Upinzani unavyoua azimio la ‘Wantam’
MIVUTANO kati ya viongozi wakuu wa upinzani inaendelea kuibua maswali kuhusu hatima ya muungano wa kisiasa wanaosuka na ndoto yao ya kumfanya Rais Ruto kuhudumu kwa muhula mmoja pekee.
Wachanganuzi wanasema kutoaminiana kwa vinara wa vyama vya upinzani kunaua ndoto ya ‘wantam’.Hali ya kutoaminiana kati ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na aliyekuwa Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i, inaendelea kuibua hisia kali miongoni mwa wafuasi wa upinzani.
Wachanganuzi wa siasa wanasema hatua ya wafuasi wao kurushiana lawama kunaweza kuchochea mgawanyiko mkubwa, kiasi cha kufifisha matumaini ya muungano wa upinzani.
Tofauti zao zinatokana na hatua ya Bw Matiang’i kukumbatia chama cha Jubilee chini ya mwavuli wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ambaye uhusiano wake na Gachagua umedorora tangu uchaguzi mkuu uliopita.
“Wakiendelea hivi, hawatawahi kuzungumza kwa sauti moja,” asema mchambuzi wa siasa, Dkt Isaac Gichuki.Anasema tofauti za wazi kati ya Kenyatta na Gachagua wote wanaotoka Mlima Kenya zinaweza kuvuruga mpango wa upinzani ikizingatiwa kuwa ngome yao ina wapiga kura wengi.
Huku Gachagua akizidi kujenga jina lake kama msemaji wa eneo hilo, wandani wa Kenyatta, wakiongozwa na katibu mkuu wa Jubilee – Jeremiah Kioni, wanadai ni kibaraka wa serikali katika upinzani.
“Hakuna njia ya kuunganisha Mlima Kenya iwapo Gachagua na Uhuru hawataonana uso kwa uso,” asema Grace Wanjiku, mchambuzi wa siasa kutoka Nyeri. Anasema hii inafumua hatua ambazo upinzani ulikuwa umepiga za kuungana.Tiketi ya Kalonzo Musyoka na Matiang’i imekuwa ikizungumziwa kwa muda kama inayofaa kumshinda Rais Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.
Hata hivyo, mdokezi kutoka Wiper asema kuwa Kenyatta anataka Matiang’i apeperushi bendera na kuteua mgombea mwenza kutoka Mlima Kenya akichukizwa na hatua ya makamu rais huyo wa zamani kushirikiana na Gachagua.
Gachagua naye anasemekana kumpendelea Musyoka kupeperusha bendera ya upinzani.Kalonzo naye amenukuliwa akipuuza pendekezo la Matiang’i kuwa mgombea urais wa muungano wa upinzani.
“Tayari Kalonzo amewahi kusema wazi kwamba hafahamu mengi kuhusu Matiang’i kama mwanasiasa isipokuwa kuhudumu kama waziri. Kauli hii inaonyesha wazi kuwa kuna ukosefu wa uaminifu baina yao,” asema Peter Makau, mchanganuzi wa siasa kutoka Machakos.
Vinara wa upinzani Gachagua, Kalonzo, Justin Muturi Martha Karua na Eugene Wamalwa wamepanga mikutano na hafla za kisiasa bila kuhusisha Matiang’i. Mnamo Ijumaa walikuwa katika kaunti ya Kajiado walikoandaa mikutano ya hadhara na kusisitiza umoja wao.
Katibu Mkuu wa UDA, Cleophas Malala na Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, wamekuwa wakirushiana maneno mara kwa mara kuhusu mwelekeo wa siasa za upinzani.
Kila mmoja anaonekana kuwa na ajenda tofauti ya mustakabali wa muungano wa vyama vya upinzani. Kila mmoja anadai mwingine ni ‘fuko’ wa serikali katika upinzani.Kioni pia amekuwa akimlaumu Gachagua kwa kutaka kulazimisha wakazi wa Mlima Kenya kukumbatia chama chake cha DCP na kutema vyama vingine vya kisiasa.
Dkt Gichuki anasema Kioni anaendeleza uhasama wa kisiasa wa kiongozi wa chama chake cha Jubilee na Gachagua.Katika eneo la Magharibi, tofauti kati ya aliyekuwa Waziri Eugene Wamalwa na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya ni mfano mwingine wa mvutano unaoweza kuua ndoto ya upinzani kuungana kumenyana na Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Natembeya ambaye amejijengea umaarufu kupitia vuguvugu lake la Tawe ametishia kugura chama cha DAP- Kenya iwapo Bw Wamalwa hatakubali mapendekezo yake ya kupanua chama kujumuisha wakazi wote wa Magharibi.“Hawa wawili wangetulia na kuungana na Malala kuimarisha upinzani eneo la Magharibi,” anasema Sarah Wekesa, mchambuzi wa siasa.
Kwa mujibu wa Dkt Gichuki, iwapo vinara wa vyama vya upinzani hawatazika tofauti zao, ndoto ya ‘wantam’ itakufa kwa sababu ya wanasiasa kutanguliza maslahi yao binafsi badala ya ajenda ya pamoja.
“Wanadai wanalenga kufanya Dkt Ruto kuwa rais wa muhula mmoja lakini kauli na vitendo vyao vinaonyesha mkondo tofauti,” asema Dkt Gichuki.Bi Wekesa naye anasema kusambaratika kwa upinzani kutakuwa baraka kwa Ruto na washirika wake katika utawala wa Kenya Kwanza.
“Ndoto ya ‘wantam’ iliwapa matumaini wafuasi wa upinzani. Ilikuwa nafasi nzuri ya kuunganisha nguvu ya upinzani dhidi ya Rais Ruto ambaye mbali na kuwa na nafasi nzuri kwa kuwa yupo madarakani, ni mweledi wa kupanga siasa,” aeleza Wekesa.
Anasema huku uchaguzi mkuu wa 2027 ukikaribia, ni wazi kuwa ikiwa viongozi hawa hawataweka kando tofauti zao, basi ‘wantam’ haitatimia.