Viongozi wa upinzani watishia kuanzisha IEBC ‘ya wananchi’
VIONGOZI wa upinzani wamekashifu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inayosubiri kuundwa walioteuliwa wakiidhinishwa na Bunge la Kitaifa.
Viongozi hao wameitaja tume hiyo kuwa ya Rais William Ruto na mshirika wake katika serikali jumuishi, Raila Odinga.
Wamekosoa mchakato na hata majina ya walioteuliwa mwenyekiti na makamishna wa IEBC, wakisema jopo la uteuzi pamoja na walioteuliwa wana uhusiano wa karibu na Rais Ruto na Bw Odinga huku baadhi yao wakishikilia nyadhifa mbalimbali serikalini.
Viongozi hao walitishia kuanzisha walichoita tume mbadala itakayofahamika kama ‘IEBC ya Wananchi’ ambayo itakuwa kama chombo cha uangalizi wa tume rasmi, kuhakikisha kuwa inazingatia viwango vya juu vya uwazi, uadilifu na Katiba.
“Tunachukua hatua za haraka kuanzisha IEBC ya Wananchi – chombo kinachoongozwa na raia kitakachoipiga darubini tume rasmi na kuishinikiza kutekeleza uwazi, uadilifu, na maadili ya kikatiba kama ilivyobainishwa katika Ibara ya 10 kuhusu maadili ya kitaifa na misingi ya utawala bora,” walisema katika taarifa.
Katika taarifa ya pamoja Jumanne, viongozi wa upinzani, Bw Kalonzo Musyoka, Bi Martha Karua, Dkt Fred Matiang’i, Bw Eugene Wamalwa, Bw Rigathi Gachagua na Dkt Mukhisa Kituyi, Bw Justin Muturi na Bw Torome Saitoti, walidai Mwenyekiti mteule wa IEBC, Bw Erastus Edung, ana uhusiano wa karibu na Ikulu kupitia kwa Msimamizi wa Ikulu, Bw Josphat Nanok.
“Erastus Edung, mteule wa kiti cha Mwenyekiti, anajulikana kuwa mwaminifu kwa Ruto na ana uhusiano wa karibu na Ikulu kupitia Josphat Nanok. Rekodi yake ya utendakazi katika Kaunti ya Turkana kama Mwanasheria wa Kaunti imejaa dosari,” ilisema taarifa hiyo.
Walidai kuwa Bw Hassan Noor aliyeteuliwa mmoja wa makamisha sita ni jamaa wa Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohammed, na uteuzi wake ulitokana na ushawishi wa Bw Junet wa kuongeza muda wa jopo la uteuzi.
Katika taarifa yao ya pamoja, viongozi hao wa upinzani walidai kuwa Bi Joy Midivo, mmoja wa walioorodheshwa kuhojiwa, ni afisa wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), huku Bw Charles Nyachae akitajwa kama mshirika wa muda mrefu wa Rais Ruto.
Pia, kwa mujibu wa upinzani, Prof Adams Aloo, aliyekuwa mwanachama wa jopo la uteuzi, pia ni mshauri wa mawasiliano wa kimkakati wa Rais.
Prof Oloo aliwahi kusema alikataa wadhifa wa ushauri alipoteuliwa kuhudumu katika jopo hilo.
Kwa mujibu wa viongozi hao, mchakato wa uteuzi wa kamati mpya ya IEBC uliathiriwa na ukiukaji wa misingi ya usawa na ni njama ya Rais Ruto na Bw Odinga, ya kupanga wizi wa kura katika uchaguzi mkuu wa 2027.
“Kuanzia mwanzo, mchakato wa uajiri ulikuwa na dosari. Jopo la uteuzi lilikuwa ni sehemu ya Ikulu, lililojaa wafuasi wa Ruto na washauri wake wa ndani,” taarifa ilisema.
“Kanuni za kikatiba za mashauriano, ushiriki wa umma, na kutopendelea kisiasa zilipuuzwa kabisa. Matokeo? Tume isiyo na uadilifu, uhalali, wala imani ya umma,” waliongeza.
“Katiba iko wazi. Ibara ya 88(2) inahitaji IEBC kuwa huru, isiyoegemea upande wowote, na isiyopendelea kisiasa. Kile ambacho Ruto ameunda ni mashine yake ya kisiasa kwa kisingizio cha tume ya uchaguzi,” walisema.
Mnamo Alhamisi, wiki jana, Rais alimteua Bw Edung kutoka Kaunti ya Turkana kuwa Mwenyekiti wa IEBC, pamoja na watu wengine sita kuwa makamishna wa tume hiyo, kufuatia mapendekezo ya jopo la uteuzi lililoongozwa na Dkt Nelson Makanda.
Wengine walioteuliwa ni Bi Ann Njeri Nderitu, Dkt Moses Alutalala Mukhwana, Bi Mary Karen Sorobit, Bw Hassan Noor Hassan, Prof Francis Odhiambo Aduol na Bi Fahima Araphat Abdallah.
Rais alituma majina hayo kwa Bunge la Kitaifa kuidhinishwa.