Uwanja wafurika watu 15 wakiwania kung’oa Ruto 2027
UCHAGUZI wa urais Kenya mwaka 2027 tayari umevutia wagombeaji wengi zaidi, miaka miwili kabla ya kufanyika. Orodha ya wagombea inazidi kuwa ndefu kutoka wakongwe wa siasa hadi sauti mpya na baadhi ya wachambuzi wanasema hii inaweza kumfaidi Rais William Ruto.
Baadhi ya wadadisi wa siasa wanaamini idadi kubwa ya wagombeaji hunufaisha walio madarakani; wengine wakisema kuwa wagombeaji wengi wanaweza kusababisha duru ya pili ya uchaguzi, na kuunga mgombea ambaye ataibuka wa kwanza au wa pili.
Huku baadhi ya wagombeaji wakiapa kuungana kumuondoa Rais Ruto madarakani katika uchaguzi huo, wengine wameahidi kukabiliana naye moja kwa moja, wakimlaumu kwa kuendesha nchi vibaya.Mnamo Alhamisi, Jaji Mkuu mstaafu David Maraga alitangaza rasmi nia yake ya kugombea urais na kufichua kwamba atatumia chama cha chama United Green Movement (UGM).
Tangazo hilo lilifuata la mfanyabiashara na mwanasiasa, Jimi Wanjigi. Bw Wanjigi alichukua rasmi uongozi wa Chama cha Safina kutoka kwa Wakili Paul Muite, akiahidi kukipa nguvu mpya akijiandaa kukabili Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027.
Akiwa na Wakili Willis Otieno kama naibu kiongozi wa chama, Wanjigi alitangaza kuwa Safina italeta enzi mpya ya uhuru wa kiuchumi na uwajibikaji wa kisiasa katika nchi aliyosema imekolea madeni na ufisadi.
Ingawa Maraga na Wanjigi wamepata baraka za vyama rasmi, watakabiliwa na kikosi kikubwa cha “upinzani ulioungana” chini ya aliyekuwa naibu rais, Rigathi Gachagua ambaye ametangaza azma yake kupitia chama cha DCP.
Gachagua ana viongozi kama Kalonzo Musyoka (Wiper), Martha Karua (PLP), Eugene Wamalwa (DAP-K) na Justin Muturi (DP). Ingawa Fred Matiang’i, ambaye ana uhusiano na chama cha Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta, pia amekuwa akijiunga na kikosi hicho, ameonyesha dalili za kujitenga na muungano huo wa upinzani.
Mnamo Ijumaa, aliepuka ziara ya vinara hao wa upinzani Kajiado siku ambayo Gachagua alimshambulia vikali kwa kutokuwa na chama asili kutoka ngome yake.Dkt Matiang’i alikuwaNakuru alikokutana na vijana.
“Nimeanza kuzungumza na wanachama wa Jubilee kutoka mashinani. Hii ni mojawapo ya mikutano 47 nitakayofanya nchini. Nitawatembelea wanachama katika kila kaunti, hata kijijini, na kuwashauri wajisajili kama wapigakura,” alisema Dkt Matiang’i na kueleza matumaini ya kupata tiketi ya kupeperusha bendera ya upinzani.
Katika ODM, utata kuhusu mipango ya Raila Odinga 2027 unaongeza mchanganyiko zaidi, hasa kutokana na ushirikiano wake na Dkt Ruto.Profesa Macharia Munene wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amerika (USIU) anaamini kwamba ushawishi wa wagombea wengi unaweza kumfaidi Dkt Ruto dhidi ya upinzani.
“Hii inafanya uwezekano wa raundi ya pili kuwa kubwa,” anasema Prof Munene.Profesa Gitile Naituli wa Multi Media University pia anakubali kwamba kufurika kwa wagombeaji urais kunaweza kumfaidi Dkt Ruto, lakini anaonya kwamba si jambo la moja kwa moja. akisema yote yanategemea jinsi upinzani utakavyojipanga.
“Katika historia ya siasa ya Kenya, walio madarakani hunufaika na upinzani ukigawanyika,” alisema.Katika chaguzi za 1992 na 1997, aliyekuwa Rais Daniel arap Moi aliendelea kushikilia madaraka kwa kiasi kikubwa kutokana na upinzani kuwa na migawanyiko mingi.
Wachambuzi wa kisiasa sasa wanaonya kuwa hali hiyo inaweza kujirudia mwaka 2027, na kumfaidi Rais William Ruto ikiwa wapinzani wake hawataungana.Profesa Gitile Naituli anasema kuwa hata kama Wakenya wengi wangetaka mabadiliko ya uongozi, ukosefu wa umoja miongoni mwa wapinzani unaweza kuwanyima fursa hiyo.
“Iwapo wapinzani wataendelea kugawanyika, basi Ruto atafaidika. Lakini kama wataungana nyuma ya mgombea mmoja aliye na ushawishi au wajenge muungano wa nidhamu, basi huo msongamano wa wagombea unaweza kuleta ushindani mzuri,” alisema.
Anasisitiza kuwa hoja si idadi ya watu wanaotangaza nia ya kugombea, bali kama wagombea hao wataungana baadaye kuunda muungano wa pamoja. “Wasipoungana, mgawanyiko utampa Ruto faida. Lakini wakishirikiana, ushindani huu unaweza kuleta mabadiliko,” asema.
Mchambuzi wa kisiasa Dismas Mokua anaongeza kuwa: “Ingawa zaidi ya Wakenya 15 tayari wametangaza nia ya kugombea urais, kwa uhalisia, asilimia 80 yao wanaota tu, hawana uwezo wa kuendesha kampeni zinazoweza kuleta mafanikio.”
Aidha, Mokua anatahadharisha kuwa Rais Ruto anaweza kufadhili wagombea wa urais kutoka maeneo ambako hahitaji ushindani mkali kama mbinu ya kupunguza nguvu ya upinzani na kudumisha madaraka.
Wengine waliotangaza nia ya kuwania urais ni Seneta wa Busia Okiyah Omtatah, mwanaharakati wa haki za binadamu Boniface Mwangi, Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya, pamoja na wagombea wa 2022 Profesa George Wajackoyah (Roots Party) na David Waihiga (Agano Party).Kwa mujibu wa Wakili Chris Omore, mgawanyiko huu unaweza kumpa Rais Ruto nafasi nzuri zaidi.
“Rais Ruto ameendelea kuimarisha nguvu serikalini tangu ushindi wake 2022, na anaendelea kufaulu katika mazingira ambapo wapinzani wake hawajaungana,” anasema Omore.