Jamvi La Siasa

Sadaka ya Ruto ya mamilioni ya pesa kwa makanisa mawili yaibua mjadala mkubwa

Na CECIL ODONGO November 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

WAKENYA wanapoendelea kunyanyasika na uchumi mbaya, Rais William Ruto na naibu wake Prof Kithure Kindiki walitoa sadaka ya Sh12.8 milioni katika ibada za Nairobi na Kirinyaga mnamo Jumapili.

Rais William Ruto alihudhuria ibada ya Jumapili katika Kanisa Katoliki la Soweto eneobunge la Embakasi Mashariki viungani mwa jiji la Nairobi.

Kwenye ibada hiyo, Rais aliandamana na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah, japo mbunge wa eneo hilo Babu Owino, mpinzani mkuu wa serikali, alikosa kuhudhuria hafla hiyo.

Kwa upande mwingine, Prof Kindiki alihudhuria ibada ya kanisa la AIPCA eneo la Karima, eneobunge la Ndia, Kaunti ya Kirinyaga akiwa ameandamana na wanasiasa kutoka eneo la Kati.

Umoja wa nchi

Nairobi, Rais Ruto alipigia debe umoja wa nchi akiomba kanisa liungane naye katika kuhakikisha kuwa taifa hili linapiga hatua kimaendeleo.

Pia alitoa ahadi ya kusaida ujenzi wa shule ya chekechea eneo la Soweto, shule ya msingi, upili, taasisi ya mafunzo, nyumba za gharama nafuu na uwanja wa sasa wa soka.

Alipomaliza, Rais aliagiza kasisi wa kanisa hilo aende akapokezwe Sh5 milioni katika afisi yake Jumatatu (jana) au leo za kugharimia ujenzi wa nyumba ya padri huku akiwaachia watoto na Sh300,000 za kununua sare. Aliipa kwaya Sh500,000.

“Watoto hawa nitawatafutia Sh300,000 sasa hivi tuwanunulie sare na kwaya pia niwanunulie sare nyingine mpya kabla sijatoka hapa lakini kazi yenu ni kuimbia Mungu si binadamu,

“Mwenyekiti Isanda ameniambia mnajenga nyumba ya padri hapa na mimi ni mtu wa kujenga na ninaelewa. Bw Isanda utakuja kuniona Jumatatu au Jumanne nitakutafutia Sh5 milioni,”akasema Rais Ruto.

“Hiyo pesa nitaifuatilia. Ukipiga kona hivi kidogo utakutana na mimi, si ulisikia mimi ni mtu wa mambo matatu? Nimeambiwa pia mnataka basi, nikirudi Januari nitarudi na basi lenu,” akaongeza Rais.

Maoni ya kuikosoa

Naibu Rais akiwa Kirinyaga alisema kuwa serikali iko tayari kupokea maoni ya kuikosoa ili kuisadia kujenga Kenya bora, thabiti na usalama.

Prof Kindiki baada ya hotuba yake alitoa sadaka ya Sh5 milioni ambazo alisema ni kutoka kwa Rais kisha akatoa Sh2 milioni kusaidia katika ujenzi wa kanisa la AIPCA.

“Mnajua mambo ya harambee tulisimamisha kwa sababu wanasiasa walikuwa wakiitumia harambee kufanya mambo yao. Hata hivyo, mambo ya kutoa sadaka haijafungwa na hakuna sheria inayozuia hiyo kwa sababu hiyo ni amri ya Mungu.

“Nimetumwa na sadaka ya Rais ya Sh5 milioni na wanahabari mwelewe sadaka ndiyo tunatoa hatushiriki harambee. Nami nina sadaka pia hata kama nilikuwa nimebeba ya mkubwa wangu na ninatoa Sh2  yangu,” akaongeza Prof Kindiki.

Naibu Rais alisema yuko tayari kusaidia katika ujenzi wa makao makuu ya AIPCA akimwambia Askofu Fredrick Wang’ombe kuwa yuko tayari kutuma pesa zaidi iwapo kutakuwa na upungufu wowote.

“Makao haya makuu tunajenga na nyinyi. Simiti ikipungua, niambieni. Si M-Pesa, Paybill na nambari ya akaunti iko? Nilizaliwa katika familia ya uchungaji na naelewa mambo ya makanisa,” akasema.

Mchango huo mkubwa kwa siku moja unakuja wakati ambapo kuna marufuku ya harambee ambayo ilitolewa na Rais Ruto mnamo Julai 5, 2024.

Maandamano ya Gen Z

Marufuku hiyo ilitolewa wakati wa maandamano ya Gen-Z nchini, vijana wakilalamikia hatua ya wanasiasa kutoa michango mikubwa huku Wakenya wakiendelea kuumia kutokana na maisha ya magumu.

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa kisiasa Herman Manyora, kutolewa kwa pesa hizo nyingi ni njama ya kunyamazisha kanisa ambalo limeanza kupinga serikali kutokana na dhuluma dhidi ya raia na utawala mbovu.

“Mbona mara moja wakaanza kutoa pesa nyingi hivyo? Ni kuwatuliza viongozi wa kanisa na waumini ambao watakuwa wakiona wanasaidiwa kumaliza miradi ya kanisa ambayo imekwama,” akasema Bw Manyora.

Kuhusu Prof Kindiki, mhadhari huyo wa Chuo Kikuu cha Nairobi anasema Rais ana nia ya kumpigia debe Mlima Kenya ili kupunguza upinzani ambao upo baada ya kutimuliwa kwa Rigathi Gachagua.

“Ruto alipenya Mlima Kenya akitumia makanisa na anajaribu kutumia hilo kuvumisha Prof Kindiki ambaye ni dhahiri hashabikiwi kutokana na jinsi Gachagua alivyohangaishwa,” akaongeza Bw Manyora.