Jamvi La Siasa

Uhasama watokota Nyanza Wanga, Omollo, Wandayi, Mbadi na Babu wakipigania viatu vya Raila

December 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

UHASAMA mkali unaendelea kushuhudiwa katika eneo la Luo Nyanza huku wanasiasa wakuu wakipigania kumrithi Raila Odinga ambaye alikuwa kigogo wa siasa za eneo hilo kabla ya mauti yake Oktoba 15.

Gavana wa Homa Bay, Gladys Wanga, Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi, Waziri wa Fedha John Mbadi, Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Raymond Omollo na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino wote wanaonekana kupambana kuvalia viatu vya Bw Raila.

Baada ya kifo cha baba yake Jaramogi Oginga Odinga mnamo 1994, Raila alikuwa kigogo wa siasa za eneo hilo huku matamshi yake yakitoa mwelekeo wa kisiasa kwa eneo hilo kila mara.

Kwa sasa kuna uhasama kati ya Bi Wanga na Bw Omollo kutokana na uchaguzi mdogo wa Kasipul ambapo Boyd Were wa ODM aliibuka mshindi.

Ingawa wanasiasa hao wawili hawajajibizana hadharani, wandani wa Gavana Wanga wanadai kuwa Bw Omollo na baadhi ya viongozi wa UDA walimuunga mkono mgombeaji huru Philip Aroko katika uchaguzi huo mdogo.

Mbunge wa Homa Bay Mjini, Bw Peter Kaluma wakati wa kampeni za uchaguzi huo mdogo alichemka na kuwalenga aliyekuwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero (Nairobi) na Okoth Obado (Migori) kwa kumfanyia Bw Aroko kampeni.

Pia aliashiria kuwa kulikuwa na baadhi ya viongozi serikalini ambao walikuwa wakimuunga mkono Bw Aroko.

“Hatuwezi kuwa ndani ya serikali ilhali viongozi wa UDA wanafanyia kazi wapinzani wetu. Wanawachanganya watu wetu na namwomba Rais William Ruto aingilie kati,” akasema Bw Kaluma.

Baada ya uchaguzi huo, kulikuwa na maandamano ya makundi ya wanawake ambayo yalimtaka Bi Wanga aachane na Bw Omollo.

Makundi hayo yalidai gavana huyo alikuwa akimshinikiza Rais Ruto amtimue katibu huyo au ambadilishe aingie wizara nyingine.

Bw Mbadi na Wandayi nao pia wamekuwa wakizunguka eneo hilo wakisaka uungwaji mkono wakitaka hadhi ya msemaji wa jamii.

Mnamo Alhamisi wiki jana, Bw Wandayi alikuwa mwenyeji wa Mwenyekiti wa Baraza la Jamii ya Waluo, Ker Odungi Randa pamoja na wanasiasa wa ODM akiwemo kiongozi wa chama hicho Dkt Oburu Oginga.

Kabla ya kuwa mwenyeji wa Dkt Oginga na baadhi ya wabunge wa eneo hilo, Bw Wandayi alikuwa amezunguka na kuandaa mikutano Kisumu, Siaya, Nairobi.

Mnamo Ijumaa wiki jana aliandaa mkutano na wasomi kutoka Siaya huku akiendelea kuwashawishi wamuunge mkono kuwa kigogo wa Luo Nyanza.

Katika mkutano huo duru zinaarifu kuwa aliidhinishwa kama msemaji wa jamii ya Waluo na wasomi hao.

“Hatuna njia nyingine ila kusalia tumeungana na tuunde serikali. Lazima tuweke mikakati ya kuridhisha kwa sababu kuwa upinzani ni kazi ngumu,” akasema Bw Wandayi.

“Tukomeshe ubinafsi na tuangalie mbele. Naapa kuwa kama hauko kwenye meza ambapo keki ya taifa inagawanywa basi hapo hujafanya chochote,” akasema Bw Wandayi.

Wabunge Gideon Ochanda (Bondo), Elisha Odhiambo (Gem), Aduma Owuor (Nyakach), Caroli Omondi (Suba South) na Moses Omondi (Ugunja) walihudhuria mkutano ulioandaliwa nyumbani kwa Bw Wandayi eneobunge la Ugunja.

Kwa upande mwingine, wasomi waliokongamana Hoteli ya Acacia, Kisumu na kutangaza wanamuunga mkono Bw Wandayi ni mbunge wa zamani wa Rarieda ambaye pia Mwenyekiti wa Bodi ya Sukari nchini Nicholas Gumbo, Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor, msemaji wa zamani wa Polisi Charles Owino na Dkt Jalang’o Midiwo ambaye ni Kamishna wa Tume ya Ugavi wa Mapato.

“Kwetu mwanasiasa ambaye anashikilia cheo cha juu zaidi ni Wandayi. Kama watu wa Siaya tunaamini kigogo wa siasa za Nyanza atatoka hapa Siaya,” akasema Bw Odhiambo.

“Opiyo Wandayi ni mwanafunzi wa Raila na ukitaka kujua mwelekeo wa kisiasa basi mtafute Wandayi,” akasema Mbunge wa Mathare, Anthony Oluoch.

Bw Mbadi naye amekuwa akizunguka akitumia matamshi ya Mama Ida Odinga kuwa yeye ndiye alikuwa akiandaliwa kumrithi Raila.

Mama Ida aliyatoa matamshi hayo pale Bw Odinga alipokuwa akijiandaa kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Naye Bw Owino mnamo wikendi aliandaa mikutano mikubwa eneobunge la Gem baada ya mazishi ya Beryl Odinga, dada yake Raila, ambapo alionekana kuchangamkiwa hasa na vijana kama kiongozi atakayetoa mwelekeo mpya wa siasa za Luo Nyanza.