Jamvi La Siasa

OKA yafufuka kuipa nguvu Azimio – Kalonzo

March 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA CHARLES WASONGA

UFUFUZI wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) ulioshirikiana na muungano wa Azimio la Umoja kuunda Azimio la Umoja-One Kenya, unalenga kumwezesha Kalonzo Musyoka kushinda mchujo ili aweze kupambana na Rais William Ruto debeni mwaka 2027.

Vinara wa OKA tuliozungumza nao kwa ajili ya makala hii walisema wamefikia uamuzi huo ili kutimiza baadhi ya masharti ambayo ODM ilitoa kwa Bw Kalonzo Musyoka iliposhikilia kuwa mgombea urais wa Azimio atateuliwa kupitia kura ya mchujo.

“Naibu Kiongozi wa ODM Wycliffe Oparanya alisema wazi kuwa tiketi ya urais ya Azimio haitatolewa moja kwa moja kwa Bw Kalonzo ila itashindaniwa. Na maseneta wa ODM Geoffrey Osotsi, Edwin Sifuna na wabunge kadhaa kutoka Magharibi na Nyanza walisema kuwa sharti kiongozi huyo wa Wiper afanye kampeni kali na asisubiri kuidhinishwa na Bw Odinga,” akasema Gavana wa zamani wa Murang’a Mwangi Wa Iria.

Kabla ya kubuni muungano mkuu na ambao ulisajiliwa kama muungano wa Azimio la Umoja-One kama muungano na chama cha kisiasa, OKA ilileta pamoja vyama vya Kanu, Wiper, Ford Kenya na Amani National Congress (ANC).

Vinara wa vyama hivi vyote Mbw Gideon Moi (Kanu), Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Musalia Mudavadi (ANC) walikuwa wametangaza azma ya kuwania urais.

Ama kwa hakika vyama hivi vilikuwa vimeanda makongamano ya wajumbe wao ambayo yaliwaidhinisha vinara hao kama wagombeaji urais.

Lakini mrengo wa Azimio ulioshirikisha vyama vya ODM na Jubilee na ule wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) ulioongozwa na Dkt William Ruto zilianzisha kampeni kali ya kugawanya OKA.

Hatimaye mnamo Januari 9, 2022 Ruto, wakati huo akiwa Naibu Rais, alifaulu kuvutia Mudavadi na Wetang’ula upande wake na wakabuni muungano wa Kenya Kwanza katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Bomas of Kenya, almaarufu kama “earthquake” (yaani tetemeko la kisiasa).

Hatua hiyo ilisababisha vinara waliosalia wa OKA, Bw Musyoka na Bw Moi, kuamua kujiunga na vinara wa Azimio Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta (sasa mstaafu) kuunda Azimio la Umoja-One Kenya uliomteua Bw Odinga kuwa mpeperushaji bendera yake ya urais.

“Kwa hivyo, kile kinachoendelea sasa ni OKA kujiimarisha ili mmoja wa vinara wake, Bw Musyoka, aweze kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Azimio la Umoja One Kenya kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2027. OKA haina nia ya kuondoka Azimio bali inajiandaa kwa mchujo wa urais. ODM na Jubilee pia zinajiandaa upande ule mwingine,” anasema Seneta wa Kitui Enoch Wambua.

Kwa upande wake, Bw Musyoka ambaye ni Naibu Rais wa zamani, alisema walimtembelea Gideon nyumbani kwake Kabarak kusaka baraka zake katika juhudi zao za kuipa nguvu OKA.

“Ifahamike kuwa hatuna nia ya kuvunja Azimio. Lengo letu ni kuiongezea nguvu zaidi huku tukirutubisha siasa vya vyama vingi. Juzi, nilisema nikiwa Homa Bay kwamba hata kama Baba ataondoka na Kwenda kule Addis Ababa sisi tuliosalia tutaendelea kujenga Azimio. Na sasa kile tunachofanya ni kuwaleta pamoja viongozi wetu walioamua kukaa kando kama vile ndugu yangu Gideon. Hatua hii isieleweke vibaya,” Bw Musyoka akaeleza.

Kiongozi wa Democratic Action Party (DAP-Kenya) Eugene Wamalwa aliyeandama na Bw Musyoka kule Kabarak alisema kuwa chama chake kitamteua Kalonzo wakati wa mchujo wa urais kuelekea uchaguzi wa 2027. Chama cha PNU pia kimeegemea upande wa OKA.

“Ninayo uhakika kwamba Bw Musyoka ataibuka mshindi,” akaeleza huku kauli yake ikiungwa mkono na Bw Wa Iria ambaye ni kiongozi wa chama cha Usawa Kwa Wote.

Lakini Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni alishikilia kuwa chama hicho kinachoongozwa na Bw Kenyatta kingali chama tanzu katika Azimio. Alidinda kuegemea mrengo wa OKA.

Msimamo sawa na huo ulichukuliwa na Kiongozi wa Narc Charity Ngilu aliyejitokeza kwa mara ya kwamba mjini Homa Bay alipohudhuria Kongamano la Kimataifa kuhusu Uwekezaji.