Jamvi La Siasa

ODM inavyojichimbia kaburi lake kisiasa

Na BENSON MATHEKA August 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM), ambacho kwa muda mrefu kimekuwa nembo ya mapambano ya kisiasa na utetezi wa haki za wananchi, sasa kinaonekana kupoteza dira yake.

Dalili za kulegea kwa misingi yake ya awali zimekuwa zikiongezeka kwa kasi, huku mgawanyiko wa ndani, kauli zinazokinzana za viongozi wake wakuu, na mwelekeo usioeleweka kisiasa vinatikisa chama hiki.

Mshikamano wa kihistoria uliokuwepo katika ngome ya Nyanza umeanza kudidimia. Hali ambayo zamani ilikuwa ya uaminifu usiopingwa kwa Raila Odinga sasa imejaa suitafahamu.

Wachanganuzi wa siasa wanasema mgawanyiko unaoonekana kati ya viongozi wa Nyanza ya Kati na Kusini unathibitisha kuwa ODM haiko salama tena ndani ya ngome yake.

Kaunti za Migori na Homa Bay, ambazo bado zinaonekana kuonyesha utiifu kwa Raila, kwa sasa zinaunga mkono ushirikiano wa ODM na UDA kwa kiwango cha kushangaza.Lakini si wafuasi wote wanasherehekea mwelekeo huu mpya.

Wapo walioanza kuona ushirikiano huu kama usaliti kwa misingi ya mageuzi, demokrasia na upinzani wa kweli. Hali hiyo inajitokeza wazi katika Nyanza ya Kati, ambapo viongozi kama Profesa Tom Ojienda na Dkt Oburu Oginga wamejibwaga kwa fujo kwenye kampeni ya kuhalalisha mkataba wa ODM–UDA.

Kauli zao kali na mitazamo ya mashambulizi haijawashawishi wengi mashinani, bali imezidi kuwagawanya wafuasi. Katika Kaunti ya Busia, kimya kilichotanda kimezua maswali mengi.

Je, wafuasi wa ODM katika kaunti hiyo wanatafakari au tayari wameanza kujiondoa kwa hatua?Katika hali ya kisiasa ambapo ujumbe na mkakati vinahitaji kusawazishwa kwa makini, ODM imeangukia kwenye mtego wa kutoeleweka.

Mshikamano wa viongozi wake uko hatarini, na kile ambacho kilikuwa chama cha watu sasa kinatishiwa kuwa chama cha makubaliano ya kisiasa ya juu bila ridhaa ya mashinani.

Katika maoni aliyochapisha katika jarida moja la mtandaoni wiki hii, mhadhiri wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Alupe, Dkt Chebii Kiprono alisema “ODM inasahau kwamba nguvu yake haikuwa tu kwa sababu ya Raila Odinga, bali kwa sababu ilionekana kama sauti ya wananchi waliotengwa. Sasa inashirikiana na serikali ambayo wananchi hao walihisi inawanyanyasa.”

Ushirikiano wa ODM na UDA

Ushirikiano wa ODM na Rais William Ruto unazua maswali mengi ya kiitikadi. Kwa wafuasi wengi wa ODM, Ruto ni alama ya siasa walizopinga kwa muda mrefu: ukosefu wa usawa wa kijamii, uongozi wa mabavu, na utawala wa kibepari.

Kile kinachofanya mambo kuwa mabaya zaidi kwa ODM ni kuwa hata umaarufu wa Rais Ruto umeanza kushuka. Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za hivi karibuni, wananchi wengi hawaridhishwi na hali ya kiuchumi, gharama ya maisha, na ukosefu wa mabadiliko, haki za binadamu na utawala wa sheria walivyoahidiwa.

“Kushirikiana na kiongozi ambaye umaarufu wake unaporomoka ni hatari ya kisiasa. Badala ya kupata faida ya muungano huo, ODM inaonekana kujichimbia kaburi kwa mikono yake,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.

Ndani ya chama, sauti za upinzani zimeanza kuzimwa. Edwin Sifuna, Katibu Mkuu wa ODM, ambaye hapo awali alikuwa na msimamo mkali wa kisera, sasa anaonekana kulemewa na presha ya chama.

Wapiganiaji wa mageuzi wa zamani kama James Orengo na Peter Anyang Nyong’o wanaonekana kupoteza mwelekeo, huku wakitoa kauli zinazokinzana kuhusu mwelekeo wa ODM.

“Inaonekana wawili hao wanataka tu kuokoa kazi zao lakini kwa ndani wanaumia kwa kuona chama kikiacha misingi yake ya awali,” asema Dkt Gichuki.

Katika hali hii, ODM inapoteza si tu mwelekeo wake wa kisera, bali pia imani ya mashinani. Wafuasi waliokuwa tayari kujitolea, kushiriki maandamano, au kupiga kura kwa hisia, sasa wanajikuta wakitazama kwa mashaka.

Dkt Kiprono anasema katika maoni yake kwamba historia ya vyama vingine vya kisiasa nchini inaonyesha wazi kuwa chama kinapopoteza sauti yake na kuwa sehemu ya miungano ya mamlaka isiyoeleweka, basi huporomoka kwa kasi. FORD, NDP, na hata KANU zimepitia mkondo huo huo

“Siasa za Kenya hazina uvumilivu kwa vyama visivyo na msimamo. Mara tu wafuasi mashinani wanapohisi kusalitiwa, hujiondoa kimyakimya na ni vigumu sana kuwarudisha,” asema.

Kulingana naye, kwa sasa, ODM ina nafasi ya kujitathmini kujirekebisha na kurejesha imani ya wafuasi kote nchini.

“Lakini muda unayoyoma. Na kama chama hicho hakitaamka mapema, historia huenda ikakiandika kama chama kilichojivunjia heshima na nguvu, si kwa sababu ya kushindwa katika uchaguzi, bali kwa sababu kilikosa kushikilia msingi wake,” asema.