• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 11:15 AM
Putin ajigamba kwa ‘jeuri’ baada ya ushindi mkubwa Jumapili

Putin ajigamba kwa ‘jeuri’ baada ya ushindi mkubwa Jumapili

NA WANDERI KAMAU

RAIS wa Urusi Vladimir Putin ametetea uvamizi nchini Ukraine na kuikosoa jamii ya kimataifa kwa kuingilia mzozo huo.

Putin alitoa kauli hiyo baada ya kupata ushindi mkubwa kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo mnamo Jumapili.

Ni uchaguzi ambao uliweka msingi thabiti wa kisiasa katika utawala wake.

Akizungumza saa chache baada ya kutangazwa kama mshindi, Putin alisema ushindi huo ulionyesha kwamba Urusi imekuwa ikifanya vizuri kupinga hatua ya mataifa ya Magharibi kuwapeleka wanajeshi wake nchini Ukraine.

Putin, aliyechukua uongozi wa taifa hilo kwa mara ya kwanza mnamo 1999, alisema kuwa ushindi huo unafaa kutuma ujumbe mkali kwa mataifa ya Magharibi kwamba Urusi imepata ushujaa mpya—bila kujali ikiwa kuna mwafaka utakaopatikana kuhusu vita vinavyoendelea nchini Ukraine au la.

“Huu ni ujumbe unaoshiria kuwa hatutahofishwa na mtu ama nchi yoyote kwa miaka mingi ijayo. Ni ujumbe kuwa Urusi imefanya maamuzi yake kwa njia huru bila hofu na bila vitisho kutoka nje,” akasema kiongozi huyo.

Matokeo hayo yanamaanisha kuwa Putin, 71, atahudumu kwa muhula mpya wa miaka sita.

Wadadisi wanasema hilo litamfanya kuwa kiongozi atakayekuwa amelitawala taifa hilo kwa muda mrefu zaidi katika miaka 200 iliyopita, kwa kumpita kiongozi wa zamani, Josef Stalin.

Putin alipata ushindi kwa kuzoa asilimia 87.8 ya kura, ushindi ambao umetajwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kupatwa na kiongozi yeyote katika historia ya taifa hilo.

Rais wa Urusi Vladimir Putin. PICHA | MAKTABA

Mashirika kadhaa yamethibitisha kuwa matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa ya kweli.

Hata hivyo, mataifa kadhaa—yakiwemo Amerika, Ujerumani, Uingereza kati ya mengine—yametaja uchaguzi huo kutokuwa huru na wenye haki, kutokana na vitisho vilivyokuwa vikielekezwa kwa viongozi wa upinzani.

Mwaniaji wa Chama cha Kikomunisti, Nikolai Kharitonov, aliibuka wa pili kwa kuzoa asilimia nne za kura. Wale waliofuata ni Vladislav Davankov na Leonid Slutsky, walioibuka wa tatu na wa nne mtawalia.

Putin aliwaambia wafuasi wake kwenye hotuba ya ushindi jijini Moscow kwamba, jukumu lake la kwanza litakuwa kulainisha masuala yanayohusiana na “ shughuli za kijeshi za Urusi nchini Ukraine” ili kulipa nguvu zaidi jeshi la taifa hilo.

“Tuna majukumu mengi yaliyo mbele yetu. Lakini tukiwa pamoja kwa saa, hakuna mtu atakayefaulu kututisha. Hatujawahi kutishwa hata kidogo, na hilo halitafanyika leo ama siku za usoni. Hawatafaulu,” akasema Putin.

Wafuasi wake walimshangilia kwa kusema “Putin, Putin, Putin” na “Urusi, Urusi, Urusi” alipoamka kuwahutubia.

Licha ya ushindi wake mkubwa, baadhi ya raia walisusia uchaguzi huo kulalamikia kifo cha kiongozi wa upinzani, Alexei Navalny, aliyefariki katika hali tatanishi kwenye gereza moja eneo la Arctic mwezi uliopita.

Hata hivyo, alisema kuwa ususisaji huo haukuwa na athari zozote kwenye ushindi aliopata.

Wadadisi wanasema kuwa ushindi huo mkubwa wa Putin umeyaacha mataifa ya Magharibi katika njiapanda, kwani unaonyesha bado ana uungwaji mkono mkubwa, licha ya kifo tata cha mpinzani wake mkuu, Navalny.

“Kwa sasa, wengi wanamwona Putin kama ‘mwanamapinduzi’ ambaye amelisaidia taifa hilo kupata usemi mpya duniani tangu kumalizika kwa Vita Baridi vya Dunia mnamo 1990. Kwa baadhi ya wafuasi wake, Putin yuko kwenye hadhi moja na viongozi kama Josef Stalin au Mao Zedong kutoka China,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mdadisi wa siasa za kimataifa.

  • Tags

You can share this post!

Simulizi ya Gachagua alivyopoteza ndugu zake kupitia pombe

Ajali: Wanafunzi wanane wa KU wahamishiwa Nairobi kwa...

T L