Usipotimiza maelewano yetu hautatupata 2027, Oburu aonya Ruto
SENETA wa Siaya, Dkt Oburu Oginga amemwambia Rais William Ruto kuwa asitarajie kuungwa mkono kwa urahisi na chama cha ODM katika uchaguzi wa 2027, akisema hilo litategemea iwapo atakuwa amechapa kazi na kutimiza ahadi zake za maendeleo kwa Wakenya au la.
Dkt Oginga, ambaye ni nduguye kinara wa upinzani Raila Odinga, alisema rekodi ya maendeleo ya Rais Ruto ndiyo itakayoamua kama ODM itamuunga mkono katika kinyang’anyiro cha 2027 au la.
“Makubaliano kati yetu na serikali kupitia muafaka tuliotia saini mnamo Machi yamejikita kwenye masuala 10 ambayo tuliyaorodhesha yatmimizwe,” akasema.
“Tutafanya kazi nao (Kenya Kwanza) hadi 2027 na iwapo watakuwa wamefanya kazi vizuri, tutakubaliana. Iwapo hawatafanya kazi vizuri, tutatengana nao,” akasema Dkt Oginga.
Kauli hii ya kaka yake Bw Raila ni kinaya kwani siku za hivi majuzi, Dkt Oginga amekuwa akisema ODM iko tayari kulipa deni la Rais Ruto aliyemuunga mkono Bw Raila kwenye uchaguzi mkuu wa 2007.
Dkt Oginga anasema watamuunga Rais iwapo yote yaliyomo kwenye mkataba walioingia mapema mwaka huu yatatimizwa.
Kati ya maelewano hayo ni kutekelezwa kwa Ripoti ya Kamati ya Maridhiano (NADCO), usawa katika mgao wa bajeti pamoja na uteuzi katika nyadhifa za umma, kuimarishwa kwa ugatuzi, uwekezaji wa kiuchumi kwa vijana, uwazi na kuzimwa kwa ubadhirifu kwenye matumizi ya pesa za umma.
Mengine ni haki ya kukusanyika kwa wanaopigania haki, fidia kwa waliojeruhiwa na kuuawa wakati wa maandamano, kutathminiwa kwa deni la taifa, kukomeshwa kwa utekaji nyara, kuheshimiwa kwa katiba na uhuru wa wanahabari miongoni mwa mengine.
Seneta huyo alisema sasa ni wajibu wa Rais kutimiza matakwa hayo yote iwapo analenga kupata uungwaji wa ODM 2027.
Mbunge huyo wa zamani wa Bondo, ndugu na mwandani wa Raila alimkumbusha Rais kuwa kuingia kwao serikalini ndiko kulisababisha iwe thabiti wakati wa maandamano ya Gen-Z mwaka jana.
“Tulikubaliana kuunga serikali baada ya mashauriano ya kina na wafuasi wetu ili isianguke. Kwa hivyo, hata wanapotapatapa, waendelee kufanya hivyo hadi uchaguzi mkuu ufike.”
“Tunataka demokrasia ifuatwe kwa sababu ni kupitia uchaguzi mkuu ndipo rais mpya huchaguliwa na sisi kama ODM hatutaki serikali isambaratike kwa sasa. Kuharibu nyumba ni rahisi lakini kuijenga si kazi rahisi ndiyo maana hatutakubali wito wa ‘Ruto Must Go’ yaani Sharti Ruto Aondoke, uvuruge nchi,” akaongeza.
Maandamano ya Gen Z mwaka jana yalitishia kusambaratisha udhabiti wa serikali hasa baada ya vijana kuvamia bunge na mauaji kutokea.
“Rais huongoza kwa muda mfupi ambao ni miaka mitano kisha Wakenya wanaelekea kwenye uchaguzi. Kwa hivyo, lazima tungehakikisha serikali hii inasalia kwa amani na umoja.
“Kama Ruto atatimiza ahadi ambazo alitoa kwa watu Wakenya hasa za maendeleo na umoja, basi tutathmini kumuunga mkono. Utendakazi wake ndio muhimu hapa,” akasema Dkt Oginga.
Kauli ya Dkt Oginga inaonyesha wazi kuwa ODM bado haijafanya uamuzi wa kuunga Rais Ruto mnamo 2027 hasa wakati huu ambapo viongozi wengine wa upinzani wameungana na wameahidi kuwavutia wanasiasa wengine kwenye kambi yao.
Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa PLP Martha Karua, kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i, wameapa kuunda muungano mkubwa ambao utampelekea Rais nyumbani 2027.
Japo Dkt Oginga hakutaja kambi ambayo Bw Odinga atajiunga nayo iwapo atamtelekeza Rais Ruto 2027, alitambua kuwa bado ni mapema kujua muungano ambao utaenda uchaguzi.
Aliitaka kambi ya Bw Gachagua iendelee na shughuli zake za kujiandaa kwa 2027 lakini akasema kuwa muungano wa mwisho utakuwa tofauti na kile ambacho kinaonekana sasa.
“Muungano wao si hoja, wajaribu tu ila hatutakubali mgawanyiko na kuharibiwa kwa nchi. Hatutakubali chochote ambacho kinaathiri au kuvuruga Wakenya,” akasema.
Kiongozi huyo alisema ukosefu wa udhabiti unaweza kusababisha Kenya ielekee mkondo wa mataifa yanayoongozwa kijeshi kama Somalia, Sudan Kusini na Sudan.