Jamvi La Siasa

Vigogo wa upinzani mbioni kusuka miungano kuhakikisha ‘Ruto anakuwa wa muhula mmoja’

Na COLLINS OMULO February 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MIPANGO ya kuunda muungano wa upinzani kwa lengo la kumtimua Rais William Ruto baada ya muhula mmoja inazidi kushika kasi huku vigogo wanaoisuka wakisema kuwa wako karibu kutoa tangazo la kutetemesha siasa nchini.

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa walisema nchi inafaa kuwa tayari kwa tangazo kubwa.

Viongozi hao watatu wanasuka kile wanachosema ni muungano mkubwa wa kumkabili Rais Ruto katika azma yake ya kuchaguliwa kuhudumu kwa muhula wa pili.

Ingawa hawakutoa maelezo, viongozi hao watatu walidokeza watatoa tamko kuu wakati wa hafla ya Martha Karua ya kuzindua chama cha People’s Liberation Party kilichobadilishwa jina kutoka Narc Kenya.

“Tulikuwa tu tunakunywa chai huku tukijiandaa kwa siku zijazo. Tutatoa kauli kuu Alhamisi wiki ijayo wakati wa uzinduzi rasmi wa chama kipya cha Martha Karua,” alisema Bw Wamalwa baada ya watatu hao kukutana katika hoteli moja jijini jana.

Kwa upande wao, Bw Gachagua na Bw Musyoka walikataa kutoa maelezo zaidi, wakishikilia walikutana kwa ‘kikombe cha chai’.

“Hakuna cha kusema leo. Tutazungumza wakati ufaao,” viongozi hao wawili walisema huku wakiondoka katika hoteli waliyokutana jana.

Hata hivyo, Taifa Leo limebaini kuwa mbunge huyo wa zamani wa Mathira ndiye aliyeitisha mkutano huo.

Bw Gachagua alikuwa wa kwanza kufika, dakika chache baada ya saa tano mchana, kabla ya kuketi kwenye kona faraghani mbali na macho ya wageni.

Mkutano huo ulijiri siku moja baada ya Naibu Rais Kithure Kindiki kuwashambulia vikali Bw Gachagua na Bw Musyoka akiwataja kama viongozi ‘waliofeli’ walipokuwa serikalini.

Viongozi hao wawili wamekuwa makamu na naibu rais wa Kenya kwa nyakati tofauti, huku Bw Gachagua akihudumu kama naibu wa rais hadi alipoondolewa ofisini mwaka jana, na Bw Musyoka akiwa makamu wa rais wa Rais Mwai Kibaki.

“Hakuna miradi ambayo Bw Kalonzo anaweza kusema alianzisha. Ana nini cha kuonyesha kwa wakati wake akiwa ofisini? Mtangulizi wangu alikuwa hapa kwa miaka miwili. Mafanikio yake makuu yalikuwa kugawanya Wakenya na kuendeleza ukabila,” alisema Bw Kindiki, huku akitaka eneo la Mlima Kenya lisidanganywe na wakosoaji wa serikali.

Bw Gachagua ameweka hadharani mpango unaoendelea wa kuunda muungano kumfanya Rais Ruto kuwa rais wa muhula mmoja.

Ameahidi kuzindua chama chake mwezi Mei na amekuwa akiwafikia viongozi wa kisiasa wenye nia moja waungane katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Ndani Dkt Fred Matiang’i pia yumo katika mpango wa upinzani, huku Rais wa zamani Uhuru Kenyatta akisemekana kuwa katika hali ngumu kuamua kumuunga waziri huyo wa zamani kumpinga Rais Ruto kupitia chama cha Jubilee au ajiunge na muungano huo unaotarajiwa.

Viongozi hao pia wamemchangamkia Seneta wa Busia Okiya Omtatah, ambaye pia alizindua azma yake ya urais mwezi uliopita, kujiunga na kundi lao.

Mwezi uliopita, viongozi hao watatu walikutana wakati wa uzinduzi wa makao makuu ya DAP-K jijini Nairobi, huku wito ukitolewa kuhimiza umoja ili kumng’oa Rais Ruto.

Dkt Matiang’i ambaye yuko nje ya nchi aliwakilishwa katika uzinduzi huo na Seneta wa Kisii Richard Onyonka, akiashiria nia yake ya kufanya kazi kwa karibu na muungano huo changa.

Viongozi hao wameungana katika kukemea Serikali Jumuishi, huku wakimkosoa vikali Rais Ruto.Wakati wa uzinduzi wa makao makuu ya DAP- K, Bw Gachagua alionyesha imani yake katika kumtimua Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027, akisema Dkt Ruto amepoteza angalau kura milioni nne Mlima Kenya.

“Sisi ni sehemu ya timu hii na tutatembea njia hii pamoja ili kuikomboa nchi hii. Tutajitolea kwa vyovyote ili kuhakikisha kuwa Ruto atakuwa rais wa muhula mmoja,” alisema Bw Gachagua.