Sababu za washirika wa Gachagua kuenda matao ya chini dhidi ya kumpiga vita Kindiki
WASHIRIKA wa Rigathi Gachagua wanaepuka makabiliano ya moja kwa moja na Naibu Rais Kithure Kindiki ili kutotumbukia mtego wa wanaounga Rais William Ruto ambao wangefurahia vita hivyo vya ubabe wa kisiasa.
Huku wakazi wa Mlima Kenya wakiwa na chuki na Rais kwa kumtimua Bw Gachagua kama naibu wake, mrengo wa naibu huyo wa zamani umeamua kutojiingiza katika mtego wa kuzua mgawanyiko kati ya Mlima Kenya Mashariki na Magharibi.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mhadhiri wa chuo kikuu Profesa Peter Kagwanja, anasema ni mbinu ya kimkakati katika jinsi mrengo wa Bw Gachagua unavyomshughulikia Prof Kindiki na kukataa kuingizwa kwenye mtego wa kumchukia.
“Mrengo wa Gachagua unakabiliwa na hali ngumu kumhusu Kindiki. Prof Kindiki anatoka eneo la mlima ambalo Bw Gachagua anatoka, huku akiwakilisha Mlima Kenya Mashariki. Ni Mlima Kenya Mashariki ambao wanamikakati wa Ikulu wanataka kutumia katika ajenda yao ya 2027. Kwa kambi ya Gachagua kushambulia Kindiki, itamaanisha wanasaidia Ikulu kufaulu,” Prof Kagwanja anahoji.
“Mrengo wa Bw Gachagua hauna mbinu mbadala ya kukabiliana na Prof Kindiki isipokuwa kukubali hali halisi, kujifunza kumpenda na kumuunga mkono,” anaongeza.
Seneta John Methu (Nyandarua), Joe Nyutu (Murang’a) pamoja na wabunge Onesmus Ngogoyo (Kajiado Kaskazini), Benjamin Gathiru (Embakasi ya Kati), Gathoni wa Muchomba (Githunguri) na Njeri Maina (Mwakilishi kike wa Kirinyaga), wanasisitiza hawana shida na Prof Kindiki ila wanapinga tu wale wanaopanga kugawanya eneo la Mlima Kenya.
“Hatuna shida na Prof Kindiki. Nathubutu kusema ni mtoto mzuri, mnyenyekevu na anayejitolea kutoka Mlima Kenya. Tunamtakia kila la kheri. Shida yetu ni wale wanaomtumia katika mpango wa kugawanya na kutawala,” akasema Bw Methu.
Seneta huyo aliongeza, “Hata Kindiki akituita kwa mkutano wa mashauriano kama viongozi wa Mlima Kenya, tutaenda. Hata tukialikwa na Gachagua, tutaenda pia kwa sababu hatumchukii.”
Bw Ngogoyo pia aliambia Taifa Leo kwamba, “shida haiko kwa Prof Kindiki, ni mtu mzuri na kiongozi aliyejitolea”.
“Sisi tunaomuunga mkono Bw Gachagua tuna jukumu la kuunga mkono Prof Kindiki kama mmoja wetu. Mwanamume ambaye atakuwa akifanya kazi chini ya hali ngumu ya kuamriwa na badala ya kumchukia, tunamhurumia,” Bw Ngogoyo aliongeza.
“Tumuache mtoto wetu afurahie maisha yake kama Naibu Rais huku tukimuunga mkono Bw Gachagua wetu. Hatutamuingilia Prof Kindiki na akianza kutengwa, tutamtetea,” Bw Nyutu aliambia Taifa Leo.
Bw Nyutu aliongeza kuwa “kama mrithi anayetambuliwa wa urais ikiwa afisi ya juu zaidi itabaki wazi, Prof Kindiki anatuletea uwezo mkubwa kutokana na kuwa karibu na ofisi kuu nchini.”
Bi Wa Muchomba alisema Mlima Kenya umeungana kumheshimu Prof Kindiki lakini “si wale ambao wamekuwa wakijaribu sana kuugawanya mlima.”
Bi Maina pia alisema tatizo si Prof Kindiki bali ni wale wanaolenga kugawanya mlima.