Roho mkononi kwa Gachagua korti ikiamua leo iwapo Kindiki ataapishwa au la
MBIVU na mbichi zitajulikana leo Oktoba 31, 2024 wakati Mahakama Kuu itakapoamua ikiwa Waziri wa Usalama Prof Kithure Kindiki ataapishwa kutwaa wadhifa wa Naibu Rais au la.
Majaji Eric Ogola, Antony Mrima na Dkt Freda Mugambi wataamua ikiwa Bunge la Seneti lilimtimua mamlakani aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa mujibu wa sheria.
Majaji hao waliombwa na Mwanasheria Mkuu Dorcus Oduor na mabunge ya Kitaifa na Seneti wafutilie mbali agizo la kuzuia kuapishwa kwa Prof Kindiki kwa madai hakuteuliwa kwa mujibu wa sheria.
Majaji hao watatu walielezwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Prof Githu Muigai na mawakili wa mabunge mawili na maspika Moses Wetang’ula na Amason Kingi hakuna sheria iliyovunjwa kumteua Prof Kindiki kutwaa wadhifa wa Naibu Rais.
Prof Kindiki aliteuliwa na Rais William Ruto baada ya Bunge la Seneti kupitisha kutimuliwa kwa Bw Gachagua Oktoba 17, 2024.
Bunge la Seneti lilimpata Bw Gachagua na hatia katika mashtaka matano ya kueneza ukabila, hujuma, madharau na kubwabwaja siri za serikali kwa umma kinyume cha sheria.
Baada ya bunge la kitaifa kumpata na hatia Bw Gachagua, ilipiga kura na kupitisha hoja ya kumtimua kazini Oktoba 8, 2024.
Uamuzi huo ulipelekwa katika Bunge la Seneti ambapo Bw Gachagua aliamriwa awasilishe ushahidi wa kujitetea dhidi ya madai ya utovu na ukiukaji wa maadili ya kiongozi wa kitaifa na ubaguzi.
Bunge la kitaifa lilipokea pendekezo la Rais Ruto la kumteua Prof Kindiki kutwaa wadhifa wa Naibu Rais.
Jina lake lilichapishwa katika Gazeti rasmi la serikali akisubiri kuapishwa.
Kabla ya kuapishwa kwa Prof Kindiki kuwa Naibu Rais, Bw Gachagua na walalamishi wengine 30 waliwasilisha ombi katika mahakama kuu wakiomba uteuzi wa waziri huyo wa usalama ufutiliwe mbali.
Katika ombi la kumzima Prof Kindiki, Bw Gachagua amedai Naibu Rais huyo mteule hajahitimu kutwaa wadhifa huo kwa vile sio mwanachama wa chama cha kisiasa cha United Democratic Alliance (UDA).
Majaji walielezwa Prof Kindiki alijiuzulu kabla ya uchaguzi mkuu Agosti 9, 2022 kuwa mwanachama wa UDA.
Mawakili Paul Muite, Prof Elisha Ongoya, Tom Macharia (wanaomwakilisha Gachagua) na Jackson Kala anayewakilisha chama cha Wiper waliomba korti ikubaliani na maamuzi ya Majaji Richard Mwongo na Chacha Mwita kwamba uteuzi wa Bw Gachagua unakinzana na mwongozo wa Katiba kuhusu uteuzi.
Mabw Muite na Macharia walieleza Majaji Ogola, Mrima na Mugambi kwamba uteuzi wa Prof Kindiki wapasa kukataliwa kwa vile haujaidhinishwa na tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC).
“Hakuna makamishna wa IEBC na kwamba uidhinishwaji wa Prof Kindiki na IEBC na tume huru ya kupambana na ufisadi (EACC) umekinzana na katiba,” mawakili Muite, Macharia pamoja na wakili wanaowakilisha Diwani Benjamin Munyi Mathenge.
Mathenge anawakilishwa na mawakili Kibe Mungai na Ndegwa Njiru.
Wakili Teresia Wanjiru na walalamishi wengine 27 wamelalamika kwamba Bw Gachagua hakuondolewa afisini kwa njia inayofaa.
Mahakama iliombwa isitishe uteuzi wa Prof Kindiki kwa vile hajajiuzulu wadhifa wa Uwaziri.
Pia wamelalama maoni ya wananchi hayakusakwa kabla ya kuteuliwa kwa Prof Kindiki.
Lakini Prof Githu Muigai, Prof Tom Ojienda na mawakili Ben Millimo, Peter Wanyama, Paul Nyamondi, Dkt Muthomi Thiankolu na Eric Gumbo waliomba mahakama iamuru Prof Kindiki aapishwe kwa vile aliteuliwa kwa mujibu wa sheria.
Prof Ojienda alieleza majaji hao kwamba “uamuzi wa Gachagua kubaduliwa mamlakani na Bunge la Seneti hauwezi kubatilishwa na mahakama kuu.”
Mawakili Prof Muigai, Prof Ojienda na mawakili Millimo, Nyamondi na Wanyama walisema mahakama kuu haina uwezo wa kubatilisha uamuzi wa Bunge la Seneti na kwamba “Bw Gachagua afungashe virago aende nyumbani. Hawezi pata msaada na usaidizi kortini.”
Dkt Thiankolu alisema mahakama kuu haiwezi kuhoji uamuzi wa suala la Rais na Naibu Rais ila Mahakama ya Juu tu.
“Ni Mahakama ya Juu tu iliyotunukiwa mamlaka ya kujadilia suala la nyadhifa za Rais na Naibu Rais. Futilieni mbali maagizo ya Majaji Mwita na Mwongo ya kusitisha kuapishwa kwa Prof Kindiki kutwaa wadhifa wa Naibu Rais,” Dkt Thiankolu alisema.
Majaji hao walielezwa na Prof Muigai kwamba maamuzi ya Majaji Mwita na Mwongo yametumbukiza nchi hii katika utata wa kikatiba kwa vile “nchi haina Naibu Rais na Waziri wa Usalama.”
Majaji hao waliombwa wasisite kutekeleza sheria jinsi ilivyo kwa kuamua hawana mamlaka ya kuamua iwapo Bw Gachagua aling’atuliwa mamlakani kwa mujibu wa sheria.