Raila ashtuka maafisa wa ODM wakionyesha dalili za uaminifu kwa Ruto
MAKUNDI mawili yaliibuka ndani ya Orange Democratic Movement (ODM) kufuatia mkutano uliofanyika Jumanne wa kamati kuu ya chama hicho, Taifa Leo imefahamu.
Vyanzo kutoka mkutano wa Kamati Kuu ya Usimamizi (CMC) vimeeleza jinsi maafisa wakuu waligawanyika katika makundi mawili wakati wa mkutano huo kuhusu kuunga mkono ushirikiano wa kiongozi wa chama Raila Odinga na Rais William Ruto.
Hali hiyo ilishtua na kumfanya Bw Odinga kupendekeza kuundwa kwa kamati ya kiufundi itakayopitia utekelezaji wa ajenda 10 ili kudhibiti mgawanyiko huo.
Sasa Bw Odinga anazidisha shinikizo kwa Rais Ruto kulinda haki ya mikutano ya amani na maandamano, kulipa fidia waathiriwa na kulinda utawala wa sheria pamoja na katiba.
Utekelezaji wa ajenda hizi unaweza kuimarisha mkataba huo au kuudhoofisha kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.
Wakati wa mkutano huo, Kiongozi wa Upinzani Bungeni Junet Mohamed, mwenyekiti wa ODM na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, kiongozi wa Vijana John Ketora, na kiongozi wa Wanawake Beth Syengo walikuwa mstari wa mbele kuunga mkono serikali ya Rais Ruto.
Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, ambaye amekuwa mkosoaji mkali wa mkataba huo, aliungwa na manaibu wawili wa chama Godfrey Osotsi (Seneta wa Vihiga) na Abdulswamad Nassir (Gavana wa Mombasa) pamoja na Mweka Hazina wa chama Timothy Bosire dhidi ya shinikizo za wenzake waliopendekeza aondolewe kutoka wadhifa huo.
Pia timu hiyo ilihoji ari ya Rais Ruto katika utekelezaji wa ajenda 10 ambazo yeye na Bw Odinga walitia saini mwezi Machi.
Bw Bosire alikataa uteuzi wa Rais Ruto kama mwenyekiti wa Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) mwezi Januari.
Gavana wa Kisumu Profesa Anyang’ Nyong’o alichukua msimamo wa kati, akilalamikia pande zote mbili kwa misimamo mikali. Pia aliwaonya maafisa wa ODM waliokuwa wakipigia debe urais wa Ruto.
“Wakifika hapa walikuwa na maoni tofauti kuhusu masuala mengi ndani ya chama na nchi, lakini kamati ilifanikiwa kuleta mshikamano usiovunjika na malengo ya pamoja ya kuhakikisha ODM inaendelea kuwa mtumishi mwaminifu wa watu na nchi,” chama kiliandika.
Afisa mmoja aliyezungumza na Taifa Leo bila kutaja jina alisema mkutano umefungua nafasi kwa wanachama kuchambua na kuhoji ari ya Rais Ruto.
“Kama kikosi kazi kitatoa ripoti na upande wa UDA ukikataa utekelezaji, tutahitimisha kuwa hawajali Mkataba wa Makubaliano (MoU),” alisema afisa huyo.
“Baadhi ya masuala kama fidia na ukatili wa polisi ni magumu na yana athari za kisiasa. Itakuwa ushindi mkubwa kwa ODM ikiwa yatafanyika kwa sababu yanagusa mwananchi wa kawaida. Lakini kwa UDA, kulipa fidia ni kukiri mauaji yaliyotokea wakati wa maandamano,” alisema.
Afisa mwingine alifichua jinsi wanachama walivyochukua msimamo thabiti bila kuwa maadui wakati wa mkutano ulioendelea kwa saa nyingi.
“Kulikuwa na hisia kwamba Katibu Mkuu alikuwa akasababisha mkanganyiko; baadhi ya wanachama walisema kama kila afisa angeleta maoni yake binafsi kuhusu masuala ya chama, basi chama kingevurugika,” alisema afisa mwingine.
“Hata hivyo, wanachama walionyesha wasiwasi kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu; masuala ya kuwakamata na kuwateka wanaodhaniwa kuwa wapinzani wa serikali. Lakini pia kulikuwa na hisia kwamba licha ya ajenda nyingi kutotekelezwa kikamilifu, kulikuwa na maendeleo fulani.”
Bw Odinga amejikuta akijaribu kusimamia makundi mawili yenye mawazo yanayokinzana.
Timu inayoongozwa na Bw Sifuna imeanza kusafiri nchini na kuvutia vijana wa kisiasa kutoka ODM na UDA.
Miongoni mwa wanachama maarufu katika timu hiyo ni Bw Osotsi, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino (ODM), Mohammed Ali (Nyali, UDA), Timothy Wanyonyi (Westlands, ODM), Anthony Kibagendi (Kitutu Chache, ODM), Caleb Amisi (Saboti, ODM) na wabunge wengine vijana.
Bw Odinga anakabiliwa na kazi ngumu ya kuhakikisha fidia kwa waathiriwa wa ukatili wa polisi wakati wa maandamano. Wengi wa waathirika wa maandamano ya 2023 walikuwa wafuasi wake.