Jamvi La Siasa

Safari ngumu ya upinzani kuelekea 2027

Na BENSON MATHEKA January 4th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

BAADA ya aliyekuwa kiongozi wa ODM, marehemu Raila Odinga kuondoka katika ulingo wa kisiasa, upinzani nchini Kenya umejipata katika kipindi kigumu, ukijaribu kujifunza kutembea bila nguzo yake kuu.

Raila hakuwa tu sura ya upinzani, bali alikuwa kiunganishi, mpatanishi na sauti iliyovutia mamilioni ya wafuasi. Kuondoka kwake kuliacha pengo kubwa kisiasa na vyama pamoja na miungano mipya sasa vinajaribu kulijaza.

“Marehemu Raila Odinga hakuwa tu nembo ya upinzani wa Kenya; alikuwa uti wa mgongo wake. Siasa zake ziliunganisha maandamano na matumaini,” anasema mchambuzi wa siasa Dismas Mokua.

Anaongeza kuwa bila Raila, upinzani unalazimika kujiunda upya bila nguzo iliyokuwa ikiufanya kuonekana kuungana.

Katika ombwe hilo, kile kinachojitokeza ni muungano mpana lakini dhaifu wa upinzani unaojumuisha vinara kadhaa.

Miongoni mwao ni kiongozi wa Democracy for the Citizen’s Party (DCP) Rigathi Gachagua, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta anayewakilishwa na naibu kiongozi wa Jubilee Dkt Fred Matiang’i, kiongozi wa Wiper Patriotic Front Kalonzo Musyoka, Kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, Justin Muturi wa Democratic Party na Martha Karua wa People’s Liberation Party (PLP).

Pia wapo Jimi Wanjigi wa Safina Party, Peter Munya wa PNU, Moses Kuria wa Chama Cha Kazi, Lenny Kivuti wa Devolution Empowerment Party, Ferdinand Waititu wa Farmers Party na The National Party inayohusishwa na Patrick Wainaina ‘Wa Jungle’.

Anayezua mjadala mkubwa ni aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko na chama chake kipya cha National Economic Development Party (NEDP) ambaye mtindo wake wa siasa unavutia watu wa kawaida.

Ingawa vyama vingi vimeapa kushirikiana kumpinga Rais William Ruto na chama chake cha UDA, ambacho sasa kinashirikiana na ODM inayoongozwa na Seneta wa Siaya Dkt Oburu Oginga,baadhi ya wanachama wa upinzani wanafuata mkondo wao binafsi.

Hata hivyo, mshikamano unaoonekana katika mrengo unaoongozwa na Gachagua na Kalonzo ndio unaotia serikali wasiwasi.

Hii ni kwa kuwa vinara wote wanakubaliana kuwa upinzani uliogawanyika hauwezi kushindana na uwezo wa serikali iliyo imara.

Ndiyo maana lugha ya umoja na miungano sasa inatawala mikutano ya upinzani. Lengo ni moja: kujenga ngome imara ya kisiasa itakayoweza kutwaa mamlaka 2027.

Kulingana na utafiti wa Infotrak kuhusu mwelekeo wa kisiasa, mrengo wa serikali unaongozwa na Rais Ruto na Dkt Oginga bado unaongoza kwa asilimia 32.

Muungano wa upinzani unaoongozwa na Gachagua na Kalonzo unafuata kwa asilimia 22, huku Kenya Moja ya kina Edwin Sifuna, Babu Owino na Gathoni Wa Muchomba ikipata asilimia 17.

Asilimia 29 ya Wakenya hawajajitambulisha na muungano wowote.

Dkt Oginga ametangaza kuwa ODM ina chaguo tatu: kuendelea na muungano na UDA, kuunda ushirikiano mpya au kuwa pekee yake. Ameonya kuwa uamuzi huo lazima ufanywe mwaka huu, la sivyo chama kitaingia katika mgawanyiko unaoweza kudhoofisha nguvu zake katika uchaguzi.

Kwa upande mwingine, Muungano wa Upinzani umeweka Machi 2026 kama tarehe ya kutangaza mpeperusha bendera ya urais. Kalonzo Musyoka tayari ametangaza nia yake, akisema ana idhini ya chama chake.

Lakini pia wapo Gachagua, Matiang’i, Karua, Wamalwa, Muturi na Munya, hali inayoashiria ushindani mkali wa ndani.

Nje ya muungano huo, wagombea wengine wa urais kama Jimi Wanjigi, Boniface Mwangi, Seneta Okiya Omtatah na aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga wanazidi kuibuka, na kufanya uwanja wa 2027 kuwa wenye msongamano mkubwa.

Wachambuzi wa siasa wanaonya kuwa hatari kubwa kwa upinzani si ukosefu wa wagombea, bali kushindwa kukubaliana mapema kuhusu mgombea mmoja.

Mchambuzi wa siasa Martin Oloo anasema historia ya Kenya inaonyesha kuwa ushindi wa urais haujawahi kupatikana bila muungano mpana kama NARC mwaka 2002.

Profesa Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multimedia anasema kuwa Rais Ruto anakabiliwa na njia finyu kuelekea uchaguzi wa 2027 kutokana na migawanyiko Mlima Kenya na kutoridhika kwa vijana.

Anaonya kuwa bila kushughulikia malalamishi ya kiuchumi na kisiasa, mrengo wa serikali unaweza kukabiliwa na upinzani mkali.

Kwa sasa, mustakabali wa upinzani utategemea kama vinara wapya wataweza kudumisha umoja wao bila Raila Odinga na kama watapata kiongozi mmoja mwenye mvuto wa kitaifa atakayewaunganisha Wakenya kuelekea 2027.