Jamvi La Siasa

Osotsi: Hatutajadili kumvua Sifuna cheo ODM sababu bado tunaomboleza Raila

Na CHARLES WASONGA October 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Kiongozi wa ODM, Godffrey Osotsi, amepuuzilia mbali madai kwamba kuna mpango wa kumvua Katibu Mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna wadhifa wake kwa kuendelea kupinga Serikali Jumuishi.

Akiongea na Taifa Leo Jumapili, Bw Osotsi alisema ni mapema zaidi kwa hatua kama hiyo kuchukuliwa kwa sababu chama kingali kinaomboleza kifo cha aliyekuwa kiongozi wake Raila Odinga.

“Uamuzi kama huo hauwezi kuharakishwa kwa sababu wanachama wa ODM na Wakenya kwa ujumla wangali wanaomboleza. Kile tunapaswa kulenga wakati huu ni kuendelea kupalilia umoja katika chama na kuendeleza maadili ambayo Baba Raila Odinga alitetea,” akaeleza.

Bw Osotsi, ambaye ni Seneta wa Vihiga, alisema kuwa mkutano wa Baraza Kuu Simamizi la ODM (CMC) utakaofanyika leo, Nairobi, utajadili umoja katika chama, chaguzi ndogo za Novemba 27 na mustakabali wa chama baada ya kifo cha Raila.

“Mkutano huo hautakuwa na ajenda nzito kwa sababu chama na wanachama wangali wanaomboleza. Baadhi ya masuala yatakayojadiliwa ni umoja ndani ya chama na chaguzi ndogo zijazo. Maamuzi mazito, ikiwa yapo, yataibuliwa baada ya mwisho wa siku 30 za maombolezo,” akaeleza.

Hata hivyo, Seneta Osotsi alisema kauli ambayo Sifuna alitoa katika hafla ya mazishi ya Raila, Bondo, Siaya, mnamo Oktoba 19 inalandana na msimamo wa ODM.

“Seneta Sifuna hakutofautiana na yeyote wala kutoa kauli za kupotosha. Tulikubaliana kusalia katika Serikali Jumuishi hadi 2027. Huo ndio umekuwa msimamo wa Baba hadi alipokufa Oktoba 15,” akaeleza.

Bw Osotsi alikariri msimamo wake wa awali kwamba ajenda 10 zilizoko katika mkataba kati ya ODM na UDA ndizo zinazoshikanisha vyama hivyo wakati huu chini ya Serikali Jumuishi.

Miongoni mwa ajenda hizo ni; kulindwa kwa kuendelezwa kwa ugatuzi, utekelezaji mkamilifu wa ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (Nadco), uteuzi wa serikali unaozingatia usawa, kulindwa kwa haki za raia kuandamana na uhuru wa vyombo vya habari, kulipwa ridhaa kwa familia za wahasiriwa wa maandamano na kuwezeshwa kwa vijana.

Mnamo Agosti mwaka huu, Rais William Ruto na Bw Odinga waliteua Kamati maalumu ya kufuatilia utekelezaji wa mkataba huo wa maelewano kati ya ODM na UDA (MoU) uliotiwa saini Machi 7, 2025 katika KICC, Nationi.

Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa zamani Agnes Zani kama mwenyekiti na wakili Javas Bigambo kama naibu wake, ingali kutoa ripoti yake kamilifu kuhusu utekelezaji wa MoU hiyo.