Jamvi La Siasa

Sababu za Wamuchomba kujipanga nje ya UDA

Na  BENSON MATHEKA February 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Malkia wa siasa za kaunti ya Kiambu, Mbunge wa Githunguri, Peninah Gathoni Wamuchomba, amekuwa wa kwanza kutangaza wazi kuwa hatatetea kiti chake kwa kutumia chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) au kukitumia chama hicho kugombea wadhifa wowote katika uchaguzi mkuu ujao.

Huku wabunge wengine wa UDA katika eneo la Mlima Kenya wakionekana kujivuta kutangaza msimamo wao, Bi Wamuchomba, amechukua hatua ya ujasiri, kama kawaida yake, kusema kwamba uhusiano wake na chama tawala umeharibika.

Na mbunge huyo ambaye amekuwa msitari wa mbele kukosoa utawala wa Rais William Ruto, pia ameashiria kuwa hatakuwa na haraka kujiunga na chama ambacho aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua anatarajiwa kutangaza kati kati ya mwaka huu.

Ikizingatiwa kuwa mbunge huyo amekuwa mmoja wa washirika wakuu wa Bw Gachagua aliyesimama naye wakati na baada ya kutimuliwa kwake, kauli yake ya kutochangamkia chama cha mbunge huyo wa zamani wa Mathira inaacha maswali mengi kuhusu mwelekeo anaopanga kabla ya uchaguzi kuu wa 2027.

Hii ni kwa sababu amekuwa mmoja wa washirika ambao wamekuwa wakikutana nyumbani kwa Gachagua kijijini Wamunyoro, Nyeri, kuweka mikakati ya kuunganisha Mlima Kenya.

“Nina maoni tofauti kuhusu suala la Wamunyoro. Nitaungana na yeyote atakayekuwa na matarajio sawa na yangu kuhusu serikali ijayo. Kwa hiyo, akija na kuniambia, ‘nina chama hiki cha kisiasa ambacho kitaleta ninachopigania,’ nitakuwa huru kufanya uamuzi wangu. Lakini kwa sasa, ninatazama, ‘alisema.

Matamshi ya Wamuchomba yanajiri huku kukiwa na minong’ono kuhusu uwezekano wa kuibuka mabadiliko ya kisiasa, hasa katika eneo la Mlima Kenya, ambapo Gachagua anajipanga kuwa kinara.Alichotangaza wazi mbunge huyo ni kwamba hatatumia UDA katika uchaguzi mkuu ujao akisema chama hicho kimesaliti raia wa nchi kwa kukosa kutimiza ahadi za uchaguzi, kuwabebesha mzigo wa ushuru, kubagua baadhi ya maeneo na kuteka nyara na kuua vijana kwa kuitisha utawala bora.

Kuteka na kuua wanangu

“Sitagombea tena kwa tiketi ya UDA, hilo lazima niliweke wazi. Iwapo nitagombea wadhifa wowote nitakaogombea Mungu akipenda, sitatumia UDA maana UDA imenisaliti. Sikumfanyia kampeni Rais Ruto kuwa rais wangu kuwateka na kuwaua wanangu wa kiume na wa kike.

Sikufanya kampeni na kumwidhinisha rais wangu kuvamia mishahara ya watu na kuwalazimishia makato makubwa ya lazima. Na ndio maana unaona mimi ninampinga Bungeni, kwa sababu naamini kila anachofanya anakifanya kivyake. Hajanipa nafasi nimshauri kama mmoja wa wale waliokuwa wafuasi wake wakuu na waliopigia kampeni,” alisisitiza.

Akizungumza kutoka Boston, Marekani wakati wa mahojiano na kituo kimoja cha televisheni cha humu nchini mnamo Jumatano, Februari 12, 2025, Wamuchomba aliweka wazi kwamba atapima iwapo chama atakachotangaza Gachagua kitakuwa na maono sawa na yake.

Japo hakutangaza iwapo hatatea kiti chake, machapisho yake katika mitandao ya kijamii yamekuwa yakidokeza kuwa kiongozi mwanamke anaweza kufanya kazi bora katika wadhifa mkubwa kupitia heshitegi #womanforthejob.

“Nilichaguliwa chini ya chama cha UDA. Chama kilichonifadhili Bungeni ni UDA, kwa hiyo bado niko UDA. Lakini sikumwomba Rais Ruto aende kuungana na ANC. Na kwa hivyo, kwa sababu kuna muungano, tutasubiri kuona ikiwa Rais Ruto atautangaza kwenye gazeti rasmi la serikali ili tuweze kutangaza misimamo yetu kwa sababu hatukumpa mamlaka ya kufanya hivyo,” akasema.

Rais Ruto amebadilisha nia ya kuunganisha chama cha ANC na UDA na badala yake chama kinachohusishwa na mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi kitavunjwa na wabunge wake kujiunga na UDA.

“UDA iliingia na kutuambia kuwa tutakuwa na ‘pesa mfukoni.’ Ilituambia kuwa tutakuwa na uhakika wa kupata mapato ya chini. Mapato hayo yalienda wapi kwa wakulima wangu wa kahawa na parachichi? Kwa hiyo, natamka kuwa nimemalizana na UDA inapohusu uchaguzi ujao. Niko UDA hivi sasa kwa sababu nilifadhiliwa na chama katika Bunge la Kitaifa, lakini sikubaliani na sera nyingi walizotoa za kukandamiza uchumi na maisha ya watu wa Kenya,” alisema.