Jamvi La Siasa

Otiende naye pia aanza kuongea lugha ya Sifuna

Na CECIL ODONGO December 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Rarieda Otiende Amollo ameonekana kupinga hatua ya baadhi ya wanasiasa kutoka Nyanza kujipiga kifua ndani ya Serikali Jumuishi akisema hakuna hakikisho lolote kuwa watamuunga mkono Rais William Ruto kwa muhula mwingine mnamo 2027.

Bw Amollo amesema kuwa hatua ya baadhi ya wanasiasa kujitapa kuwa walizungumza na Hayati Raila Odinga kuhusu kuunga mkono Rais William Ruto 2027 ni uongo na kile kinachoaminika ni kile tu marehemu alisema hadharani wakati alipokuwa hai.

“Watu ambao hata Raila hakuongea nao sasa wanasema eti Raila aliwaongelesha kama watu binafsi. Kile tunachoamini ni kile Raila alisema hadharani na hakusema kuwa tuunge mkono Rais Ruto baada ya 2027,” akasema Bw Amollo akiwahutubia waumini katika kanisa moja eneobunge lake.

Mbunge huyo alisema kuwa aliamua kukimya baada ya mauti ya Raila lakini misukosuko ambayo imekuwa ikishuhudiwa katika chama cha ODM baada ya Raila kuaga dunia sasa si ya kunyamaziwa tena.

“Wewe unasema tutaunga mkono Ruto 2027 lakini hakuna mtu amekuuliza. Sisi tunakubali tu na kudidimiza thamani yetu mbele ya serikali,” akaongeza Bw Otiende.

Kauli ya mbunge huyo sasa inaashiria kuwa yupo kwenye tapo moja na wabunge waasi ambao wamekuwa wakipinga Serikali Jumuishi.

Mrengo huo una Winnie Odinga, ambaye ni mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), mbunge wa Embakasi ya Mashariki Babu Owino, mwenzake wa Saboti Caleb Amisi na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna.

“Tunaweza kuwa na Rais Ruto au kukosa kuwa naye 2027. Hakuna mtu anafaa kutulazimisha kuhusu hilo. Uamuzi huo utategemea jinsi siasa zitakavyokuwa,” akasema.

Mbunge huyo alisema Nyanza haifai kujitapa ilhali uwakilishi wake katika serikali ni mdogo kuliko Mlima Kenya.

“Tuna mawaziri wawili pekee nao Mlima Kenya wana wanane. Sisi tuna makatibu wa wizara wanne na Mlima Kenya wana 12 halafu hata badala ya kujipiga kifua wanateta.

“Iwapo tutaendelea kusema kwamba tuko serikalini, basi tunashusha thamani yetu. Tunafaa kuitwa na kuwaniwa badala ya kusema tu tunaunga Rais na kushusha thamani yetu,” akaongeza.

Mbunge huyo alisema eneo la Nyanza halijakataa kuunga mkono Rais Ruto lakini mambo lazima yafanyike kwa maelewano na kwa kuwa ODM ni chama kikubwa, lazima waambiwe watapewa nini serikalini.

Kauli hiyo inajiri wakati ambapo Rais Ruto anaonekana bado ana uungwaji mkono Mlima Kenya baada ya ushindi katika eneobunge la Mbeere Kaskazini.

Ushindi huo unaonekana kuimarisha nafasi ya Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki kusalia katika wadhifa wake hadi baada ya 2027.

“Ukiangalia Kindiki ni naibu rais lakini kitambo mtu achaguliwe ngome yake ni vita. Sisi mbona tunakubali tu kwa wepesi? Thamani yetu iko wapi?” akauliza Bw Otiende anayehudumu muhula wake wa tatu bungeni.