Jamvi La Siasa

Raila roho mkononi mataifa 16 ya kusini mwa Afrika yakivuruga hesabu zake AUC

Na JUSTUS OCHIENG February 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WANACHAMA wa kampeni ya mgombeaji wa Kenya wa kiti cha mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) Raila Odinga, wangali na ujasiri kwamba atashinda hata baada ya Jumuiya ya nchi 16 ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kumuunga Waziri wa Masuala ya Nje wa Madagascar, Richard James Randriamandrato dakika za mwisho.

Kwa miezi kadhaa, Bw Odinga na Waziri wa Masuala ya Nje wa Djibouti, Mahmoud Ali Youssouf walikuwa wamepigiwa upatu kuwa wagombea wakuu lakini kuidhinishwa dakika za mwisho kwa Bw Randriamandrato kunaweza kubadilisha matokeo.

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Jumamosi, Februari 15 mjini Addis Ababa, Ethiopia.

“Jamhuri za Madagascar na Mauritius, katika Baraza la Agosti 2024, ziliwasilisha mgombeaji kila moja kwa wadhifa wa Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika, ambao ni Bw Richard J. Randriamandrato na Bw Anil Kumarsingh Gayan, mtawalia.

“Tangu wakati huo tumegundua kuwa Mauritius imeondoa mgombeaji wake, na kuiacha Madagascar kuwa nchi pekee mwanachama kutoka eneo la SADC anayegombea kiti hicho,” ilisema barua hiyo.

Iliongeza: “Naandika kukujulisha, Mheshimiwa Waziri, kwamba, Mheshimiwa Richard J. Randriamandrato, aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Nje wa Jamhuri ya Madagascar, ameorodheshwa kuwa mgombea pekee kutoka SADC wa kiti cha Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika.

Katika suala hili, Jamhuri ya Madagascar imeandikia rasmi ofisi kuu ya Jumuiya ikitaka mgombeaji wake kuungwa mkono na nchi wanachama wa SADC.

Kwa hivyo, barua hii, inatumwa kuhimiza nchi wanachama wa SADC kumuunga mkono Bw Richard J. Randriamandrato, mgombeaji kutoka kanda yetu, kwa wadhifa wa Mwenyekiti wa AUC,” ilisema taarifa ya Elias M. Magosi, Katibu Mkuu wa SADC.

Bw Odinga aliwasili Addis Jumatano jioni, Februari 12 baada ya kuhitimisha kampeni zake jijini Bujumbura, Burundi, ambako alikutana na Rais Evariste Ndayishimiye.Bw Odinga, mwanasiasa mkongwe wa Kenya, Jumatano usiku na Alhamisi alikutana na Mawaziri mbalimbali wa Masuala ya Nje pembezoni mwa kikao cha 46 cha kawaida cha Baraza Kuu ya AU.

Katibu Mkuu wa Masuala ya Kigeni Korir Sing’oei, ambaye pia ni mkuu wa sekretarieti ya kampeni ya Bw Odinga, alisema Alhamisi kwamba wana uhakika watapata ushindi licha ya mawasiliano ya dakika za mwisho ya SADC kwa mataifa wanachama wake.