Jamvi La Siasa

Raila ataka lalama zote za Wakenya zishughulikiwe akijiandaa kuingia serikalini

Na GEORGE ODIWUOR February 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga ametoa wito wa suluhu ya kudumu kuhusu masuala yanayozonga nchi, akikiri hadharani Wakenya wamemlilia kuhusu hali ngumu ya maisha na ukosefu wa maendeleo nchini.

Bw Odinga Alhamisi alisema amewasikiza Wakenya na wengi wao wanachukia changamoto na mkondo ambao taifa linaelekea.

“Jinsi unavyojua tulitoka kwenye kampeni kali ya kuzunguka Afrika, tumerudi nyumbani na watu wanataka sana kujua mwelekeo ambao tutauchukua,” akasema Bw Odinga.

“Tumeshuhudia watu wakitekwa nyara na kuzuiliwa kwa siku kadhaa. Pia tumeona watu wakiuawa kinyama na hayo ni mambo ambayo lazima yakome,” akaongeza.

Alikuwa akiongea mjini Homa Bay wakati wa kushauriana na wananchi kuhusu ushirikiano ambao ameuanzisha na Rais William Ruto.

Wanasiasa hao wawili wameonekana kuafikiana kugawana serikali na Bw Odinga amekuwa akizunguka ngome yake kuwaeleza wafuasi wake kwa nini amekumbatia mwelekeo huo kisiasa.

Mnamo Jumanne, waziri huyo mkuu wa zamani alikuwa Kaunti ya Kisumu na jana kabla ya kufika Homa Bay alitua Migori. Hii leo atakuwa Busia wakati ODM itakuwa ikiadhimisha miaka 20 tangu ianzishwe.

Uongozi mbaya, ufisadi, ukabila, vijana kukosa ajira, migomo ya mara kwa mara ya wafanyakazi na watu kunyimwa uhuru wa kuongea ni baadhi ya mambo Bw Odinga alisema yanastahili kutatuliwa.

Kiongozi huyo wa ODM pia alitoa wito kaunti ziongezewe mgao hadi asilimia 30 akisema ugatuzi hauwezi kufanya kazi kama magavana hawapati pesa za kutosha.

“Tunataka kuona rasilimali zaidi zikitengewa kaunti ili kuimarisha sekta ya afya na ile miundomsingi,” akasema.

Wakati wa kikao hicho, vijana walisema wanahitaji nafasi za ajira na uwezo mkubwa wa kujiendeleza. Bw Odinga alisema atahakikisha serikali inasaidia vijana kutumia teknolojia kusaka riziki.

“Vijana ndio wengi nchini na wanastahili kutumia teknolojia kujiendeleza wakisaidiwa na serikali,” akasema.

Kuhusu Bima ya Afya ya Kijamii (SHA), Bw Odinga aliitaka serikali kushughulikia malalamishi ya raia wanaosaka matibabu.

“Watu wanahitaji huduma bora ndiyo maana suala la SHA linastahili kupata utatuzi,” akasema Bw Odinga.