Jamvi La Siasa

Tahadhari, kambi yako imejaa fuko wa Ruto, Rigathi amshauri Matiang’i

Na BENSON MATHEKA January 18th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa chama cha Democracy for the Citizens (DCP), Rigathi Gachagua, amemuonya Naibu Kiongozi wa Chama cha Jubilee, Fred Matiang’i, kwamba huenda anazungukwa na watu waaminifu kwa Rais William Ruto wanaojifanya wanamuunga mkono.

Akiendelea kumuonya dhidi ya kutegemea vyama vya kisiasa vilivyoundwa na watu wengine, Bw Gachagua alisema kuwa watu wenye ushawishi waliowahi kufanya kazi naye wanaweza kuvuruga ndoto yake ya kisiasa.

Gachagua alikuwa naibu rais wa Rais Ruto kabla yao kutofautiana na akabanduliwa serikalini.

Akizungumza katika mahojiano na redio ya Kameme FM mnamo Jumatatu, Januari 13, 2026, Gachagua alisema Matiang’i yuko katika hatari ya kupoteza mwelekeo iwapo hataunda chama chake mwenyewe ili kudhibiti ngome yake ya kisiasa na kuwaweka wafuasi wake.

Haikuwa mara ya kwanza ya Gachagua kumshauri Matiangi kutotegemea Jubilee kuingia katika siasa, ushauri ambao Matiang’i hakufuata.

Gachagua alitumia fursa hiyo kueleza kwa nini anaamini kuwa na chama ni jambo la msingi katika siasa za Kenya na kwa nini Matiang’i anapaswa kuwa makini na washirika waliowahi kufanya kazi chini yake lakini sasa wako ndani ya chama cha Jubilee.

“Kwa upande wangu, sikujua kama angenisikiliza kwa sababu nilimpa ushauri, lakini si lazima afanye kile ninachomwambia. Nilimshauri aunde chama cha kisiasa ili aunganishe na kudhibiti ngome yake. Njia moja ya kuleta nidhamu katika eneo lolote ni kuwa na chama cha kisiasa; la sivyo watu watakudharau. Kwa mfano, ODM inasema haiwezi kumuunga mkono kwa sababu anatumia chama cha jamii fulani (Jubilee),” alisema Gachagua.

Alifafanua msimamo wake kuhusu vyama vya kisiasa na kupuuza madai kwamba ana uhasama na Jubilee au vyama vingine.

“Ningependa kusema wazi kuwa Riggy G hachukii chama chochote cha kisiasa. Tatizo ni kwamba siwezi kuvumisha vyama vya watu wengine. Waendelee kushikilia vyama vyao, hakuna atakayewazuia. Kama ni chama cha Jubilee, na wavumishe chama chao,” alisema.

Gachagua aliendelea kueleza kwa nini anaamini baadhi ya wanasiasa ndani ya Jubilee hawaaminiki, akiwahusisha na kambi ya Rais William Ruto na kuwatuhumu kwa kunyamaza wakati Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alipokuwa akishambuliwa.

“Hakuna vita baridi kati ya DCP na vyama vingine, ikiwemo Jubilee. Kinachoendelea ni kwamba kuna watu wa Ruto waliojificha ndani ya Jubilee. Kwa mfano, wakati Uhuru Kenyatta aliposhambuliwa na watu wa Ruto ndani ya ODM, hawa watu wa Jubilee walinyamaza kimya kabisa. Hakuna aliyezungumza hadi mimi mwenyewe nilipozungumza,” alisema.

Alisisitiza kuwa uaminifu wake kwa Uhuru Kenyatta uko thabiti na kwamba hatanyamaza kamwe rais huyo mstaafu anapodhalilishwa.

“Kazi yangu ni kumlinda Uhuru dhidi ya mashambulizi kutoka nje. Siwezi kudai nalinda jamii halafu nikae kimya nikiona Uhuru akitukanwa na watu walio karibu na Ruto. Nitaendelea kumtetea kwa sababu Uhuru amestaafu, ni mtu mwema, na hakuna siku nitanyamaza nikiona watu wakiendelea kumdharau mwana wetu,” alisema Gachagua.

Hata hivyo, alimuonya Matiang’i kufikiria upya watu anaofanya nao kazi iwapo anataka kufanikiwa kisiasa.

“Namwambia Matiang’i, watu hao walikuwa katika kambi yangu. Kama anataka kufika mbali, afikirie upya kuwahusu. Nawajua, na akiendelea nao, hataenda popote,” alisema.