ODM yanusa ‘uvundo wa serikali’, yatishia kujitenga kura ya 2027
CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kinaonekana kunusa uvundo wa serikali ya Kenya Kwanza ambayo kinaunga mkono kwa kujitenga na wanachama wake wanaoitetea.
Licha ya wanachama wake kutwaa nyadhifa za juu serikali za mawaziri na washauri wa rais, na baadhi ya maafisa na viongozi wake kutangaza wazi wataunga Rais William Ruto kwa muhula wa pili mwaka wa 2027, chama hicho sasa kimejitenga na matamshi yao huku mgawanyiko ukionekana kudhihirika.
Katika taarifa kutoka kwa Kamati Kuu ya Usimamizi inayoongozwa na kaimu kiongozi wa chama, Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o, chama hicho kilionya kuwa ODM bado ni chama imara na kinalenga kuingia mamlakani 2027.’
“ODM inasalia kuwa chama imara cha kisiasa kushindana na vingine vyote ili kutwaa mamlaka kwa njia za kidemokrasia,” Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alisema katika taarifa baada ya mkutano huo.
Hatua hii inajiri baada ya Seneta wa Kisumu Tom Ojienda kusema kuwa ODM itashirikiana na United Democratic Alliance (UDA) katika uchaguzi ujao.
Mwenyekiti wa chama hicho Glady’s Wanga na Kiongozi wa Wachache Junet Mohamed pamoja na wanachama wa ODM katika Baraza la Mawaziri John Mbadi (Fedha) Hassan Joho (Madini), Opiyo Wandayi (Kawi) na Wycliffe Oparanya ( Ushirika) wamekuwa mstari wa mbele kusifu serikali ya Rais Ruto.
Kulingana na Prof Ojienda, ODM inaweza kushinikizwa kutoa mgombea mwenza wa Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.
“ODM itamuunga mkono Rais Ruto kwa muhula wa pili. Mnamo Februari 28, 2025, Raila atakuwa mwenyekiti wa AUC. Ataenda Addis Ababa,” Ojienda alidai.
Kamati Simamizi ya ODM, kwa upande wake, ilijibu kwa kusema: “Tunatoa wito kwa wanachama wetu wote kukumbuka kuwa ODM inasalia kuwa chama cha kisiasa kushindana na vingine vyote ili kutwaa mamlaka kwa njia za kidemokrasia.
“Ikaongeza taarifa ya chama hicho cha chungwa: “Kwa hivyo, ni lazima sote tuchunge matamshi yetu kuhusu mustakabali wa chama na hasa tuepuke kupiga ngoma za washindani wetu. Lazima tuendelee kujiimarisha katika kujiandaa na vita vilivyo mbele yetu.”
Kauli hii inajiri saa chache baada ya Rais William Ruto kuonyesha imani kuwa atashinda kwa muhula wa pili licha ya ukosoaji mkubwa unaoikabili serikali yake akijigamba kuwa hana mshindani. Ruto na kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga wanashirikiana huku waziri mkuu huyo wa zamani akisema hana mkataba wowote na kiongozi wa nchi.
Baadhi ya wanachama wa ODM wanasema utawala wa Ruto haupendwi na unaweza kushindwa katika uchaguzi kwa urahisi hata akiungwa mkono na ODM na kuzamisha maisha ya kisiasa ya wengi ndani ya chama cha upinzani.
“Kama hupendwi, haijalishi unaleta viongozi wangapi karibu nawe. Ruto atashindwa uchaguzini hata kama tunamuunga mkono kama ODM, sina shaka na hili,” Sifuna alisema katika mahojiano na Citizen TV.
“Ukiangalia mienendo ya kisiasa nchini hivi sasa, itakuwa ni upumbavu kwa ODM kutowasilisha mgombeaji urais. Itakuwa ni upumbavu sana. Ukiangalia hesabu, Ruto alitangazwa kuwa Rais kwa tofauti ya kura 200,000. Raila anachohitaji kufanya, inachohitaji ODM kufanya, ni kudumisha ngome zake. Hatujapoteza ngome yetu yoyote. Yeye amepoteza karibu nusu ya ngome yake katika Mlima Kenya.”
Mnamo Ijumaa ODM ilifanya mkutano wake wa kwanza wa Kamati Kuu mwaka huu, ambapo mustakabali wa chama ulijadiliwa na kikajitenga na wito wa kuunga Ruto 2027.
Mkutano huo uliongozwa na Kaimu Kiongozi wa Chama Anyang’ Nyong’o ambaye mwishoni mwa mwaka jana alikosoa serikali kufuatia visa vya ukiukaji wa haki za binadamu ukiwemo utekaji nyara na matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji. Kulingana na Prof Nyong’o, serikali ya Ruto inakiuka misingi ya demokrasia kwa kunyima raia uhuru waliotwikwa kikatiba.