Ushirika wa Rigathi na Natembeya, uko njiani unakuja?
USHIRIKIANO wa kisiasa kati ya aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya unanukia baada ya gavana huyo kuashiria kuwa yuko tayari kushirikiana na kiongozi huyo.
Kwenye mahojiano Jumatatu na redio ya Kameme FM inayopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Gikuyu, gavana huyo alisema ataendelea kushirikiana na eneo la Mlima Kenya kisiasa kwani alipandishwa vyeo katika utawala wa mkoa kutokana na ushawishi wa watu wa eneo hilo.
Alieleza kuwa watu kama marais wa zamani Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta, aliyekuwa mkuu wa Utumishi wa Umma Francis Kimemia na mshauri wa rais kuhusu masuala ya usalama Monica Juma, walimsaidia kupanda ngazi kutoka afisa wa cheo cha chini hadi akawa Kamishna wa Ukanda wa Bonde wa Ufa 2022.
“Ikiwa mtu anaamini kuwa ninafaa kuwa adui wa mtu kutoka Mlima Kenya kwa sababu ya tofauti zake na mtu huyo, ajue anaota mchana,” Bw Natembeya akasema.
Gavana huyo alisema wakereketwa wa serikali wanampiga vita kisiasa, kiasi cha kupanga hoja ya kumtimua afisini, kutokana na uhusiano wake na Bw Gachagua na uamuzi wake kuendelea kukosoa utawala huu wa Rais William Ruto.
“Wanataka kunitimua kutokana na msimamo wangu kisiasa. Waendelee na mipango hiyo kwani itanipa nafasi nzuri ya kwenda mashinani kutetea maslahi ya umma, nikishirikiana wa Gachagua na wazalendo wengine,” akasema.
Gavana Natembeya alidai Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah ni miongoni mwa wadhamini wakuu wa mikutano ya kumwondoa afisini.
Hata hivyo, alimpuuzilia mbali Mbunge huyo wa Kikuyu kama “mtu anayepayuka tu ilhali hana hekima yoyote”.
Mnamo Januari 3, Bw Ichung’wah alimshambulia hadharani Bw Natembeya wakati wa mazishi ya mamake Spika wa Bunge Moses Wetang’ula katika Kaunti ya Bungoma kwa kuihusisha serikali na visa vya utekaji nyara wa Wakenya.
“Wewe Gavana Natembeya haufai kulalamikia utekaji nyara ilhali rafiki yako Rigathi Gachagua ndiye anaendeleza utekaji huo ili ailaumu serikali. Ulihudumu kama Kamishna wa Ukanda katika utawala uliopita wakati mamia ya watu walitekwa na kuuawa katika Bonde la Kerio kisha miili yao ikatupwa katika Mto Yala. Je, ulithamini maisha ya raia wakati huo?” Ichung’wah akauliza kwa hasira mbele ya Bw Natembeya aliyehudhuria hafla hiyo.
Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na Rais William Ruto.
Siku moja baada ya kushambuliwa kwa Gavana Natembeya, Bw Gachagua alimpa moyo huku akimtaka kutokubali kuyumbishwa na vitisho kama hivyo.
“Ndugu yangu Gavana Natembeya. Tafadhali usikubali watetezi hao wa udhalimu na wenye matusi wakuzuie kuwahudumia watu wa kaunti ya Trans nzoia. Watu hawa wamekodiwa kukushambulia ili kumfurahisha mkubwa wao,” Bw Gachagua akamwambia.
Naibu huyo wa rais wa zamani alimshauri Natembeya asiogope kuongea ukweli, akiongeza kuwa anashambuliwa na wandani wa Rais Ruto kwa sababu analeta mabadiliko katika jamii.
“Na usiogope kupaza sauti yako ukitetea raia wa Kenya kwa sababu huo ndio wajibu wako kama kiongozi,” Bw Gachagua akaongeza.
Gavana Natembeya, aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K), amekuwa akihimiza umoja wa jamii ya ‘Mulembe’ huku akiwakosoa viongozi wakuu eneo hilo, Bw Wetang’ula na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi kwa kutosaidia kukuza eneo hilo kimaendeleo.
Kando na kumtetea Bw Natembeya, Bw Gachagua na wandani wake, wamemwalika gavana huyo katika mikutano kadhaa maeneo ya Mlima Kenya, hali ambayo imeibua tetesi kuhusu uhusiano wake na mbunge huyo wa zamani wa Mathira.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati anasema bado ni mapema kubashiri iwapo ushirikiano wa kisiasa kati ya Gavana Natembeya na Bw Gachagua utayumbisha siasa nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
“Bw Natembaye ambaye ameanzisha vuguvugu la Tawe, angali mchanga katika siasa. Isitoshe, ameonyesha wazi kwamba bado anapania kutetea kiti chake cha ugavana 2027. Kwa hivyo, huenda akajishughulisha zaidi na juhudi za kutetea kiti hicho badala ya kumsaidia Gachagua katika ajenda yake ya kuangusha Rais Ruto 2027,” anaeleza.