Raila aachiwa Mungu kura ya AUC ikiwadia wiki hii
KINARA wa upinzani Raila Odinga anaingia wiki ambayo mustakabali wake wa kisiasa utaamuliwa huku viongozi mbalimbali wakimtilia dua afanikiwe kwenye azma yake ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Bw Odinga amekuwa akiendeleza kampeni kali ya kuzunguka kote bara Afrika na viongozi wa ODM Jumapili waliongoza mkutano mkubwa katika Kaunti ya Kakamega kumwombea afanikiwe.
Uchaguzi huo utafanyika Jumamosi wiki hii.
Gavana wa Kisii Simba Arati ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama na mwenzake wa Homa Bay Gladys Wanga (mwenyekiti wa chama) pamoja na mwenyeji wao Fernandes Baraza, Jumapili waliwaongoza wanasiasa kumwombea kinara huyo wa ODM ili afanikiwe AUC.
Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi na wabunge kadhaa pia walihudhuria mkutano huo ambapo pia Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alitetewa baada ya kushutumiwa na baadhi ya wana ODM kwa kuikashifu serikali jumuishi.
Maombi hayo yalifanyiwa kwenye Kanisa la House of Grace Kakamega.
Bw Odinga atakuwa akikabiliana na Waziri wa Masuala ya Nje wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Kisiwa cha Madagascar James Randriamandrato.
Jana, viongozi wa ODM walisema kuwa wana imani Raila atatwaa kiti cha AUC mnamo Jumamosi, wakitoa wito kwa kila Mkenya kuzidisha ibada ili waziri huyo mkuu wa zamani afanikiwe.
Akiongea na redio ya Nam Lolwe inayopeperusha matangazo yake kwa Lugha ya Kiluo, Bi Wanga aliwataka Wakenya hasa wakazi wa Nyanza washiriki mfungo wiki hii yote, ili waiombee azma ya Raila.
“Nawaomba watu wetu kuwa wiki hii ni takatifu hatutakula na tutakesha tukiomba ili kigogo wetu Raila afanikiwe kwenye azma yake. Tufunge, tunyenyekee na tujizuie na jambo lolote lile hadi Raila ashinde,” akasema Bi Wanga.
Kauli yake Bi Wanga imezua mdalaho huku wengi wakifasiri kuwa huenda alikuwa akiwataka wasishiriki unyumba hadi Raila apate ushindi.
Akiwa Kakamega, Gavana huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa ODM alisema kuwa wote wana matumaini kuwa ifikapo Jumamosi, Bw Odinga atarudi nyumbani akiwa nyapara wa AUC.
“Sina shaka kwa sababu Raila amefanya kampeni kabambe, amezuru Afrika kote, amekutana na Marais na kile ambacho kimesalia sasa ni maombi ya kufaulisha azma yake,” akaongeza Bi Wanga.
Mbunge wa Funyula Oundo Midenyo alisema Wakenya wote wanastahili wakeshe wakimwombea Raila wiki hii yote bila kusita kwa sababu kilichobakia sasa ni hilo tu.
“Malengo yetu wiki hii ni kuomba ili ifikapo Jumamosi kiongozi wetu Raila Odinga awe amefanikiwa AUC,” akasema Bw Oundo.
“Sisi sote tunajua Raila amejaribu kupata uongozi wa nchi hasa 2007 ambapo tulisherehekea ushindi wake lakini mambo yakabadilika. Nawataka wote mumwombee ili mara hii afanikiwe kwa sababu anatosha kuwa kiongozi wa Afrika,” akasema Mbunge wa Kisumu Magharibi Akinyi Buyu.
Gavana Barasa, alisisitiza kuwa wapo nyuma ya Raila na wakazi wa kaunti hiyo wanasubiri tu atangazwe mshindi Jumamosi ili washerekee ushindi wake.
Bw Odinga mwenyewe ameonyesha imani kuwa atashinda kura hiyo.
Bw Odinga alisema kampeni zake zimekuwa za mafanikio na anatarajia kupata idadi kubwa ya kura kutokana na juhudi za kampeni zake ambazo zilimpeleka katika mataifa mbalimbali barani Afrika kutafuta uungwaji.
“Kampeni zimefanikiwa. Tumefanya kampeni katika maeneo mbalimbali barani Afrika, na tuna uhakika tutapata kura kutoka kwa mataifa mengi katika bara hili,” akasema Bw Odinga.
Akizungumza wakati wa ziara katika eneo la Eastleigh, eneo bunge la Kamukunji, alipotembelea ghafla jumba la biashara la Business Bay Square (BBS), Bw Odinga alisisitiza umuhimu wa kushirikisha sekta ya binafsi katika maendeleo ya Afrika.