Jamvi La Siasa

Upinzani waingia baridi baada ya Gachagua kuenda ziara Amerika

Na JUSTUS WANGA, CECIL ODONGO August 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TANGU aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua aondoke nchini, Upinzani umeonekana kupoteza dira huku shutuma zilizokuwa zikielekezwa dhidi ya serikali zikipungua na hata mikutano ya hadhara ya mrengo huo kuadimika au kukosa msisimko kama hapo awali.

Bw Gachagua aliondoka nchini Julai 9 kwa ziara ya miezi miwili nchini Amerika ambapo alisema lengo lake ni kukutana na Wakenya wanaoishi huko pamoja na kuwaeleza kuhusu hali halisi nchini katika utawala wa Rais William Ruto.

Kabla ya kuondoka nchini, Bw Gachagua na vinara wengine wa Upinzani walikuwa wakiandaa mikutano ya kila mara ya umma na kuhutubia hadhira au halaiki ya watu katika kaunti mbalimbali wakionekana kuilemea serikali.

Tangu kuondoka kwake vinara wa Upinzani Kalonzo Musyoka (Wiper), Eugene Wamalwa (DAP-Kenya), aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i na Kiongozi wa PLP Martha Karua wameonekana kutokuwa na shughuli nyingi za kisiasa.

Wamegeuka tu watumiaji wa mitandao ya kijamii na vikao vya wanahabari kushutumu serikali.

Bw Musyoka na Wamalwa wamekuwa wakiandaa vikao na wanahabari, kikao cha mwisho kikiwa kile cha kumrai Katibu wa ODM Edwin Sifuna agure chama hicho baada ya tangazo la Kinara wa ODM Raila Odinga kuwa yuko tayari kushirikiana na Rais William Ruto hadi baada ya 2027.

Kikao hicho kiliandaliwa na Bw Musyoka na Wamalwa wikendi iliyopita baada ya kauli hiyo ya Bw Odinga wakati wa mazishi ya Phoebe Asiyo katika Kaunti ya Homa Bay mnamo Ijumaa wiki iliyopita.

Naibu Kiongozi wa DCP Cleophas Malala na Seneta wa Nyandarua John Methu ndio wamekuwa wakichangamkia mikutano ya DCP ila pia hafla hizo haziangaziwi na kuchangamkiwa kutokana na kutokuwepo kwa Bw Gachagua.

Serikali nayo inaonekana kupumua na kutulia kwa sababu makombora ambayo Bw Gachagua alikuwa akiyarusha akiwa nchini na kuchemsha umma sasa anayafanya kutoka ng’ambo wala hayahisiki sana na Wakenya jinsi ilivyokuwa awali.

Akiwa Amerika, kitengo cha mawasiliano cha mbunge huyo wa zamani wa Mathira kimekuwa kikiwajulisha Wakenya kuhusu shughuli na mikutano yake wakati wa ziara hiyo.

Kutokana na hali iliyopo ambako ushawishi wa Bw Gachagua unaonekana kuzidia wenzake hata bila uwepo wake, baadhi ya wachanganuzi sasa wanakisia huenda akataka mamlaka zaidi na nafasi nyingi kwenye mkataba na vinara wenzake katika Upinzani kuelekea 2027.

Mwandani wake mmoja alidokeza kuwa huenda akataka kutengewa angalau asilimia 40 ya nyadhifa serikalini, na kuwaacha vinara wengine watano au zaidi kugawana nafasi zitakazosalia.

Tangu alipozindua chama cha DCP katika mtaa wa Lavington jijini Nairobi, mnamo Mei 15, 2025, Bw Gachagua amefanya ziara katika sehemu kadhaa za nchi akiuza sera za chama hicho.

Baadhi ya kaunti ambazo alizuru ni Murang’a, Kiambu, Kakamega, Makueni, Meru, Tharaka Nithi na kaunti za pwani, akiandamana na Bw Musyoka.

Bw Gachagua ametumia mikutano hiyo kuishambulia serikali kutokana na masuala kama ufisadi, maovu katika uchaguzi na jinsi ilivyopambana na maandamano ya Gen-Z mwaka wa 2024 na mwaka huu.

Aidha, amekuwa akihudhuria mazishi ya waathiriwa wa mauaji ya polisi nyakati za maandamano na michango ya kusaidia shule na makanisa.

Kabla ya hapo, aliongoza mikutano kadhaa nyumbani kwake, kijijini Wamunyoro, kujadili mikakati ya kisiasa jicho likiwa hasa kwa kura za 2027.