• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 2:53 PM
Raila ataka Ruto ‘ashuke’ naye akiwekewa presha

Raila ataka Ruto ‘ashuke’ naye akiwekewa presha

NA WANDERI KAMAU

SHINIKIZO zinaendelea kumzidia kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, kumtaja mrithi wake ielekeapo 2027, baada ya kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, kusema kuwa hatamuunga mkono tena Bw Odinga kuwania urais.

Hizi presha zinajiri wakati ambapo Bw Odinga anajaribu kunyanyuka baada ya maruerue ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Kiongozi huyo wa Azimio na chama cha Orange Democratic Movement (ODM) anaendeleza mashambulio yake ya kisiasa kwa utawala wa Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto akisema ni sharti ikome kutoza ushuru dhalimu na iteremshe gharama ya maisha nchini.

Lakini sasa Bw Musyoka ambaye ni mwandani wake wa muda mrefu, ameshasema kuwa atakuwa debeni 2027, hivyo hawezi tena kumuunga mkono Bw Odinga, baada ya kufanya hivyo mara tatu—2013, 2017 na 2022.

Kwenye mahojiano mapema wiki hii, Bw Musyoka alisema yuko tayari kuwania nafasi hiyo, kwani sasa “yeye ni kifaranga aliyepevuka kisiasa”.

“Ikiwa nilikuwa tayari kuwania urais mnamo 2002 na 2013, ni sababu ipi inakufanya kufikiri kwamba sitakuwa tayari 2027? Wakati umefika nchi hii kumtambua kiongozi ambaye imekuwa ikimkataa. Nimejitolea…nimewaunga mkono wengine bila kujipenda. Ikiwa nchi iko tayari, niko tayari kuwania.

Kutowania nafasi ya urais kutamaanisha niende nyumbani. Tuko kwenye mwisho wa mchakato ambao unafaa kulikomboa taifa hili. Mara hii, Azimio itampa Rais William Ruto mwaniaji atakayempa ushindani mkubwa,” akasema Bw Musyoka, kwenye mahojiano na runinga ya NTV.

Kando na Bw Musyoka kusema hatamuunga mkono Bw Odinga, washirika wake pia wamemshinikiza kutomuunga mkono kiongozi huyo tena.

Badala yake, washirika hao wanamtaka Bw Odinga “kumrudishia mkono” Bw Musyoka, kwa kumuunga mkono kuwania urais 2027.

Kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, Bw Odinga alimteua Bi Martha Karua kama mgombea-mwenza wake.

Baadhi ya washirika wa Bw Musyoka ambao wamejitokeza wazi na kumtaka Bw Odinga kutowania 2027 na badala yake kumpigia debe Bw Musyoka ni maseneta Enoch Wambua (Kitui), Dan Maanzo (Makueni), wabunge Jessica Mbalu (Kibwezi Mashariki), Patrick Makau (Mavoko), Gideon Mulyungi (Mwingi ya Kati) na Makali Mulu (Kitui ya Kati).

Akasema Bw Wambua: “Bila tashwishi yoyote, Bw Musyoka ndiye Rais ambaye Kenya imekuwa ikimngoja. Tayari, Wakenya wengi wanajiandaa kwa urais wa Bw Musyoka. Lazima Kalonzo achukue nafasi hiyo ifikapo SAgosti 2027.”

Bw Maanzo alisema huwezi kufanya jambo moja kwa njia moja kwa muda mrefu na kutarajia matokeo tofauti.

“Changamoto zetu kwa Bw Musyoka ni kwamba mara hii, lazima awe debeni. Hana jingine ila kuzingatia uamuzi huo, ikiwa anataka kutimiza ndoto yake ya kuwa rais wa taifa hili,” akasema Bw Maanzo.

Kutokana na shinikizo hizo, wadadisi wanasema kuwa katika hali hii, Bw Odinga hana jingine ila kumuunga mkono Bw Musyoka au kumtangaza mrithi wake kisiasa.

“Ni wazi kuwa Bw Odinga yuko katika njiapanda kisiasa. Shinikizo zinazotolewa na Bw Musyoka na washirika wake ni ishara za mapema kwamba hawatamuunga mkono. Pili, amekuwa akishinikizwa na baadhi ya viongozi kutoka eneo la Nyanza kumtaja mrithi wake kisiasa. Tatu, ushirikiano wake na Rais Ruto si hakikisho kwamba atamuunga mkono kwa nafasi yoyote ya kisiasa katika siku zijazo. Bila shaka, ni wazi kuwa yuko kwenye njiapanda kisiasa,” asema Bw Micah Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

Miguna Miguna: Simba kwa mapenzi anatulia

Gachagua aahidi kuponda wafufuaji wa ‘Mungiki’

T L