Suluhu aruhusu Maraga kuingia TZ kwa kesi ya Lissu huku akizima Karua, Mutunga
SIKU moja baada ya kiongozi wa chama cha People’s Liberation Party (PLP) Martha Karua kufurushwa nchini Tanzania alikoenda kumwakilisha kiongozi wa upinzani Tundu Lissu mahakamani, Jaji Mkuu wa zamani David Maraga amehudhuria kutajwa kwa kesi hiyo.
Jumatatu, Mei 19, 2025 Bw Maraga alitangaza kuwasili kwake katika taifa hilo jirani kuhudhuria kesi dhidi ya kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
“Nimewasili salama jijini Dar es Salama. Naelekea mahakamani kuhudhuria kesi dhidi ya Tundu Lissu,” Bw Maraga akasema kwenye taarifa fupi kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X. Aliambatisha ujumbe huo na picha yake akiwa pamoja na mwanaharakari wa kutetea haki za kibinadamu na mbunge wa zamani wa Ndhiwa Agostino Netto.
Bw Lissu aliwasilisha katika Mahakama ya Kisutu Mei 19 kwa mara ya kwanza tangu kukamatwa kwake mnamo Aprili 9, mwaka huu.
Mwanasiasa huyo anakabiliwa na mashtaka ya uhaini na tuhuma za kuchochea raia wa Tanzania kususia uchaguzi mkuu ambao umeratibiwa kufanyika mnamo Oktoba mwaka huu. Bw Lissu, kupitia chama chake cha Chadema, amekuwa akishinikiza mageuzi ya sheria ya uchaguzi akisema sheria ya sasa inapendelea chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) chake Rais Samia Suluhu Hassan.
Mnamo Jumapili, Bi Karua aliilaani na kuikashifu serikali ya Rais Suluhu kwa kumzuia kuingia Tanzania na kumrejesha Kenya kwa nguvu, akidai hatua hiyo ni ukiukaji wa haki zake kama raia wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Waziri huyo wa zamani wa Haki na Masuala ya Kikatiba alidai masaibu yaliyomfika ni sehemu ya juhudi za viongozi wa mataifa wanachama wa EAC kuwanyanyasa viongozi wa upinzani na wafuasi wao.
“Kama raia wa Jumuiya ya Afrika Mashariki sitachoka kupinga udhalimu huu ambao ni tishio kwa undugu kati yetu kama wananchi,” akasema Jumapili jioni alipowasili katika uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi.
Bi Karua, ambaye alikuwa ameandamana na wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu Gloria Kimani na Lynn Ngugi, alikuwa amesafiri Tanzania kwa mwaliko wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki (EALS), kwa ajili ya kumtetea Bw Lissu mahakamani.
Mnamo Jumatatu, Mei 19, 2025 aliyekuwa Jaji Mkuu nchini Kenya Willy Mutunga na watetezi wa haki za kibinadamu Hussein Khalid na Hanifa Adan walizuiwa walipofika katika uwanja wa kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salam, Tanzania.
Wao pia walipanga kuhudhuria kikao cha mahakama ambapo kesi dhidi ya Lissu ilitajwa.
Katibu wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Kenya Korir Sing’Oei alilaani kuzuiliwa kwa Dkt Mutunga na wenzake akisema kuzuiliwa kwao ni kinyume na kanuni za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Tunawataka maafisa wa Tanzania wamwachilie aliyekuwa Jaji Mkuu wa Kenya Dkt Willy Mutunga na ujumbe wake, kulingana na kanuni zinazoongoza mahusiano kati ya mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” Dkt Sing’Oei akaeleza kwenye taarifa fupi kupitia akaunti yake ya mtandao wa X.
Baada ya Bw Lissu kukamatwa kwa uhaini na kuwachochea Watanzania kususia uchaguzi, Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi Nchini Tanzania iliizima chama chake, Chadema, kushiriki katika uchaguzi mkuu.
Hii ni kufuatia hatua ya chama hicho cha upinzani mnamo Aprili 12, 2025 kudinda kutia saini kanuni ya kuhusu mienendo bora wakati wa kampeni.