Uwezekano wa handisheki ya Ruto na Raila kuhusu AU bado wazua wasiwasi Mlimani
Na MWANGI MUIRURI
LICHA ya eneo la Mlima Kenya kung’ang’ania kwamba Rais William Ruto asiwahi kuthubutu kujiingiza katika handisheki na Bw Raila Odinga, ishara ni kwamba ilifanyika au itafanyika.
Kwa msingi kwamba eneo hilo lilimpa Bw Ruto asilimia 87 ya kura zao katika uchaguzi mkuu wa 2022 hivyo basi kumpa asilimia 47 ya mamlaka yake Ikulu, Naibu wa Rais Rigathi Gachagua amekuwa akipinga uwezekano wowote wa handisheki kati ya hao wawili.
Bw Gachagua amekuwa akitangaza kwamba “mimi sitakuwa mahali ambapo Bw Odinga anasalimiana na Rais huyu wetu kwa kuwa kufanya hivyo ni kutukoroga akili tuchanganyikiwe na tuishie kupoteza ufahamu wetu kisiasa”.
Hata hivyo, sasa inaonekana ni kama Rais Ruto aliridhiana na Bw Odinga kitambo na handisheki ikafanyika kimyakimya ikizingatiwa kwamba Bw Odinga katika siku za hivi karibuni hajakuwa na presha zile zake za kawaida dhidi ya utawala wa Ruto.
Hatua ya Rais Ruto kumuunga mkono Bw Odinga kuwania wadhifa wa mwenyekiti wa Muungano wa nchi za Afrika (AU) ndio sasa umewafanya wengi katika Mlima Kenya kuhofia kwamba Bw Odinga na Rais ni kitu kimoja.
Gachagua hajamuidhinisha kuhusu AU
Taswira ni kwamba, ikiwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alisalimia Bw Odinga nje ya Ikulu ya Nairobi, huenda sasa handisheki ya Ruto na Odinga ifanyike nje ya makao makuu ya AU mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia.
Katika hali hii, Mlima Kenya umeonekana kujitenga na kuunga mkono Bw Odinga kupata wadhifa huo wa AU huku Bw Gachagua akiwa hajamuidhinisha.
Wengine wote katika mirengo mikuu ndani ya serikali ya Rais Ruto wakiwa tayari wamemchangamkia kinara huyo wa upinzani afaulu, Gachagua anaonekana kukwamilia pingamizi tu.
“Tuliwaambia kwanza tujipange kabla ya kuruka kuahidi mtu kura zetu lakini mkakataa. Sisi tuliokuwa ndani ya Azimio tulikuwa na mkataba wetu wa kutekelezwa iwapo Bw Odinga angenyakua ushindi. Tulikuwa na chama chetu cha Jubilee cha kushirikisha mkataba huo kutekelezwa,” asema mwandani wa Bw Odinga, Bw Zack Kinuthia.
Bw Kinuthia anasema kwamba wale wa Jubilee wakiongozwa na Gachagua “waliingia katika muungano na Ruto wakiwa hawana chama chao, bila mkataba na bila maono yoyote wakitwambia kwamba waliwekeza imani yao kwa uungwana”.
Sasa, Bw Kinuthia anawatahadharisha wenyeji Mlima Kenya kwamba “siasa ni mduara na vile kivumbi kinaambwa, huenda 2027 jamii za Mlima Kenya zijipate katika upweke wa kisiasa wengine wote wakiwa wameungana dhidi ya eneo hili letu”.
Aliyekuwa mbunge wa Ndaragwa Bw Jeremiah Kioni alisema kwamba “sisi ni kama waliorogwa kwa kuwa tulimposa mrembo wetu ukweni pasipo hata kujadiliana kuhusu mahari”.
Alisema kwamba kwa sasa “kile kinatekelezewa Mlima Kenya na utawala wa Rais Ruto ni dharau kwa kuwa mrembo akishafika kwa boma la wakwe na anazidi kutumiwa thamani yake hushuka na wakati ukiwadia wa kulipiwa mahari, utakubali tu kiwango kitakachowekelewa mezani”.
Aliyekuwa Gavana wa Murang’a Bw Mwangi wa Iria aliteta kwamba “kwa sasa mtoto aliyezaliwa ndani ya ndoa hii ya Rais Ruto na Mlima Kenya analia kwa mahangaiko na itabidi tu tutafute mbinu ya kumtuliza”.
Alisema kwamba Bw Gachagua tayari amekiri hadharani kwamba “tuliingia ndani ya United Democratic Alliance (UDA) kupitia ahadi ya mdomo tu na kwa sasa hatuna wa kutetea masilahi yetu”.
Dharura kujumuika pamoja Jubilee
Bw Iria alisema kwamba “kwa sasa ni wakati wa kuunga mkono wote wetu walio mamlakani ili kufufua ndoto ya eneo la Mlima Kenya ya kuafikia malengo ya ufanisi”.
Alisema “ni wakati hata wa kuunga Bw Gachagua mkono ili akimbizane na yale yanayotuhusu nasi tukiwa katika ule mrengo wa upinzani tushirikiane kusaka ufaafu zaidi”.
Mbunge wa bunge la Afrika Mashariki (EALA) Bw Kanini Kega kwa sasa anasema kwamba ni dharura watu wa Mlima Kenya wajumuike pamoja ndani ya chama cha Jubilee kama chama cha nyumbani.
“Kwa sasa hamuwezi mkaelewa umuhimu lakini katika kipindi cha mwaka mmoja au miwili baadaye mtakuja kuelewa maana ya kuwa na chama chetu,” akasema.
Aliongeza kwamba kuna masuala ya kisiasa yanayoendelea kujiangazia na ambayo hayawiani na nia njema kati ya washirika wa sasa wa kisiasa.
Hili ni suala ambalo hivi majuzi Seneta wa Nyeri Bw Wahome Wamatinga akiwa na Gavana wa Nyeri Bw Mutahi Kahiga walilila wakisema kwamba kuna uchochezi fiche wa kutenga Mlima Kenya, wakionya kwamba kuna uwezekano nao wajibu mipigo.
Kujibu mipigo kuliwekwa wazi kama kudai mkataba wa ushirikiano kati ya Mlima Kenya na utawala wa Rais Ruto ujadiliwe upya na wenyeji waweke matakwa mapya katika ushirika huo.
Matamshi hayo ndiyo Bw Gachagua hivi majuzi aliyapuuza akiyataja kuwa “maongezi ya matope” lakini tetesi bado zimezidi kwamba hali si shwari ndani ya ushirika wa Mlima Kenya na utawala wa Rais Ruto.