Jamvi La Siasa

Ngunjiri ahepa Gachagua, arudi kwa Uhuru

Na MWANGI MUIRURI May 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu amehama mrengo wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kurejea katika Chama cha Jubilee, akisema kwa sasa si rahisi kumbwaga Rais William Ruto mnamo 2027.

Bw Wambugu aliondoka Jubilee na kuwa mshirika wa Bw Gachagua baada ya uchaguzi mkuu wa 2022 lakini sasa amerejea katika chama hicho kinachoongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Mbunge huyo wa zamani amesema haungi mkono wito wa Bw Gachagua wa kuundwa kwa chama cha watu wa Mlima Kenya na kusema kuwa ghadhabu dhidi ya utawala wa Rais Ruto sasa zimepungua ikilinganishwa na mwaka jana.

“Watu wanaendelea kupona kutoka kwa ghadhabu ambazo walikuwa nazo Bw Gachagua alipotimuliwa mamlakani. Sasa hata waliomwondoa Gachagua wanahutubia mikutano bila tafrani ikilinganishwa na hapo awali ambapo walikuwa wakizomewa,” akasema Bw Wambugu.

“Siwezi kuunga mkono kuundwa kwa chama kimoja cha kieneo kwa sababu huo ni udikteta na mimi nasimamia haki na ukweli. Siwezi kubadili tabia na msimamo wangu kwa sababu Kenya ni taifa ambalo linazingatia demokrasia,” akaongeza.

Alilinganisha ghadhabu dhidi ya utawala Rais Ruto na zile zilizomwaandama Rais Mwai Kibaki (sasa marehemu) mnamo 2005 na hata mrengo wake ukashindwa kwenye kura ya maamuzi.

Vivyo hivyo, alisema kuwa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta ulikumbana na hasira za raia miaka miwili baada ya kuingia mamlakani.

Licha ya visiki hivyo, wawili hao walifanikiwa kumaliza muhula wao wa uongozi ambao ulichukua miaka 10.

“Nafahamu watu ndani ya serikali ambao hawalali wakitaka serikali hii iwe na umaarufu. Kuna wale ambao wanasahishisha makosa yao na hata baadhi wakisema Rais atahudumu muhula moja, kwa sasa hiyo ni ngumu sana,” akasema

Mbunge huyo wa zamani alisema kuwa iwapo Rais Ruto atahudumu kwa muhula moja basi atakayechukua nafasi yake pia hatachaguliwa tena kwa sababu ghadhabu dhidi ya serikali na matarajio ya raia si mambo ya kuyeyuka au kupuuzwa tu na utawala wowote ule.

Kutokana na jinsi Rais Ruto alivyojikakamua wakati wa kampeni na kushinda uchaguzi mkuu mnamo 2022 licha ya kutoungwa na serikali, Bw Ngunjiri alisema itakuwa vigumu sana kumshinda na kwa sasa anaendelea kuchapa kazi ili kuonyesha matunda ya kazi yake.

Mwanasiasa huyo aliweka wazi kuwa alikuwa kwenye kambi ya Bw Gachagua kuanzia Juni 2023 kumsaidia katika kitengo cha mawasiliano na baada ya kufurushwa kwake na bunge, basi kazi yake iliisha ndiposa sasa anajipanga upya kisiasa.

Alishangaa kwa nini kambi ya Bw Gachagua sasa inamwelekezea matusi ilhali yeye alichapa kazi na hata kumwezesha kuanzisha wito wa kuunganisha Mlima Kenya.

Bw Wambugu aliwakumbusha wanaompiga vita kutoka kwa mrengo wa Bw Gachagua kuwa aliwahi kufanya kazi na Raila Odinga, kwa sasa yupo mrengo wa Uhuru Kenyatta na hawajui kuwa siku zinazokuja azma ya kisiasa inaweza kuwaunganisha tena.

Hasa alikanusha vikali kauli ya Bw Gachagua kuwa vyama vingine vidogo Mlima Kenya ni wilbaro za Rais Ruto, akisema matamshi hayo ni madharau na yanakiuka hitaji la kidemokrasia ya kila mtu kuunga mkono chama anachokitaka.

Mbunge huyo aliwakumbusha wakazi wa Mlima Kenya kuwa wasipofanya hesabu zao vyema hata kiti cha naibu rais kinachoshikiliwa na Profesa Kithure Kindiki huenda wakapokonywa 2027 iwapo wataendelea kupinga utawala wa Kenya Kwanza.