Ruto anavyojaribu kutikisa ngome ya Kalonzo
Ziara ya Rais William Ruto katika eneo la Ukambani wiki hii inaonekana kuwa mkakati uliopangwa kwa ustadi wa kisiasa kupenya ngome ya muda mrefu ya kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka.
Wiki hii, Rais alizuru kaunti za Machakos, Makueni na Kitui, akizindua miradi ya maendeleo na kuendeleza ujumbe wake kwamba jamii ya Wakamba “haiwezi tena kubaki upande wa upinzani.”
Katika ziara yake ya Makueni, Ruto alizindua barabara na miradi ya maji, sambamba na ahadi za kuharakisha utoaji wa hatimiliki za ardhi kwa mamia ya wakazi.
Alisema kuwa Ukambani limekuwa nyuma kwa muda mrefu na kwamba ushirikiano na serikali yake ndio njia ya kufungua fursa za kiuchumi. Aliisema hii inawezekana kupitia maendeleo badala ya kubaki mateka wa siasa zinazowazuia kunufaika na rasilimali za serikali.
Wachambuzi wa siasa wanasema ziara hii ni juhu za kupenya katika ngome ya mmoja wa wapinzani wake wakuu kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Eneo hilo limemuunga mkono kiongozi wa wiper Kalonzo Musyoka kwa zaidi ya miaka 20. Ingawa Rais amekuwa akisisitiza kwamba ziara hizo ni za maendeleo, wachambuzi wanasema kuwa ujumbe wa kisiasa uko wazi katika kila hotuba na kila ahadi aliyotoa.
Katika baadhi ya hafla, viongozi kadhaa wa eneo hilo wakiwemo wale wa Wiper walionekana kuchangamkia mikutano ya Rais, hatua iliyozua gumzo kuhusu iwapo siasa za Ukambani zinaanza kupata sura mpya.
Mchanganuzi wa siasa, Mike Kimeu anataja ziara hiyo kama mkakati wa Ruto kumshinikiza Kalonzo kujitetea nyumbani badala ya kupanua ushawishi wake kitaifa hasa baada ya washirika wa makamu rais huyo wa zamani kuhudhuria hafla za Rais.
“Ruto anachofanya Ukambani si maendeleo pekee. Ni kupenya katika ngome ya Kalonzo. Anataka atumie muda nwingi katika ngome yake kujitetea na kumfanya ashughulike na siasa za eneo hilo, badala ya kujiimarisha kama mgombea wa urais wa 2027 kote nchini,” asema.
Hata hivyo, anasema inaweza kuwa vigumu kuvunja ushawishi wa Kalonzo kwa kuwa Rais hakugusia masuala halisi yanayoathiri wakazi.
Kulingana na mchambuzi wa siasa Caroline Mutua mkakati huu unalenga kuvutia maeneo yanayoonekana kuwa nje ya serikali kwa muda mrefu.
“Rais anatumia miradi ya serikali kama chambo kuwashawishi wananchi,” anasema. “Barabara, maji, hospitali—hivi ni vitu vinavyogusa maisha ya watu. Anatoa taswira kwamba ushirikiano na serikali unaleta matokeo ya moja kwa moja, na kwamba kuwa katika upinzani hakufaidi,” asema.
Anasema japo Ukambani imekuwa ngome thabiti ya kisiasa ya Kalonzo, Ruto anajaribu kuwasilisha serikali yake kama mshirika mkuu wa maendeleo, Kalonzo naye anatarajiwa kuongeza kasi ya kampeni ili kuhakikisha kuwa ngome yake haitikisiki.
“ Anachofanya Rais ni kuzua mgongano wa ushawishi kati ya Ikulu na Wiper lakini itakuwa vigumu kuyumbisha ngome hiyo bila mabadiliko ya sera,”asema Kimeu.
Kinachosubiriwa, asema, ni iwapo mkakati wa Ruto utaweza kupenya ndani ya moyo wa wapiga kura wa Ukambani, au iwapo Kalonzo ataendelea kushikilia ngome yake bila kuyumba.
“Ni wazi kuwa mkakati wa Ruto una sura mbili kuu. Kwanza, anajenga picha ya Ukambani kama sehemu ya serikali ili kuvutia wananchi ambao wanataka kuona maendeleo ya haraka. Pili, anajaribu kusababisha mgawanyiko wa kimkakati ndani ya Wiper, kwa kuwa baadhi ya viongozi wa eneo hilo wamekuwa wakijitokeza katika hafla zake na hivyo kuanzisha gumzo kuhusu msimamo wao wa kisiasa,” asema Mutua