw Mudavadi, Wetangúla na Oparanya wapo serikalini, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya naye amekuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali Jumuishi kupitia vuguvugu lake la Tawe.

Pia waliohudhuria mkutano ugani Bukhungu walimtaka Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini Francis Atwoli ashauriane na viongozi wote kisha atoe mwelekeo wa kisiasa watakaoufuata 2027.