Viongozi saba vijana na jasiri walio mwiba kwa Ruto
UTAWALA wa Rais William Ruto umepata upinzani mkubwa kutoka kwa viongozi vijana ambao hawasiti kukosoa serikali.
Viongozi hao wanafuata nyayo za wabunge saba ambao walikuwa wakosoaji wakali wa utawala wa Kanu miaka ya themanini na tisini – James Orengo, Abuya, Koigi Wamwere, Mwachegu wa Mwachofi, Chibule wa Tsuma, Chelagat Mutai na Lawrence Sifuna.
Kwa sadfa, mmoja wa wanaokosesha Dkt Ruto usingizi ni seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, mpwa wa marehemu Lawrence Sifuna ambaye alikuwa mbunge wa Bungoma Kusini (kwa sasa Kanduyi).
Viongozi hao saba, wameibuka kuwa mwiba kwa Rais Ruto na kupendwa na wengi kwa kuwa hawaogopi kumkosoa moja kwa moja katika hafla tofauti au kupitia kauli zao kwa wanahabari na hata Bungeni.
Mapema wiki hii, mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya alimkabili Rais katika ziara yake ya Mumias na kumwambia kwamba nchi inaelekea pabaya.
”Heri niwe mshauri wako, kwa sababu, Bw Rais, wandani wako hawakuambii ukweli. Wanakudanganya kuhusu SHA (Bima ya Afya ya Jamii), nyumba za bei nafuu, na mfumo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu. Najua una nia ya kuwatumikia wananchi, lakini wanaokuzingira hawakwambii ukweli. Watu hawa wameweka makato makubwa kwenye mishahara ya Wakenya, na ndiyo maana watu wana uchungu na hasira nawe,” Bw Salasya alisema.
Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na mwenzake wa Busia Okiya Omtatah pia wameibuka kuwa viongozi jasiri wa kisiasa ambao wamedumisha ukosoaji mkali kwa utawala wa sasa.
Bw Omtatah ambaye ni mwanaharakati, hivi majuzi alizindua azma yake ya kuwania kiti cha urais 2027. Wabunge hao wawili wa upinzani wanaungana na takriban wengine wanne vijana kukabiliana na utawala wa Dkt Ruto.
Wabunge wa Kenya Kwanza wanaojizolea umaarufu mkubwa kutokana na mzozo kati ya Rais na Bw Gachagua ni Seneta wa Kiambu Karungo Thang’wa, Joe Nyutu (Murang’a) na John Methu (Nyandarua) ambao ni maseneta wa muhula wa kwanza.
Orodha hiyo inakamilishwa na Mbunge wa Gatanga Edward Muriu, aliyekuwa mshirika wa rais na ambaye sasa ni mkosoaji mkuu wa utawala wa Kenya Kwanza, na mbunge wa Kajiado Kaskazini, Onesmus Ngogoyo.
Lakini Kiongozi wa Wengi Bungeni Kimani Ichung’wah, ambaye ameibuka kuwa mtetezi mkuu wa Rais, hivi majuzi amemtaka Dkt Ruto kutowasikiza wakosoaji wake.
Alipuuzilia mbali wakosoaji hao, akimwambia Rais asitoe jasho kukabiliana nao, akisema kutoegemea upande wowote kutawazima wakosoaji.’Hao watu wa kelele, niachie mimi nipambane nao,’ akasema Bw Ichung’wah.
Nyutu, Ngogoyo na Muriu ni miongoni mwa wabunge wanaotaka kuundwa kwa tume ya uchunguzi kumulika visa vinavyoendelea vya utekaji nyara.
Ijumaa wiki jana, Seneta Nyutu alifichua kuwa Mlima Kenya unanuia kumsuta Rais na washirika wake kutoka eneo hilo, akisema wako tayari hata kujiuzulu na kuomba wachaguliwe kwa tiketi ya chama kipya.