• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
Rais Ruto aonya wanaotaka kuzima nyota yake

Rais Ruto aonya wanaotaka kuzima nyota yake

NA MWANGI MUIRURI

RAIS William Ruto mnamo Jumatano amelia kwamba baadhi ya mabwanyenye almaarufu ‘masonko’ nchini, wameungana kuzima nyota yake ya kuwahudumia mahasla.

Rais alilalama kuwa kuna njama ya kuteka nyara utawala wake ndio ukwame na upoteze umaarufu kabla ya 2027 ambapo uchaguzi mwingine mkuu utawadia.

Lakini akaahidi wanaosuka njama hizo kwamba kutazuka mtitimuano mkali wa misuli ambao alionya yeye hayuko tayari kuwapisha au kupoteza mchezo.

Alisema kwamba masonko hao hawaelewi kwamba alikabidhiwa upanga katika kiapo chake cha urais.

“Wanadhania huo upanga ni wa kukatakata mboga. Watashangaa kwa kuwa nitautumia kuondolea taifa hili siasa za utapeli, ufisadi na ukora,” akasema Rais Ruto.

Alisema upanga huo ulimfanya kuwa rais wa kudhibiti hali zote za taifa hili ambalo limechelewa kimaendeleo na katika jitihada zake, “mtashangaa ninyi wa njama chafu za kuombea taifa hili umaskini ndipo muendelee kulidhibiti na kujipakulia manufaa yenu ya kibinafsi”.

Rais William Ruto (kati) akiwa na viongozi wengine wakati wa uzinduzi wa mradi wa nyumba za bei nafuu mjini Nanyuki mnamo Januari 10, 2024. PICHA | JOSEPH KANYI

Akihutubu katika Kaunti ya Laikipia, Rais Ruto ambaye alishinda kura ya Agosti 9, 2022, kwa msingi wa ahadi ya kuinua walala hoi, alisema hilo ndilo linapingwa kwa mikakati ya wapinzani ndani ya siasa na kupitia kesi mahakamani.

“Lakini nimeamua kukabiliana nao kimasomaso na nitawakalia ngumu. Sitakubali wachache wahujumu ajenda yangu ya kimaendeleo kwa kuwa mimi niko na wajibu wa kikatiba unaonilazimisha kuinua maisha ya maskini,” akasema.

Alisema kwamba wakora, matapeli na mafisadi ndio mahangaiko makuu katika utawala wake, akiapa kuwa “sasa mimi ndio kuamua, sitanunua wakili na sitahonga mahakama mimi sasa ndio idhini ya miradi ya serikali “.

Rais William Ruto akiwa na viongozi wengine wakati wa uzinduzi wa mradi wa nyumba za bei nafuu mjini Nanyuki mnamo Januari 10, 2024. PICHA | JOSEPH KANYI

Rais alishikilia kauli yake ya wiki moja sasa kwamba hatakubali maamuzi ya mahakama ambayo yanalenga kuhujumu miradi yake mikuu kama afya bora kwa wote na pia ujenzi wa nyumba kwa bei nafuu.

“Wanaonipinga mahakamani wako na kazi, wake wao wana kazi, watoto wao wana ajira na hata wamewekeza katika biashara. Wote hao wako na majumba aushi na bima za afya. Sasa wanapinga hasla wangu asinufaike na afya bora na makazi kwa bei nafuu. Nawakanya wasahau, na wasiposikia ni mimi na wao, ” akasema Rais.

Aliongeza kwamba taifa hili limechelewa kimaendeleo kutokana na siasa mbaya na pia uongozi wa walioogopa kufanya maamuzi magumu.

“Liwe liwalo hayo maamuzi mimi sasa nitayafanya. Mimi sitangojea idhini ya wachache mafisadi walio na pesa ya kuhonga wakili na kununua jaji kunitatiza. Nitaamua hadi nchi ikwamuke,” akasema.

Rais William Ruto akiwa na viongozi wengine wakati wa uzinduzi wa mradi wa nyumba za bei nafuu mjini Nanyuki mnamo Januari 10, 2024. PICHA | JOSEPH KANYI

Rais alisema kwamba mpango wa ujenzi wa nyumba nafuu kwa sasa umeajiri watu zaidi ya 200,000 katika sekta mbalimbali na pia maeneo 40 ya ujenzi.

“Sasa wakisikia tunapanua maeneo ya mijengo hadi zaidi ya 100 na kwa mfano hapa Laikipia niunde wamiliki wa nyumba zaidi ya 10,000 wanakimbia mahakamani kupinga,” akasema.

Rais Ruto katika ziara hiyo ya Laikipia alizindua mradi wa ujenzi wa nyumba Mjini Nanyuki,  akaanzisha ujenzi wa barabara ya Ngobit-Withare-Lamuria hadi kwa shule ya upili ya wasichana wa Ngobit na ile ya msingi ya Kihara.

Hatimaye alizindua kiwanda kipya cha New KCC mjini Nyahururu.

  • Tags

You can share this post!

Shule yalia matokeo licha ya kuwika Kilifi

Pauni moja ya Uingereza sasa ni Sh200 katika tukio la...

T L