Jamvi La Siasa

Umaarufu wa Rigathi tishio kwa Raila,Ruto na Uhuru

Na JUSTUS OCHIENG October 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Huku siasa za Kenya zikipamba moto kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, ukuruba ambao haukutarajiwa umeanza kujitokeza kati ya wapinzani wakuu wa kisiasa nchini Rais William Ruto, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Ingawa mitazamo yao ya kisiasa na uhusiano wa vyama yao umekuwa tofauti kwa miaka mingi, sasa wanaonekana kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu mtu mmoja, aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua.

Gachagua ameibuka kuwa kitovu cha nguvu ya kisiasa, akitumia kufukuzwa kwake madarakani na kauli za kuvutia wananchi kuimarisha ushawishi wake, hasa katika eneo lake la Mlima Kenya.

Ingawa hapo mwanzo alionekana kama mwanasiasa asiye na ushawishi, ari yake ya kisiasa na mtazamo wake thabiti baada ya kufukuzwa madarakani Oktoba mwaka jana, imezua hofu kwa wanasiasa wenye uzoefu nchini.Kuibuka kwa Gachagua kunatokana na juhudi zake zisizo za kawaida za kujijenga kama kiongozi wa kisiasa wa eneo lenye kura nyingi la Mlima Kenya.

Rais Ruto kwa kushirikiana na Naibu wake Profesa Kithure Kindiki wanajitahidi kudumisha ushawishi wa eneo hilo, lakini Gachagua, ambaye sasa ni kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizen’s Party (DCP), ameweza kupata sehemu kubwa ya wapiga kura wa eneo hilo.Wataalamu wa siasa wanasema ujumbe wake — mara nyingi mkali, umevutia wengi vijijini.

Kwa Rais Ruto, hili ni changamoto ngumu la kukabili. Alipata ushindi 2022 kwa msaada wa Mlima Kenya kupitia Gachagua, lakini kauli za kisiasa za Gachagua katika kanda hiyo zimeibua wasiwasi katika kambi ya Kenya Kwanza.

Mikakati ya Gachagua, kama vile kuzungumzia umma kuhusu ukosefu wa maendeleo katika eneo la kati mwa Kenya, imetatiza Ikulu.Rais Ruto amezindua mipango mikubwa ya kuwainua kiuchumi watu wa Mlima Kenya na sehemu nyingine za nchi, huku Naibu wake Profesa Kindiki akiongoza juhudi hizo kwa lengo la kuimarisha msaada.

Kwa upande wa upinzani, kambi ya Odinga ina wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa ushawishi wa Gachagua anayeshirikiana na viongozi wa vyama kama Kalonzo Musyoka wa Wiper, Martha Karua wa People’s Liberation Party (PLP) na Eugene Wamalwa wa DAP-K, wote waliomsaidia Odinga katika uchaguzi wa 2022.

Washirika wa Odinga wanaona Gachagua kama mpinzani hatari zaidi kuliko walivyowahi kufikiria: mtu asiyetabirika lakini anayezidi kupendwa katika maeneo muhimu.Gachagua, hata kama ataamua matokeo bila kuchaguliwa, anaweza kubadilisha hali ya siasa hasa iwapo Mlima Kenya utaungana nyuma yake.

Hivyo basi, si ajabu kuwa washirika wa Odinga pamoja na Rais Ruto wamemkosoa Gachagua, wakimtuhumu kuwa “mchochezi wa chuki za kikabila.”

Kaka ya Odinga, Seneta wa Siaya, Dkt Oburu Oginga, aliongoza mashambulizi dhidi ya Gachagua wakati wa mazishi ya Waziri wa zamani Dalmas Otieno huko Rongo, Migori, akimtahadharisha kuhusu mapambano makali ya kisiasa mwaka 2027.

“Gachagua, tafadhali, achana na sisi. Sajili watu wako, sisi pia tunasajili wetu, na tusubiri 2027 tuone matokeo,” alisema Dkt Oginga.Dkt Oginga alionyesha kuwa mapambano ya 2027 yatakuwa kati ya Rais Ruto na Odinga upande mmoja dhidi ya kambi ya Gachagua.

“Watu wetu wanapaswa kujua kuwa serikali hii jumuishi ni mpangilio bora zaidi kwetu. Nimekuwa katika muungano na Moi, na Kibaki, na Uhuru, na nawaambia huu ni mpangilio bora zaidi tulio nao,” alisema Seneta huyo wa Siaya.

Ushawishi wa Gachagua katika Mlima Kenya ni tishio kubwa Kenyatta.Mbunge wa Githunguri, Gathoni Wamuchomba, mwanachama wa muungano wa Kenya Moja, alisisitiza kuwa Kenyatta bado ni “mfalme asiye pingwa wa Mlima Kenya.”