Jamvi La Siasa

Uasi ODM viongozi wakisusia ziara Ikulu na kulazimu Oburu kwenda peke yake

Na JUSTUS OCHIENG’, MOSES NYAMORI December 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

UASI baridi umeibuka ndani ya chama cha ODM baada ya maafisa wake wakuu kususia mkutano wa Ikulu ulioitishwa na Rais William Ruto na wabunge wapya waliochaguliwa kupitia Serikali Jumuishi na kumuacha kiongozi wa chama hicho, Dkt Oburu Oginga, kuhudhuria mkutano huo peke yake.

Taarifa kutoka kwa maafisa mbalimbali waliozungumza na Taifa Leo zinaonyesha kuwa viongozi hao walijiondoa kimakusudi wakilalamikia kile walichokitaja kuwa kuingiliwa kwa chama na Ikulu, kupuuzwa kwa miundo ya uongozi na mvutano wa ndani, hasa katika siasa za Homa Bay.

Maafisa waliosusia hafla hiyo – Katibu Mkuu Edwin Sifuna, manaibu wa kiongozi wa chama Abdulswamad Nassir, Godfrey Osotsi na Gavana Simba Arati pamoja na Mkurugenzi Mtendaji Oduor Ong’wen – walikuwa wamehudhuria kikao cha asubuhi katika makao makuu ya Chungwa House siku hiyo, lakini hawakumsindikiza Dkt Oginga kwenda Ikulu.

Mwenyekiti wa chama, Gavana Gladys Wanga, hakuhudhuria kikao chochote.

Kususia kwao kulimuacha Dkt Oginga kuandamana na wabunge watatu wapya wa ODM, Boyd Were (Kasipul), Moses Omondi (Ugunja) na Harrison Kombe (Magarini), katika Ikulu ambako Rais Ruto aliwapokea pamoja na wabunge wapya wa UDA.

Kinyume chake, wabunge wapya wa UDA waliwasili wakiwa na kundi la viongozi kama Katibu Mkuu Hassan Omar, Mwenyekiti Cecily Mbarire, Mweka Hazina Japheth Nyakundi na Kiongozi wa Wengi Bungeni Kimani Ichung’wah.

Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, uamuzi wa ODM kususia ulitokana na “kosa la kiutaratibu”.

Inaelezwa kuwa Ikulu iliwapigia simu wabunge wateule moja kwa moja bila kupitia uongozi wa chama, na mwaliko rasmi ukatumwa baadaye tu baada ya wabunge kuarifu uongozi wa ODM.

“Mwaliko wa Ikulu ulitumwa baada ya wabunge kumjulisha Dkt Oburu,” afisa mmoja wa ODM alisema, akibainisha kuwa uongozi ulichukulia hatua hiyo kuwa jaribio la kudhoofisha chama kwenye kipindi kigumu cha mpito baada ya kifo cha Raila Odinga.

Uongozi wa ODM uliwazia kususia kabisa, wakihofia kuwa mkutano huo ungeonekana kama njama ya kuonyesha kuwa wabunge wa ODM wanaungwa na Rais Ruto kibinafsi na kupuuza chama.

Hata hivyo, inadaiwa kwamba mjumbe fulani wa serikali alikutana na Dkt Oginga binafsi na kumshawishi kuhudhuria akiwa na wabunge wateule.

Bw Arati, Bw Nassir, Bw Osotsi na Bw Sifuna, ambao wote walikuwa katika mkutano wa asubuhi, hawakufika Ikulu.

Bw Osotsi alisema shughuli za Seneti ndizo zilimzuia, akisema: “Sikuhudhuria mkutano wa Ikulu kwa sababu kulikuwa na jambo la dharura katika Seneti.”

Hata hivyo, Dkt Oginga, ambaye pia ni Seneta, hakuenda Seneti siku hiyo, jambo lililoongeza tetesi kuwa sababu za kutohudhuria hazikuwa ratiba bali mvutano wa ndani.

Bw Nassir alikanusha kuwa kulikuwa na mgawanyiko chamani. “Tuliitwa kwa chakula cha mchana Ikulu. Baadhi yetu hatukuweza kupatikana. Kutoenda hakumaanishi uasi,” alisema.

Alithibitisha kuwepo kwa kikao Chungwa House na kueleza kuwa alikuwa amefahamishwa kuwa Dkt Oginga angehudhuria.

“Tulikuwa na shughuli zilizotutangulia. Hakukuwa na njama yoyote,” alisema.

Hata hivyo, taswira ya kisiasa haikuwa nzuri kwa chama.

Katika upande wa Homa Bay, mvutano uliendelea kukua. Gavana Wanga hakuhudhuria mikutano yote miwili, hatua ambayo wadadisi wanasema inatokana na kutoridhishwa kwake na afisa mmoja mkuu wa serikali kutoka eneo la Nyanza ambaye anamlaumu kwa kufadhili maandamano ya kumpinga.

Katika uchaguzi mdogo wa Kasipul, hali ilikuwa mbaya zaidi. Naibu wa Gavana Wanga, Oyugi Magwanga, alimuacha mgombeaji wa ODM, Were na kumuunga mkono mgombeaji huru Philip Aroko.

Wanasiasa wa UDA pia walimuunga mkono Aroko licha ya makubaliano ya kitaifa kati ya Rais Ruto na ODM yaliyomtambua Were kama mgombeaji wa Serikali Jumuishi.

Mbunge wa Homa Bay Town, Bw Opondo Kaluma, aliwalaumu baadhi ya wanasiasa wa UDA kwa kukiuka makubaliano ya Rais Ruto na Raila Odinga.

“Kama tuko katika serikali jumuishi, kwa nini UDA inafanya kampeni dhidi ya mgombeaji wetu?” aliuliza.

Katika mkutano wa Ikulu, Dkt Oginga alisisitiza kuwa ODM imedhamiria kuona makubaliano ya vipengele 10 ya Serikali Jumuishi yakitekelezwa kikamilifu kabla ya uchaguzi wa 2027.

Aliwasihi viongozi wa ODM kuimarisha chama na kuonyesha uwezo wake ndani ya serikali.