Jamvi La Siasa

Ruto anavyobomoa umaarufu wa Raila

Na BENSON MATHEKA May 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

USHIRIKIANO wa kiongozi wa ODM Raila Odinga na Rais William Ruto unaonekana kubomoa sio tu uthabiti wa chama chake bali umaarufu na sifa za waziri mkuu huyo wa zamani ambaye kwa miaka mingi aliheshimiwa kama mtetezi wa haki na demokrasia.

Hatua ya kushirikiana na serikali, iliyoonekana kama ya mabadiliko ya kimkakati kwa upande wa Raila, imeibua hisia tofauti ndani ya chama, huku baadhi ya viongozi wakisema ni mkakati wa Ruto kumfifisha.

 “Kila dalili zinaonyesha kuwa ushirikiano wa UDA na ODM ni pigo kwa Raila. Chama chake kimekumbwa na misukosuko ya ndani, ngome zake zinabomoka na sifa zake za miaka mingi kama mtetezi wa haki zimemomonyoka miongoni mwa raia,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.

Japo Raila anasisitiza kuwa ushirikiano huo si wa kisiasa bali wa maslahi ya taifa, baadhi ya viongozi wa ODM wanauchukulia kama hatua ya kufifisha nguvu za chama, upinzani na kutoa nafasi kwa serikali ya Kenya Kwanza kujiimarisha zaidi kisiasa.

Raila amekuwa akisisitiza  anataka kuhakikisha kuwa masuala muhimu kwa Wakenya, kama vile gharama ya maisha, utawala bora na uwajibikaji, yanashughulikiwa kwa njia ya mazungumzo ya wazi na ya heshima.

Baadhi ya viongozi wa ODM wamejitokeza hadharani kuunga mkono hatua ya Raila kushirikiana na Ruto akiwemo kaka yake Oburu Odinga, Mbunge wa Homa Bay Town, Peter Kaluma, wenzake wa Rarieda Sam Atandi na Junet Mohamed wa Suna Mashariki ambaye ni mmoja wa wandani wa karibu wa Raila.

Katibu Mkuu wa ODM na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna na Gavana wa Siaya James Orengo amekuwa mstari wa mbele kukemea kile anachokiita “usaliti wa kisiasa:

“Ikiwa jambo ni baya, ni baya. Tusiwe watu wa kuendeshwa na tamaa ya mamlaka au vyeo,” Sifuna na viongozi vijana wa ODM kama Babu Owino na Caleb Amisi wamekuwa wakisema wakipinga ushirikiano huo.

Bw James Orengo, ambaye kwa muda mrefu amekuwa mfuasi wa Raila,  amekuwa akikosoa ushirikiano huo kiasi cha kutengwa na wanaoutetea.

“Kwa viongozi kama Orengo, kushirikiana na Ruto kunamaanisha kuwasaliti wananchi waliowachagua kama sauti ya upinzani. Wanahofia kuwa ODM inageuka kuwa ‘kivuli cha serikali’ badala ya kuwa sauti mbadala ya kuikosoa serikali iwajibike. Migogoro kama hii ni tishio kwa sifa za Raila,” asema Gichuki.

Kwa miaka mingi, asema, Raila Odinga amejijengea taswira ya mtetezi wa demokrasia, utawala bora na haki za wananchi. Hata hivyo, ushirikiano huu mpya umeanza kuufuta polepole wasifu huo.

“Kwa sasa, Raila anaanza kuonekana kama kiongozi anayetanguliza maelewano ya kibinafsi  kuliko mapambano jambo ambalo limewafanya baadhi ya wafuasi wake kuhoji dhamira yake,” aeleza.

Ngome za Raila, hasa katika maeneo ya Nyanza na Magharibi mwa Kenya, zimeanza kuonyesha dalili za kumhepa. Viongozi wa maeneo haya wamegawanyika, huku baadhi wakimfuata Ruto moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupitia ushirikiano.

Paul Bulindi, mchanganuzi wa siasa anatoa mfano wa Kisii ambapo hata viongozi wa ODM walimchangamkia aliyekuwa waziri wa usalama wa ndani kama kubomoka kwa ngome za Raila.

“Sio hii peke yake, kuna manung’uniko. Hata kule Nyanza kwenyewe, kuna wale wasiofurahishwa na kupenya kwa Rais Ruto akitumia jina la Raila,” asema.

Jana, mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga alionya viongozi wa UDA dhidi ya kuteka mazishi ya mbunge wa Kaspul Charles Were akisema Homa Bay ni ngome ya ODM.

Kufuatia ushirikiano wake na Ruto, Raila amepoteza washirika wake wa zamani na vigogo wa upinzani.

“Kwa sasa, vigogo wa upinzani akiwemo rais mstaafu Uhuru Kenyatta, Kalonzo Musyoka, Martha Karua na wengine waliokuwa naye katika Azimio la Umoja One Kenya wamejitenga naye. Ruto amefaulu kumnyima imani ya vinara hao kimakusudi,” asema Dkt Bulindi.

Anaongeza: “Ndoa ya kisiasa ya Ruto na Raila ilikuja wakati ambao vijana walikuwa wameuawa wakipigania haki na kulalamikia sera za ushuru za serikali ambayo anaunga sasa. Kuunga serikali iliyowachukiza, kuwaua na kuwateka nyara bila kutatua shida zao kulimtenga na kizazi hiki,” asema.

Kwa sasa, Raila ana jukumu kubwa la kuthibitisha kuwa bado ana ushawishi wa kisiasa, uwezo wa kuunganisha chama chake, na nia ya kweli ya kuwatetea Wakenya.

Bila hilo, asema Bulindi, historia inaweza kumbeba kama kiongozi aliyebomolewa na mpinzani wake kwa kutumia silaha ya ushawishi, mazungumzo na ujanja wa kisiasa.