Nitatoboa yote kuhusu Ruto, aapa Gachagua
Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amethubutu serikali ya Rais William Ruto kumkamata, akisisitiza kuwa hana hatia na kuwa haogopi kuhojiwa kuhusu matamshi aliyotoa akiwa Amerika.
Bw Gachagua, ambaye aliondolewa mamlakani mwezi Oktoba 2024 baada ya kutofautiana na Rais Ruto, alisema yuko tayari kutoa ushahidi wa tuhuma nzito alizotaja kuhusu utawala wa Ruto.
“Nilieleza kila mtu niliyekutana naye kuwa hii ni nchi yenye fursa nyingi lakini inazama kutokana na utawala wa mabavu wa Rais Ruto. Nilisema shida si Kenya, shida ni Ruto. Huo ni uongo upi? Hilo ni kosa gani?” aliuliza.
Alipuuzilia mbali wito wa Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, kwamba akaandikishe taarifa kufuatia matamshi hayo, akisema hana cha kuomba msamaha.
Bw Gachagua alirudia madai kwamba yuko tayari kutoa ushahidi mbele ya Bunge la Amerika, kufuatia pendekezo la mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Kigeni ya Seneti ya Amerika kutathmini hadhi ya Kenya kama mshirika mkuu wa nchi hiyo asiye mwanachama wa NATO.
Pendekezo hilo litachunguza sera za kidiplomasia za Kenya, hususan uhusiano wake na China, Urusi, Iran, na makundi hatari ya kigaidi Afrika Mashariki.
“Tunataka maelezo kuhusu uhusiano wa kisiasa na kifedha kati ya viongozi wa Kenya na mataifa kama China, Urusi, na Iran,” pendekezo la kamati linasema, na kuongeza kuwa matumizi mabaya ya misaada ya usalama ya Amerika yatachunguzwa pia.
Bw Gachagua alisema yuko tayari “kushirikiana na yeyote anayetambua umuhimu wa kufichua Kenya kama kitovu hatari kwa usalama wa dunia.”
“Wakati Bunge la Amerika lilitaka kujua ikiwa Nairobi inawateka nyara na kuwaua watoto, kushirikiana na waasi nchini Sudan, au kushirikiana na magaidi, nilijibu kuwa kama mtu aliyekuwa serikalini, nina taarifa za ndani zinazoweza kusaidia kufichua ukweli. Nilisema niko tayari kushirikiana kikamilifu na uchunguzi wowote halali na wa kuaminika, kutoka kwa yeyote.”
Aliongeza kuwa “nia hiyo ya kusaidia kufichua uhusiano wa utawala wa Rais Ruto na vtisho vya usalama wa ndani na nje huenda ilimkera Bw Murkomen, ambaye sasa anadhani nilikuwa tayari kuandika taarifa kwake binafsi.”
Gachagua alisisitiza kuwa wito wa kuandikisha taarifa unapaswa kuwa maalum kutoa ushahidi dhidi ya Rais Ruto na washirika wake wa karibu ambao alidai tayari wanachunguzwa na Amerika.
“Wito wowote unaotolewa nje ya kiwango hicho ni kelele ninazodharau… na kama wanadhani wanaweza kunilazimisha kushirikiana nao kwa nguvu, basi wanajua makazi yangu yote. Wanajua mahali pa kunipata,” alisema.
Sasa, kiongozi huyo wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) anatumia redio za lugha za mama na mitandao ya kijamii kufikisha ujumbe wake kwa wafuasi wake, baada ya mikutano yake ya hadhara kuzimwa mara kadhaa.
Akizungumza kwenye redio ya Kameme FM, alimlaumu Bw Murkomen kwa ‘kutumia sarakasi’ badala ya kushughulikia masuala ya usalama wa taifa.
Gachagua ameahidi kuongoza kampeni ya kuhakikisha Rais Ruto atahudumu kwa muhula mmoja tu.
“Sasa tukijiondoa kutoka kwa Ruto, wanaanza kutuita wabaguzi na wakabila. Tulikuwa wazalendo tulipompigia kura, lakini tunaitwa wabaguzi tunapomkataa? Kama huo ndio ubaguzi, basi tunajivunia,” alisema.
Kuhusu kung’atuliwa kwake, Gachagua alisema: “Leo naona kufurushwa kwangu kama baraka. Nilihisi Mungu amenisahau, lakini leo najua alinitendea wema. Nafasi yangu sasa ni kubwa zaidi ya ile ya Naibu Rais.”
Aliuliza kwa kejeli: “Ni nani alidhani kuwa Gachagua angekuwa na nguvu kitaifa na tumaini kwa wengi wanaojaribu kuishi chini ya utawala huu wa dhuluma? Kama ningalikuwa bado Naibu Rais, ningekuwa nikiwambia nini kuhusu fedheha hii ya utawala wa Ruto?”
Aliongeza kuwa hawezi kukubali wito wa Rais Ruto kwamba upinzani utoe mipango mbadala.
“Unawezaje kutarajia tuahidi wananchi kuwa tutawateka nyara, kuwaua, au kuwatoza ushuru kupita kiasi vizuri zaidi? Hapana. Ahadi pekee tunayoweza kutoa ni kumuondoa Ruto 2027 ili kuanza kusafisha nchi,” alisema.
Kwa sasa, anasema lengo lake kuu ni kuandaa chama chake cha DCP kwa chaguzi ndogo 24 zijazo.
‘Nimejikita kupanga DCP kushiriki katika chaguzi hizi, hasa ule wa ubunge Mbeere Kaskazini. Eneo hilo ni muhimu sana kwa ajenda yetu kama chama. Ufanisi wetu katika chaguzi nyingine pia utakuwa msingi wa mipango yetu ya 2027,’ alisema, akirejelea kiti kilichoachwa wazi kufuatia uteuzi wa Geoffrey Ruku kujiunga na Baraza la Mawaziri.
Alipuuza dhana kwamba upinzani uliingia baridi alipokuwa nje ya nchi.
‘Tutakutana kama viongozi wa upinzani kutathmini tulipo sasa. Kisha tutafuatilia malengo yetu ya pamoja kama timu. Sisi ni kikosi cha vinara walio na vipaji tofauti. Siasa si tu kuonekana hadharani, mambo mengi hufanyika nyuma ya pazia,’ alisema Bw Gachagua.
Kuhusu kuvurugwa kwa mikutano yake na kuwekewa vikwazo na serikali, Gachagua alitoa onyo kali.
“Mtu yeyote ndani ya serikali hii anayefikiri kuwa wafuasi wangu wataendelea kuvumilia vitisho, mateso na kuwekewa vizingiti vya kisiasa bila kuchukua hatua, anafaa kufikiri upya.”