Vinara wa upinzani wapigana chenga badala ya kujipanga
MPANGO wa upinzani wa kuwa na mgombeaji mmoja wa urais kumkabili Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2027 unaonekana kuyumba baada ya siku ya matukio ya kisiasa jana ambayo yalionyesha vinara wanapigana chenga.
Huku chama cha Rais Ruto, United Democratic Alliance (UDA), kikionyesha umoja na kusherehekea mafanikio yake jijini Nairobi, upinzani ulionyesha wazi wazi kutokuwepo kwa mpango imara wa kuungana.
Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta, pamoja na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i walihudhuria mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe wa Jubilee (NDC).
Wakati huo huo, Bi Martha Karua alikuwa pia jijini akitangaza nia yake ya kugombea urais kwenye mkutano wa Chama cha People’s Liberation Party (PLP), akiwa pamoja na Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka, Justin Muturi, Eugene Wamalwa na Mithika Linturi miongoni mwa viongozi wengine wa “upinzani ulioungana”.
Mikutano hiyo ilifanyika wakati mmoja, na kuashiria kuwa upinzani unapata ugumu wa kujenga muungano mmoja imara dhidi ya UDA ya Rais Ruto tofauti na taswira ambayo vinara wanaisawiri.
Japo Dkt Matiang’i alitarajiwa kutangazwa kuwa kinara wa Jubilee katika NDC, Bw Kenyatta aliibuka kama mtu anayetaka kurejesha hadhi yake akilaumu watu ambao hakuwataja kwa majina kwa kujaribu kumpokonya chama.
“Siku ya leo ni miaka mitatu tangu tufanye NDC yetu. Hili si kosa langu, ni kutokana na wale waliotaka kuchukua chama chetu kwa nguvu. Walitumwa kufanya hivyo,” alisema.
Alitafakari kuhusu siasa zake za miaka mingi zinazovuka miaka zaidi ya thelathini, akisema amepata ushindi na hata mapigo bila chuki.
“Kisiasa, hauwezi kuongozwa na ghadhabu. Nimepata mafanikio na kushindwa. Tukitazama nyuma, kuna mambo tunayoweza kujivunia na mengine tungeweza kuyafanya vizuri zaidi,” alisema.
“Kuanzia leo, tutaanza safari mpya. Katika wiki chache zijazo, tutashuhudia zoezi la kusajili. Milango iko wazi kwa wote,” alitangaza Kenyatta na kusema haondoki katika siasa.
Uwepo wa Matiangi katika NDC ya Jubilee uliwachanganya waangalizi, kwani Bw Gachagua na Bw Musyoka walikuwa katika mkutano wa Bi Karua wakati huo huo japo wanasisitiza upinzani umeungana.
Katika NDC ya chama chake, Bi Karua, alitoa tamko lake kubwa kabisa hadi sasa, akitangaza azma yake ya kugombea urais kwa tiketi ya PLP japo alisisitiza upinzani umeungana na utatoa mgombea urais mmoja kumenyana na Ruto.
“Tunahitaji kutembea pamoja kama upinzani ulioungana. Kila mmoja wetu atatangaza azma yake na kuijenga, lakini mwisho wa siku, tutapunguza matamanio yetu kwa maslahi ya Wakenya. Tutaketi pamoja na kuleta mgombea mmoja,” aliwaambia wajumbe.
Aliongeza: “Nitaongoza kwa muhula mmoja tu. Viongozi wanapofika madarakani wanakataa kuondoka. Katika miaka mitano, inawezekana kuweka msingi. Hakuna mtu atakayemaliza kazi ya kufanya Kenya kuwa na ustawi kamili.”
Kwamba mkutano wake ulivutia baadhi ya viongozi wakuu wa upinzani akiwemo Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka, Justin Muturi, Eugene Wamalwa na Mithika Linturi kunaonyesha kwamba upinzani bado unapigana chenga kabla ya kuamua iwapo utaungana 2027.Gachagua, Musyoka, Wamalwa na Matiang’i wametangaza azma zao za kugombea urais 2027.Bw Musyoka ameapa kwamba hataacha azima yake naye Bw Gachagua ametoa masharti makali kwa wanaotaka kuungwa mkono na wapiga kura wa Mlima Kenya akisema hatasita kugombea urais iwapo hakuna akayeyatimiza.
Chama cha Jubilee cha Kenyatta, pia kina ushawishi eneo la Mlima Kenya ambalo Gachagua na Karua wanatoka.
Bw Matiang’i ambaye anapigiwa upatu na Jubilee kupeperusha bendera pia ametangaza azma yake na jana, Katibu Mkuu wa chama hicho Jeremiah Kione alisema kiko katika muungano wa upinzani.
Wachanganuzi wa siasa wanasema matukio ya jana yazidisha hofu kwamba upinzani wa Kenya hauna njia wazi ya kusonga mbele.“Yamkini wanapimana nguvu au wanapangana wenyewe kwa wenyewe. Hii sio ishara nzuri kwa wafuasi wao. Pia, inaweza kuwa mipango yao ya kufanya upande wa serikali kutong’amua mwelekeo wao mapema, wajifanye wamegawanyika. Wanaweza kuwa hawaaminiani na ndio maana kila mmoja anajipanga kivyake kwa lolote,” alisema mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.
Hata hivyo anasema wanapaswa kupanga muungano wao mapema ili kujenga imani miongoni mwa wafuasi wao.