Jamvi La Siasa

Orengo: Ni ndoto kwa Kenya kuwa Singapore bila chaguzi za amani

Na BENSON MATHEKA November 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

GAVANA wa Siaya, James Orengo, amekosoa vikali hali ya demokrasia nchini Kenya, akisema haiwezekani taifa kutamani kuwa nchi iliyostawi ilhali inashindwa kuandaa uchaguzi wa amani.

Kauli yake inajiri wakati wa chaguzi ndogo zilizogubikwa na ghasia, madai ya vitisho na wasiwasi mkubwa kuhusu kuhusika kwa taasisi za serikali.

Kupitia chapisho katika mtandao wa X jana, Orengo alisema safari ya demokrasia ya Kenya imechukua mkondo wa kutisha, akiongeza kuwa ahadi ya Katiba ya 2010 bado haijatekelezwa ipasavyo.

“Hatuwezi kuwa nchi iliyostawi ikiwa, miaka mingi baada ya Katiba ya 2010, bado hatuwezi kufanya uchaguzi wa amani na haki,” aliandika.

Katika ujumbe wake, gavana huyo alilaumu serikali kwa kutumia mbinu zinazoathiri uhuru wa kujieleza na ushiriki wa wananchi, akisema kiwango cha nguvu na kuingiliwa (na serikali) kwa mchakato wa uchaguzi hakikubaliki.

Orengo pia alionya kuwa mtindo huu si wa Kenya pekee, akielekeza lawama kwa utawala kandamizi unaoibuka katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Kauli za Orengo zinaonekana kumlenga moja kwa moja Rais William Ruto, ambaye mara nyingi ametangaza kuwa Kenya iko njiani kuwa taifa lililostawi duniani.

Kulingana na Orengo, hakuna nchi inayoweza kupiga hatua ya aina hiyo bila kulinda misingi ya demokrasia, kuheshimu haki na kuhakikisha uchaguzi wa kuaminika.