Uhuru alipodokeza alikataa kumeza chambo
RAIS mstaafu Uhuru Kenyatta wiki hii alitoa kauli iliyoashiria kwamba alikataa mapendekezo ya baadhi ya viongozi waliotaka aungane nao kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Katika kauli kali isiyo ya kawaida, aliwataka waache kutafuta visingizio vya kushindwa kwao na badala yake wakabiliane na wapigakura kwa sera na uongozi thabiti.
Akizungumza Jumanne, Desemba 30, 2025, wakati wa mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Lugari, marehemu Cyrus Jirongo, huko Lumakanda, Kaunti ya Kakamega, Uhuru alikana vikali madai kuwa anaingilia siasa za ODM.
Alisema lawama hizo mara nyingi hutumiwa na wanasiasa ambao mipango yao kushawishi wengine inakosa kufaulu.
“Mtu akishindwa njia ya kujipendekeza kule anataka kujipendekeza, lazima atafute mtu wa kumlaumu na aseme watu wanamkataa kwa sababu ya fulani na fulani,” alisema Uhuru.Kauli yake ilijiri baada ya kauli za baadhi ya vigogo wa Serikali Jumuishi kudai alikuwa akichochea mipasuko katika chama cha ODM.
Rais huyo wa nne aliwahimiza viongozi waache “fikira mbovu”, na badala yake waende mashinani wazungumze na wananchi, wajenge vyama vyao, waeleze sera zao waziwazi na wazitetee kwa ujasiri.
“Vua hizo fikira mbovu, enda zungumza na wananchi. Unda na usimamishe chama chako. Kuwa na sera zako kama mwanamume,” alisema.Uhuru pia alikemea wanasiasa wanaozunguka nchi nzima wakitoa matamshi ya uchochezi yasiyo na mchango wowote kwa umoja wa taifa au ukuaji wa demokrasia. “Si kuzunguka huku na kule ukitoa mambo ya upuzi ambayo hayapeleki nchi mbali,” aliongeza.
Akisisitiza maono yake kwa Kenya hata baada ya kustaafu, Uhuru alisema taifa hili linahitaji umoja, demokrasia imara na kuheshimu uamuzi wa wananchi. Hata hivyo, alionya kuwa kustaafu hakumaanishi kukubali kudharauliwa.
“Mimi ni mstaafu, lakini hiyo haimaanishi uniingize kidole kwenye macho. Tuheshimiane,” alisema kwa ukali.Kauli zake zilijiri mvutano ukiendelea ndani ya ODM, ambapo baadhi ya vigogo wa chama hicho, wakiongozwa na mwenyekiti wake Gavana Gladys Wanga na Kiongozi wa Wachache Bungeni Junet Mohamed, wamemlaumu Uhuru kwa madai ya kutumia watu wa ndani kusababisha migawanyiko.
Akizungumza Homa Bay Jumapili, Desemba 28, 2025, mbele ya Rais William Ruto, Gavana Wanga alidai kwamba Uhuru anafadhili “mabroka wa kisiasa” ili kuvuruga ODM, chama ambacho kwa sasa kina ushirikiano wa karibu na UDA katika Serikali Jumuishi.“Tunaheshimu Rais Uhuru Kenyatta, lakini hatutakubali juhudi zozote za kukivuruga chama chetu,” alisema Wanga.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna aliomba msamaha Uhuru kwa niaba ya chama, akisema baadhi ya viongozi hawashukuru kwa jukumu alilotekeleza mwaka wa 2022 alipomuunga mkono marehemu Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais.“Nikiwa bado Katibu Mkuu wa ODM, naomba msamaha kwa matusi yanayoelekezwa kwako,” alisema Sifuna.
Wachanganuzi wa siasa wanasema msimamo mkali wa Uhuru unaashiria kuwa hayuko tayari “kumeza chambo” wala kubaki kimya anapolaumiwa. Mchambuzi wa siasa Dkt Peter Macharia asema Uhuru anajaribu kulinda urithi wake wa kisiasa na hadhi yake kama kiongozi mstaafu.
“Uhuru anajua bado ana ushawishi mkubwa kisiasa. Kauli yake ni onyo kwa wanaotaka kumtumia kama kisingizio cha migogoro yao,” anasema.Anasema kauli hiyo inaashiria pia kuwa Uhuru ana shaka kushirikiana na Rais William Ruto katika Serikali Jumuishi.Rais William Ruto amekuwa akisema mara kwa mara kuwa anashauriana na Uhuru kuunganisha Kenya, jambo linaloweza kuwa na athari kuelekea uchaguzi wa 2027.
“Ruto amekuwa akiashiria kwamba amekuwa akirushia Uhuru chambo. Kwa hivyo, katika muktadha huo, kiongozi huyo wa Jubilee anaashiria kuwa amekataa kukimeza,” anaeleza.Kwa mujibu wa wachanganuzi, inawezekana shutuma dhidi ya Uhuru kutoka kwa ODM zinatoka kwingine.
“Kuna uwezekano kwamba hizi si shutuma za ODM pekee ikizingatiwa baadhi ya viongozi wa UDA walimkashifu pia,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.Huku 2027 ikizidi kukaribia, kauli ya Uhuru inaweka wazi kuwa yeye bado ni mhusika muhimu katika siasa za Kenya na licha ya kustaafu atatekeleza jukumu muhimu kuamua mustakabali wa taifa 2027.
“Kumbuka chama chake kina mgombea urais ambaye ni Dkt Fred Matiang’i ambaye amekuwa akishirikiana na upinzani huku baadhi ya minong’ono ikishuku kwamba yeye ni mradi wa UDA. Kauli ya Uhuru inaweza kuashiria kwamba chama chake kimekataa ushirikiano wowote na utawala wa sasa,” akasema Dkt Gichuki.