Uasi wa Weta utakavyofifisha chama cha UDA kuelekea 2027
WIMBI jipya la uasi limechipuza ndani ya muungano wa Kenya Kwanza baada ya chama cha Ford Kenya, kinachoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula kutangaza kuwa kitadhamini wagombeaji katika chaguzi ndogo zijazo huku kikijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027.
Hayo yanajiri wakati ambapo tayari muungano huo umepata pigo kutokana na uasi uliochochewa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, aliyekuwa kiongozi wa chama cha Democratic Party (DP) Justin Muturi na katibu wa zamani wa wizara Irungu Nyakera, ambaye ni kiongozi wa Farmers Party.
Bw Gachagua ametangaza kuzindua chama kipya mwezi ujao na vyama vya Mabw Muturi na Nyakera vimeanza mchakato wa kujiondoa kutoka Kenya Kwanza.
Viongozi wa chama cha Ford Kenya, pia kimesisitiza kuwa hawatakiunganisha na chama cha United Democratic Alliance (UDA), kinachoongozwa na Rais William Ruto, bali kitaendelea kuwa chama huru.
Hatua hiyo ni kinyume cha ndoto ya Rais Ruto ya kuhakikisha kuwa vyama vyote tanzu katika muungano huo kujiunga na UDA ili kuipa sura ya kitaifa ili ishinde kwa urahisi katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Lakini Katibu Mkuu wa Ford Kenya John Chikati anashikilia kuwa itasalia chama huru ndani ya muungano wa Kenya Kwanza huku ikiendelea na mipango ya kujiimarisha kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
“Mkutano wetu wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) uliamua kuwa Ford Kenya haitavunjwa. Tutasalia chama huru na hivyo karibuni tutaaanza kampeni mpya ya kujiimarisha kupitia uandikishaji wa wanachama wapya tujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027,” akaeleza Mbunge huyo wa Tongaren.
“Hii ndio maana NEC pia imeamua kwamba Ford Kenya itadhamini wagombeaji katika chaguzi ndogo zijazo katika maeneobunge ya Malava, Ugunja na Banissa. Tayari tumetambua wagombeaji watakaopeperusha bendera ya Ford Kenya na tuweka mikakati itakayotuwezesha kushinda viti hivyo,” Bw Chikati akaeleza, akirejelea mojawapo ya maamuzi katika NEC ya Ford Kenya iliyofanyika Naivasha, mnamo Aprili 12.
Msimamo wa Ford Kenya unajiri miezi michache baada ya chama cha Amani National Congress (ANC) kilichoasisiwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi kuvunjwa na kujiunga na ANC.
Kufuatia hatua hiyo iliyoidhinishwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu Februari 8, mwaka huu, aliyekuwa kiongozi wa ANC Gavana Issa Timamy alitunukiwa wadhifa wa naibu kiongozi wa UDA sawa na Naibu Rais Kithure Kindiki.
Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanasema msimamo wa viongozi wa Ford Kenya wa kutokubali kuivunja, utamkera zaidi Rais Ruto ambaye analenga kutwaa udhibiti kamili wa kisiasa katika eneo la Magharibi mwa Kenya baada ya kuvunjwa kwa ANC.
“Bila shaka tangazo hilo la Ford Kenya limekwaza Rais Ruto na sasa atamsawiri Spika Wetang’ula kama mtu anayevuruga hesabu zake za kisiasa za kumwezesha kuhifadhi kiti chake cha urais. Sasa Wetang’ula ni muasi,” anasema Bw Martin Andati.
“Sababu ni kwamba, baada ya ANC kujiunga na UDA Rais alipata matumaini ya kuanzisha mchakato wa kupenya katika eneo la magharibi. Ndoto hiyo ingetimia kikamilifu iwapo Ford Kenya ingefuata nyayo za ANC kwa kujiunga rasmi na chama hicho tawala. Lakini sasa hilo halijawezekeza na Bw Wetang’ula sasa anasawiri kama ‘adui’ ndani ya Kenya Kwanza,” anaeleza.
Aidha, tangazo la Ford Kenya kwamba kitadhamini wagombeaji katika chaguzi ndogo za Malava, Banissa na Ugunja imesawiriwa kama sio tu hujuma kwa UDA bali ushirikiano wake na chama cha Orange Democratic Movement (ODM), chake Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.