Patanisho: Ruto alipelekea Uhuru mbuzi 12 Gatundu
RAIS William Ruto alichagua mbuzi kama zawadi katika ziara yake ya kwanza iliyotangazwa hadharani nyumbani kwa mtangulizi wake Uhuru Kenyatta huko Ichaweri, Gatundu, kaunti ya Kiambu.
Mbuzi ni mnyama mwenye umuhimu mkubwa miongoni mwa Wagikuyu na inaonyesha nia njema ya kuzika uhasama kati ya vigogo hao wawili wa kisiasa ambao awali walikuwa marafiki.
Mahojiano na walioandamana na rais hadi Kiambu yalifichua kwamba, alibeba mbuzi 12 pamoja naye. Walisafirishwa kwa lori kabla ya kuwasili kwake na Bw Kenyatta aliwapokea binafsi.
Nchi ilishangashwa Jumatatu, Desemba 9 na ziara isiyotarajiwa ya Rais Ruto katika boma la mashambani la mtangulizi wake huko Ichaweri, Gatundu Kusini, Kiambu.Ruto alikuwa naibu wa Kenyatta kutoka 2013 hadi 2022.
Wawili hao walitofautiana kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 na baada ya Dkt Ruto kuingia mamlakani, Bw Kenyatta alilalamika kuhangaishwa na serikali.ri
Shamba la Northlands lilivamiwa na wahuni waliokodishwa na watu wenye ushawishi serikalini ambapo mifugo wake waliibwa. Maafisa wa usalama walivamia nyumba ya mwana wa Uhuru kwa madai ya kusaka silaha haramu na walinzi wa mama yake, Mama Ngina Kenyatta waliondolewa.
Imeibuka kuwa, kabla ya ziara ya Ruto huko Ichwaweri, wawili hao walikutana Nairobi mnamo Novemba 16 na baadaye wakahudhuria kuwekwa wakfu kwa Askofu Peter Kimani Ndung’u wa Kanisa Katoliki kaunti ya Embu.
“Pia walikutana wiki iliyopita huko Caledonia( nyumbani kwa Uhuru, Nairobi) jioni moja,” duru zilifichua.Mwenyekiti wa Baraza la wazee wa Kikuyu Wachira Kiago alikiri kutohusika kwake katika ziara hiyo, akisema katika sherehe ambazo mbuzi huchinjwa, kuna sehemu ambazo huliwa katika karamu ya kuashiria kusameheana.
“Mbuzi huchukuliwa na wazee kutoka pande zote mbili na tambiko hufanywa,” alisema. “Je, mbuzi walikuwa wa matambiko au kama zawadi ya kirafiki? Taratibu pia lazima zitofautishwe. Je, ni matambiko kwa pande mbili au kwa jamii? Ikiwa ni kwa jamii, basi lazima wazee kutoka jamii hiyo wahusishwe na mahali pa kuwapeleka na kuwapokea mbuzi ni katika msitu au madhabahu. Ikiwa hii ilihusu wanaume hao wawili au familia zao, basi hilo ni jambo la kibinafsi la kifamilia,” alisema.
Baraza la Wazee
Katika mahojiano na Taifa Leo, Stephen Githinji, mwanachama wa Baraza la Wazee wa Kikuyu, alieleza kuwa mbuzi wana maana mbili kuu katika jamii; malipo ya mahari na kuwafanya vijana kuwa watu wazima katika jamii.Mbuzi wanaotumiwa kulipa mahari huashiria baraka za wazazi kwa wanandoa waweze kufanikiwa.
Ingawa haijafahamika ni kwa nini Ruto alichagua kupeleka mbuzi kwa Kenyatta, Bw Githinji alipendekeza kuwa ikiwa Rais alikuwa akiomba msamaha kwa matendo yake ya awali, lingekuwa jambo la busara kuwahusisha wazee wa Kikuyu wanaofahamu utamaduni huo.Hata hivyo, haijulikani ikiwa wazee kutoka pande zote mbili walihudhuria mkutano huo wa faragha.
“Japo Kenyatta anasalia kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya, yeye si mzee wa Kikuyu. Ili tuhitimishe kuwa Ruto amesamehewa na kutafuta baraka za Kenyatta kupitia mbuzi, wazee walipaswa kuwepo. Vinginevyo, hatua hiyo haina maana yoyote,” Githinji alisisitiza.
Uhusiano kati ya Ruto na Kenyatta ulidorora kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.Bw Kenyatta alimuunga mkono Bw Odinga, ambaye aliwania urais kwa tikiti ya muungano wa Azimio la Umoja, hatua ambayo haikumpendeza Dkt Ruto.
Licha ya hayo, Ruto alifanikiwa kuwania urais na tikiti ya muungano wa Kenya Kwanza na kumbwaga Bw Odinga.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA